Na Mwandishi Wetu, Dar es Salam
MEYA wa Ilala, Jerry Silaa, amekabidhi magari kwa washindi saba wa promosheni ya Airtel Yatosha promosheni inayoendeshwa na Kampuni ya Simu ya Airtel kwa wateja wa bando za Yatosha Zaidi.
Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana na washindi hao waliotangazwa wiki iliyopita kukabidhiwa magari yao mapya aina ya Toyota IST.
Washindi hao ni mamalishe mkazi wa Dar es Salaam, Sakina Mshamu Libwana, mganga wa tiba asilia kutoka Katavi Said Mashiko, utingo wa mabasi mkazi wa Tabata Justin William, Edson Mwansasu (mkulima wa Kyela), Hamim Yoyo (mfanyakazi wa saluni, Korogwe, Tanga) na Ester Mashauri, muuguzi wa Hospitali ya Bugando, Mwanza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Silaa alisema. “Ninafarijika sana kuona Watanzania kutoka kanda mbalimbali wakiibuka washindi wa promosheni hii. Hii inaonyesha ni namna gani Airtel wamejipanga kuboresha maisha ya Mtanzania mmoja mmoja.
“Kingine kilichonifariji kwa leo ni kuona miongoni mwa washindi, wapo pia wakazi wa Manispaa ya Ilala ambako mimi ni meya wao. Lakini, pongezi zangu ni kwa washindi wote nikiwaomba wasiache kutumia huduma za Airtel wao na jamaa zao,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Sunil Colaso, alisema. “Kwa jinsi zawadi hizo zilivyosambaa nchini ni alama ya kuenea kwa uhakika kwa mtandao na huduma za Airtel Tanzania. Kwa magari haya 10 tu ya mwanzo, tayari tumepata washindi kutoka kila kona ya nchi, hii inafurahisha sana,” alisema.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Airtel, Jackson Mmbando, aliwataka wateja wa Airtel waendelee kujiunga na huduma ya Airtel Yatosha Zaidi na pia kutozima simu zao za mkononi au kusita kupokea hasa kwa siku za Ijumaa ya kila wiki ambapo droo hiyo huchezeshwa.