NA AGATHA CHARLES,
MKE wa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, Melania (46) anaingia Ikulu baada ya mumewe kushinda urais wa Marekani kwa kura 276 za wawakilishi wa majimbo dhidi ya Hillary Clinton 218.
Melania anakuwa ‘first lady’ akiwa na sifa za kipekee tofauti na watangulizi wake akiwemo Michelle Obama ambaye mumewe anamaliza muda wake.
Wachambuzi wa masuala ya mitindo wanamwona Melania kuwa ana nafasi ya kufanya vyema katika mitindo, akiwa ni ‘first lady’ kwa kuwa aliwahi kuwa mwanamitindo.
Wapo pia ambao wanakwenda mbali zaidi na kumwona kuwa ‘first lady’ huyo anaweza kumpiku Michelle katika suala zima la mwonekano wa mavazi yaliyobuniwa kwa uwezo wa hali ya juu.
Tofauti ya Melania na Michelle ambao wote wanapenda mavazi ya kisasa, ni kwamba mwanamama huyo anapenda zaidi rangi zilizotulia kama nyekundu, nyeupe au nyeusi, huku Michelle akionekana kupenda rangi mchanganyiko na wote wanapenda zaidi wabunifu kutoka Marekani.
Wote wawili wanapovaa baadhi ya nguo zao huvuta macho ya watu kutokana na namna zinavyobuniwa.
Usiyoyajua mengine kwa Melania ni kwamba ni fist lady’ wa kwanza kuolewa mke wa tatu ambaye alifunga ndoa na Trump mwaka 2005 ambako kabla yake alikuwepo Marla Maples aliyekuwa mtangazaji na mama wa Tiffany  aliyeolewa mwaka 1990.
Katika mitandao mbalimbali ikiwemo Daily na USA today inamwelezea Melania na Trump kuwa walikutana wakati mfanyabiashara huyo akiwa na mkewe wa kwanza, Czechoslovakian Ivana Zelnickova ambaye wana watoto watatu Ivanka, Eric na kaka yao Donald Trump Jr ambaye ana miaka 38, akiwa na tofauti ya miaka nane na mama yake wa kambo Melania.
Jambo jingine ni kwamba harusi ya Trump na Melania wakati huo ilihudhuriwa na Bill Clinton na Hillary ambao walikuwa miongoni mwa wageni 350.
Melania ambaye ni ‘first lady’ wa kwanza kuzaliwa nchi ya Kikomunisti huko Yugoslavia, ni wa pili pia kutoka ng’ambo baada ya Louisa Adams ambaye alikuwa mke wa rais wa sita John Quincy. Melania anazungumza lugha tano ikiwemo Kislovenia, Kiingereza, Kifaransa, Kisebia na Kijerumani.
Pamoja na sifa hizo, Melania anakuwa ni ‘first lady’ pekee aliyewahi kupiga picha za uchi katika kazi yake ya mitindo, ikiwa ni miaka mitatu kabla hajakutana na Trump.
Katika malezi, Melania anamlea mwanaye Barron kama Donald mdogo ambaye anatoa maamuzi hata ya kuwafukuza wafanyakazi.
Pamoja na hayo, yuko bega kwa bega na mumewe kuhusu suala la wakimbizi kuondolewa Marekani.