24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Fidel Castro Jabali la mapinduzi limeondoka

Fidel Castro
Fidel Castro

HAVANNA, CUBA

KWAHERI Fidel Castro. Ama wasemavyo wananchi wa Cuba, ‘Hasta la vista’, yaani kwaheri ya kuonana ama kwaheri pale wanapoagana au kutenganishwa na mtu wao muhimu maishani.

Hivyo ndiyo kauli pekee inayofaa kutumika baada ya kiongozi mashuhuri, mwanamapinduzi, aliyekuwa Rais wa Cuba, Fidel Castro,  kufariki  dunia  akiwa  na  umri  wa miaka 90 usiku wa kuamkia jana.

Taarifa ya kifo cha mwanamapinduzi  huyo ilitolewa na ndugu  yake,  Rais Raul  Castro, kwenye  Televisheni  ya Taifa, ambapo alisema; “Ndugu wananchi wa Taifa la Cuba,  marafiki wa Amerika yetu na  dunia  nzima, ninayo majonzi mazito, kuwapa  taarifa hii, kwamba  leo Novemba 25 (juzi) Kamanda  Mkuu wa Mapinduzi  ya Cuba, Fidel Castro Ruz  amefariki  dunia.”

Fidel  Castro  aliiongoza  Cuba kupitia chama cha Kikomunisti, baada  ya kufanikisha mapinduzi yaliyoung’oa  utawala  wa  dikteta wa  Fulgencio  Batista mwaka 1959. Hatua alizochukua ikiwa pamoja  na  kuleta mageuzi katika sera  ya  ardhi  na  kutaifisha viwanda na  makampuni, zilisababisha uadui  kati yake  na  Marekani.

Marekani ilijibu kwa kuiwekea Cuba  vikwazo vya  kibiashara.  Hata  hivyo,  Cuba  ilipata misaada  mikubwa  kutoka Umoja  wa Kisoviet na hivyo  kuwa tegemezi wakati  wote.

Kisiwa cha Cuba kiliingia katika kipindi kigumu sana cha matatizo ya kiuchumi  baada ya Umoja  wa Kisovieti (USSR) kusambaratika mnamo mwaka 1990. Hata hivyo, mfumo wake wa kikomunisti uliweza kukihimili kipindi hicho hadi hivi karibuni ambapo Cuba na Marekani zilirejesha uhusiano wa kibalozi baina yao.

Fidel Castro amefariki huku akiacha kumbukumbu nyingi nzito ya mapambano dhidi ya ubepari, umasikini na uonevu kwa jamii ya watu masikini. Anakumbukwa kama mtu aliyeweza kudumisha uhusiano mzuri na viongozi waliokuwa wakifuata itikadi na misimamo yake. Mathalani Julius Nyerere, Hugo Chavez na Nicholas Maduro (Venezuela), Mikhael Gorbachev (Urusi) kwa kuwataja wachache.

Fidel Castro alikuwa mzalendo aliyeongoza Cuba kwa takribani miaka 50 na kuwa kiongozi wa tatu aliyekaa muda mrefu madarakani, toka mwaka 1959 hadi 2008 alipokabidhi uongozi kwa mdogo wake, Raul Castro.

Kifo cha rais huyo kimekuja ikiwa ni mwezi mmoja baada ya Chama tawala cha Kikomunisti kubashiri mwisho wa uhai wake hapa duniani.

Akizungumzia kifo hicho, rais wa zamani wa Urusi, Mikhail Gorbachev, amemsifu Fidel Castro kwa kuimarisha hali ya usalama na maslahi ya wananchi wa Cuba wakati wa uongozi wake.

“Fidel alikuwa imara, aliimarisha nchi yake katika kipindi kigumu cha vikwazo wavyowekewa na Marekani, hata wakati aliopewa shinikizo dhidi ya nchi yake, alisimama imara kuilinda kwa kila hali na kusisitiza uhuru wa maendeleo,” alisema Gorbachev.

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, alimwelezea Fidel Castro kama alama ya watu bora katika karne ya 20. “India inakiri kumpoteza kiongozi rafiki. Ninatoa pole kwa serikali na wananchi wote wa Cuba kwa huzuni waliyonayo kumpoteza kipenzi chao Fidel Castro. Alale mahali pema,” alisema Waziri Modi.

Naye Rais wa Mexico, Enrique Pena Nieto alisema, “Fidel Castro alikuwa rafiki bora wa Mexico, mhamasishaji mwenye heshima, mpenda majadiliano na mzalendo kwa nchi yake.”

Salvador Sanchez Ceren, Rais wa El Salvador, alisema, “Kwa huzuni kubwa niliyonayo, baada ya kupokea taarifa za kifo cha Fidel, ninawapa pole makamanda wote kwa kumpoteza Kamanda Fidel Castro.”

Hali ya Fidel Castro ilibadilika zaidi miaka minne iliyopita, baada ya kushindwa hata kujua maumivu ya kichwa ni kitu gani. Castro hakuonekana hadharani, alikuwa mtu adimu hata pale alipohitajika. Mapema Agosti mwaka huu alionana na Rais wa China, Xi Jinping na Vladimir Putin wakati akiadhimisha sherehe ya miaka 90 ya kuzaliwa kwake.

FIDEL CASTRO MKOSOAJI

Licha ya kuwa kiongozi wa taifa na hata alipostaafu, alipenda kuandika mawazo yake na alikuwa na safu yake maalumu katika magazeti ya Serikali ya Cuba. Katika kipindi hicho cha umri mkubwa bado alibaki kuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Barrack Obama wa Marekani kupitia safu yake gazetini.

Mei mwaka huu, Castro amewahi kumshutumu Obama kutembelea mji wa Hiroshima, akidai kiongozi huyo alishindwa kutamka maneno ya kuomba radhi dhidi ya mauaji yaliyofanywa na majeshi ya Marekani katika mji huo uliopo nchini Japan.

Katika safu yake hiyo Machi mwaka huu, Castro alimtuhumu Obama kuzungumza lugha laini na tamu kwa wananchi wa Cuba alipokuwa ziarani na kusahau kupongeza kazi nzito iliyofanywa na chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo.

Baada ya kushuhudia mahusiano mapya ya kidiplomasia kati ya Cuba na Marekani mnamo Desemba 17, 2014 kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1961, Fidel Castro alibariki mpango huo wa kihistoria uliowakalisha chini maadui na kupata mwafaka. Akiandika katika safu yake gazetini alisema; “Sina imani na sera za Marekani, hata nikizungumza nao mara nyingi, lakini hiyo haina maana kuwa napinga suluhisho la mgogoro uliopo.”

UHASAMA WAKE NA MAREKANI

Katika uongozi wake alifanikiwa kuondoa ushawishi wa Marekani nchini mwake, alimudu kuleta huduma za afya za bure na kuboresha elimu.

Kisiwa cha Cuba, kilicho maili 90 kutoka jimbo la Florida la Marekani, kilikumbwa na uvamizi wa kijeshi uliojulikana kama Bay of Pigs, kutokana na mpango wa Castro wa kutengeneza silaha za kikemikali ambazo zilitambulika duniani na kuibua vita dhidi ya silaha za nyukilia.

Ugomvi wake mkubwa na Marekani ulitokana na suala la sera. Castro aliamini katika sera za ujamaa na baadaye ukomunisti. Lakini utawala wa Marekani ulitarajia baada ya Castro kuingia madarakani angeleta utawala wa kidemokrasia kuliko Rais Batista, hali haikuwa hivyo, Castro akatangaza kuendesha sera za kisoshalisti.

Kutokana na misimamo yake ya kujiunga kambi ya Kisoviet, Serikali ya Marekani ilianza mikakati ya kumng’oa madarakani. Marekani ilianza kuacha kununua sukari ya Cuba, hali ambayo iliyumbisha uchumi wa Cuba. Aidha, mwaka 1961 Marekani iliweka vikwazo vya kibiashara na kidiplomasia dhidi ya utawala wa Cuba, isipokuwa kwenye maeneo ya chakula na madawa. Aprili 16, mwaka huo huo Castro akatangaza mapinduzi ya kisoshalisti.

Kufuatia hatua hiyo, shirika la kijasusi la CIA liliwachukua wafungwa 1,400 wa Cuba waliokuwapo nchini Marekani na kuwapa mafunzo ya kivita ili kumwangusha Castro. Mafunzo hayo ndiyo yalikuja kuibuliwa katika vita ya Bay of Pigs ambapo Marekani ikiwa chini ya Rais John F. Kennedy ilishindwa vibaya na kusababisha aibu kimataifa. Maadui wa Castro wote walikimbilia Marekani, ambako walipatiwa hifadhi ya kisiasa na wakatumiwa kumwangusha Castro bila mafanikio.

Hadi kifo chake kilipotokea Novemba 25 mwaka huu, Fidel Castro alijaribiwa kuuawa mara 630 na askari wa zamani wa Cuba waliokuwa uhamishoni, kwa msaada na Serikali ya Marekani. Uhasama wa Cuba na Marekani ulishamiri baada ya ujenzi wa kinu cha nyukilia uliofadhiliwa na serikali ya Urusi kabla ya kuondolewa na Nikita Krushchev. Tangu wakati huo Marekani ilikuwa ikiitaja Cuba kama mhimili wa uovu na kwamba ilifadhili vikundi vya kigaidi kabla ya kubadilisha kauli miaka miwili iliyopita na kuwa nchi ‘marafiki’.

UASI WA FIDEL CASTRO

Kiongozi huyo alifanikiwa kuvunja minyororo ya kuwa mfungwa wa kisiasa huko Mexico kipindi ambacho Cuba ilikuwa ikitawaliwa na dikteta Fulgencio Batista. Harakati za uasi alianza nazo huko Mexico kabla ya kuizingira Havana Januari mwaka 1959, na baadaye kuwa kiongozi kijana zaidi kuliko wote katika nchi za Latini Amerika aliposhika madaraka akiwa na miaka 32.

Kwa kipindi chote cha utawala wake aliunga mkono na kusaidia makundi mbalimbali ya kipiganaji katika nchi za Amerika kusini na Afrika. Aliziunga mkono China na Vietnam kwasababu tu zilikuwa mkondo mmoja na mitazamo yake ya uongozi.

Maisha yake ya uasi yalianza mwaka 1953, katika shambulizi dhidi ya kambi ya jeshi ya Moncada iliyopo jijini Santiago. Katika shambulizi hilo, makamanda wengi wa jeshi waliuliwa, hivyo Fidel na Raul wakiwa miongoni mwa walioshambulia walifungwa jela.

Hata hivyo, Castro aliondoka Mexico baada ya kupewa amri ya kutoonekana nchini humo kutokana na vitendo vyake vya uasi. Baadaye alirudi kwenye uasi mwaka 1956 kupitia ghuba moja ya Mexico iliyoitwa Granma, ambayo ilitumika kama kambi yao ya kikosi chao.

Katika kipindi chake cha uasi alisaidiwa kwa kiasi kikubwa na Raul Castro pamoja na bingwa wa vita vya misituni, Ernesto Che Guevarra, ambapo walianzisha maasi yao katika milima ya Sierra Maestra.

Miaka mitatu baadaye, mnamo Januari 8, 1959 maelfu ya wananchi wa Cuba waliingia mitaani jijini Havana kushangilia kuanguka utawala wa Dikteta Batista, kutokana na kushambuliwa na vikosi vilivyoongozwa na Fidel Castro. Mara baada ya kuingia madarakani alifungia vyombo vya habari binafsi na kuwateketeza viongozi 582 wa serikali ya Batista.

Mwaka 1964 alifunga jela watu 15,000, hali ambayo ilisababisha maelfu ya wananchi kuikimbia nchi hiyo, akiwemo binti yake, Alina Fernandez Revuelta na dada yake Juana Castro.

ASALITIWA NA DADA YAKE

Wakati wa uongozi wake alimwamini mno Raul Castro, ambaye ni mdogo wake kwa kuzaliwa. Mojawapo ya mambo ya kukumbukwa katika uongozi wa Fidel Castro nchini Cuba ni kitendo cha dada yake, Juana Castro kumsaliti kwa makachero wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA).

Hadi sasa Juana Castro anaishi uhamishoni huko Florida, Marekani, na amekuwa adui mkubwa wa kaka yake huku ndugu hao wakishindwa kuzungumza kabisa kwa miongo minne, sawa na miaka 40. Juana Castro alimtuhumu Fidel kuwa ni ‘zimwi’.

MAISHA NA FAMILIA YAKE

Mtoto wake wa kwanza wa kiume, Fidelito Castro ni mwanasayansi mahiri na mmoja wa wataalamu wa nyukilia nchini Cuba. Alimpata mtoto huyo alipokuwa na mkewe, Mirta Diaz Balart, ambaye aliachana naye mwaka 1956.

Mnamo mwaka 1980 alioana kimya kimya na Dalia Soto del Valle, ambapo walifanikiwa kupata watoto watano wa kiume. Pia anadaiwa kuwa na mamia ya wanawake aliohusiana nao kimapenzi wakati wa uhai wake.

Binti yake, Alina Fernandez, alimshambulia baba yake huyo kupitia redio akiwa uhamishoni jijini Miami, Marekani.

Fidel Castro alizaliwa Agosti 13, 1926 kwa baba mhamiaji wa Kihispania aliyeingia Cuba kama kibarua katika moja ya kampuni za sukari zilizomilikiwa na Marekani. Baba yake aliachana na kibarua hicho na kuanzisha mashamba yake ya Miwa nchini humo.

Fidel Castro alisoma shule za Shirika la Jesuit, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Havana alikosomea shahada ya sheria na sayansi ya jamii.
RAIS MIGUEL DIAZ-CANEL 

Raul Castro amekuwa bega kwa bega na Fidel Castro katika maisha yao ya ujana, uasi na uongozi. Wamepitia misukosuko mingi kabla ya kushika hatamu ya uongozi. Mwaka 2013 Raul Castro alitangaza kuwa atastaafu urais wa Cuba ifikapo mwaka 2018 na nafasi yake itachukuliwa na Miguel Diaz-Canel. Kwa sasa Migeul ndiye makamu wa rais.

MATUKIO MUHIMU

 

Januari 1, 1959: Waasi wakiongozwa na Fidel Castro walichukua madaraka nchini Cuba. Upesi Serikali ya Marekani inamuunga mkono Fidel Castro kabla ya uhusiano kuvunjika.

 

Oktoba 1960: Serikali ya Marekani inatangaza kuweka vikwazo dhidi ya biashara ya sukari ya Cuba. Na Januari 1961 inatangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia. Miezi mitatu baadaye Cuba inatangazwa kuwa nchi ya kijamaa.

 

Oktoba 1962: Serikali ya Marekani yatoa tishio kwa Serikali ya Urusi kuondoa mpango wake wa ujenzi wa kinu cha nyukilia nchini Cuba.  Tishio hilo lilitolewa na Rais Kennedy ambapo Marekani ilikuwa tayari kuivamia Cuba kabla ya kufuta mpango huo.

 

Mei 22, 1977: Fidel Castro anakutana na Rais wa Tanzania, Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.

 

1977:  Rais wa Marekani, Jimmy Carter baada ya kuingia madarakani alijaribu kulegeza msimamo mkali wa nchi yake dhidi ya Cuba. Wakati huo Cuba ilielekeza nguvu zake za kuchangia maendeleo kwa nchi za Afrika.

NUKUU ZA FIDEL CASTRO

Mwaka 1953: “Mnaniulaumu mimi? Hakuna chochote muhimu kwangu. Nadhani historia itaamua kuhusu mimi.”

Mwaka 1959: “Nilianza mapinduzi nikiwa na wapiganaji 82 tu. Kama ningeambiwa nifanye tena mapinduzi basi ningechukua wapiganaji 10 au 15 wenye uaminifu. Haijalishi ni kiasi kidogo ulichonacho bali imani na mipango uliyonayo.”

Mwaka 1985: “Nimefika hitimisho muda mrefu uliopita, kitu ninachotakiwa kujitoa sadaka ni kuacha kuvuta sigara ili kulinda afya ya wananchi wa Cuba, toka niache wala sina hisia za kutamani tena kuvuta.”

Mwaka 2006: Januari 21 katika sherehe za kuzaliwa kwake:

“Nina furaha nimefikisha miaka 80. Sikutarajia kitu kama hiki, wala majirani zangu. Watu wenye nguvu duniani wamejaribu kuniua kila mara lakini hawakufanikiwa.”

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles