Elizabeth Hombo na Shabani Matutu, Dar es Salaam
SIKU moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi kuwa ni miongoni mwa viongozi waadilifu, baadhi ya wasomi na wanasiasa wamesema kauli hiyo ni ya kutetea mtandao wa kifisadi.
Baadhi ya wasomi wametilia shaka uadilifu wa Membe kujitokeza hadharani kumsafisha Maswi ambaye jina lake limetajwa katika kashfa ya Akaunti ya Escrow kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC).
Membe alitoa kauli ya kumsafisha Maswi juzi wakati akihutubia mkutano wa Kanisa la Waadventista Wasabato uliofanyika katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam juzi ambapo alimtaja Maswi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira kuwa ni miongoni mwa viongozi waadilifu wanaotoka katika kanisa hilo.
Akizungumzia kauli hiyo ya Membe, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema ni dhahiri kwamba kiongozi huyo wa serikali anatetea mtandao wa kifisadi.
“Tuna tatizo kwa upande wa serikali, rais pia ni tatizo katika hili kwa sababu alieleza hadharani kuwa zile fedha za Tegeta Escrow si za umma wakati ripoti ya CAG na PAC imetueleza kuwa fedha zile ni za umma.
“Sasa huyu Membe inakuwaje anakuja na kueleza Maswi ni mwadilifu hapa lazima anatetea mtandao wa kifisadi, “alisema Profesa Lipumba.
KITILA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo alieleza kushangazwa na kuhoji kauli hiyo kutolewa na kiongozi huyo wa serikali.
“Iliundwa kamati ya serikali ya kumchunguza Maswi, sasa katika hili lazima tuhoji Membe ametoa kauli hiyo kama sehemu ya serikali au ni ya kwake…je ile kamati inafanyakazi gani kama yeye anakuja kutueleza kuwa mtu aliyetuhumiwa ni mwadilifu,” alisema Profesa Kitila.
LISSU
Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu yeye alieleza kuwa anatilia shaka uadilifu wa Membe kutokana na matamshi yake yanayolenga kumsafisha Maswi.
“Anabishana na uchunguzi wa CAG na PAC Maswi anayetajwa kushiriki katika uchotwaji wa fedha hizo hatujajua alichukua ngapi anamtetea, basi napata shaka na uadilifu wa Membe,” alisema.
DK. BANA
Akizungumzia kauli hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana alitoa wito kwa viongozi wakubwa kuwa makini na kauli zao wanazozitoa kwa kupima eneo na wakati wanapozitoa ili kuondoa tafsiri hasi zitakazotolewa na umma.
“Kwa sasa Maswi bado ni mtuhumiwa kutokana na ukweli kwamba Mahakama ndicho chombo chenye uwezo wa kumtia mtu hatiani au kumuondolea hatia, haimaanishi kwamba kauli ya waziri haikustahili kutolewa katika kipindi hiki na badala yake angekwepa hilo na kuzungumzia masuala mengine ambayo yasingetoa tafsiri,” alisema.
Kauli hiyo ya Membe inakuja wakati Serikali ikiwa imemsimamisha kazi Maswi, Desemba 23 mwaka jana ili kupisha uchunguzi dhidi yake na utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge kuhusu kashfa ya uchotwaji wa miamala ya zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Jana baadhi ya vyombo vya habari vilimkariri Membe kwa kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara Nishati na Madini aliyesimamishwa Eliakim Maswi na kusema kuwa ni kiongozi mwadilifu jambo ambalo limeibuka maswali.