BARCELONA, HISPANIA
UONGOZI wa klabu ya Barcelona umepanga kukaa mezani na nyota wa klabu hiyo, Lionel Messi, mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa El Clasico dhidi ya Real Madrid.
Mchezo huo wa wababe wa nchini Hispania unatarajiwa kupigwa mwishoni mwa wiki ijayo katika uwanja wa Camp Nou.
Barcelona kwa sasa ipo katika mvutano na klabu ya Manchester City, ambayo inanolewa na kocha wa zamani wa klabu hiyo, Pep Guardiola, ambapo klabu hiyo ya nchini England imedai kuwa ipo tayari kuweka mezani kitita cha pauni milioni 200 na mshahara wa pauni 500,000 kwa ajili ya kumsajili mchezaji huyo.
Kwa kuliona hilo, Barcelona wamepanga kutaka kumalizana na mchezaji huyo kwa kumpa mkataba wa maisha ndani ya klabu hiyo, mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa wiki ijayo.
Mkataba wa mchezaji huyo ndani ya klabu ya Barcelona unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao mwaka 2018, lakini Barcelona wanaamini wasipomalizana na mchezaji huyo mapema, wanaweza kumkosa.
Rais wa klabu hiyo, Josep Bartomeu, tayari amefanya mazungumzo na baba wa mchezaji huyo, Jorge, ambaye pia ni wakala wa mchezaji huyo na tayari wamekubaliana hatua za awali.
Hata hivyo, wiki iliyopita mchezaji huyo alifanya mazungumzo na kampuni ya kutengeneza vifaa vya michezo, Adidas, na kuwaambia kwamba hana mpango wa kuondoka ndani ya klabu hiyo.
“Hakuna kitu kama hicho, nipo katika klabu bora duniani ambayo ina wachezaji wenye uwezo mkubwa, siku zote imekuwa ikifanya vizuri bila kumtegemea mchezaji mmoja, sifikirii suala la kuhama,” alisema Messi.
Hadi sasa mchezaji huyo amecheza jumla ya michezo 550 na kufunga mabao 475, huku akichukua mataji 29 na Ballon d’Or mara 5.