BERLIN, UJERUMANI
KANSELA wa Ujerumani Angela Merkel ameahidi kuongeza hatua za Serikali yake katika kusaidia sekta binafsi barani Afrika dhidi ya misukosuko ya kisiasa na utaratibu wa malipo usio wa kawaida.
Alitoa ahadi hiyo alipokutana na wafanyabiashara na marais 12 wa Afrika katika mkutano wa kilele mjini hapa unaonuia kuongeza uwekezaji binafsi barani Afrika.
Merkel alisema fedha za maendeleo zitakazotolewa zinapaswa kusaidia uwekezaji wa kampuni ndogo na kiwango cha kati ya barani Ulaya na Afrika kupitia hisa na mikopo.
“Tunataka kutoa ishara bayana, tunapendelea ushirikiano mwema na wenye faida wa ujirani mwema kati ya Afrika na Ulaya. Sisi ni majirani, washirika, na sisi wa Ulaya tuna masilahi makubwa zaidi kuona Afrika yenye nguvu na matumaini mema ya kiuchumi.
“Na hilo kulifikia panahitajika si tu vitega uchumi vya Serikali bali zaidi kuliko vyote vya binafsi,” alisema Merkel.
Lengo hasa la mkutano huu wa kilele ni kutoa nafasi nzuri za ajira kwa Waafrika, kupunguza umasikini ambao pamoja na misukosuko ya kisiasa na vurugu ndiyo mambo yanayosababisha idadi kubwa ya Waafrika kukimbilia barani Ulaya.