23.4 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

Itachukua miongo sita kumpata Sitta II

samuel-sitta
Samuel Sitta

 

JIMMY CHARLES,

NI jambo la kawaida kwa binadamu kumwagiwa sifa kedekede pale anapohitimisha safari yake ya mwisho duniani.

Pamoja na mambo mengine, mara nyingi sifa amwagiwazo hazitofautiani sana. Nyingi ni zile za marehemu alikuwa mwema, alikuwa mkarimu na mwenye upendo wa hali ya juu na nyingine zinazofanana na hizo.

Bahati mbaya hali ni tofauti kwa Samuel Sitta, mwanasiasa, kiongozi, mzazi na mwanaharakati. Sita amefariki dunia alfajiri ya Jumatatu ya wiki hii, nchini Ujerumani, akiwa katika harakati za kupigania uhai wake.

Amefariki akiwa na utayari wa kukabiliana na kifo. Alijiandaa kuhitimisha safari yake ya mwisho duniani kwa amani na utulivu. Ukweli wa maandalizi hayo uliwekwa bayana na mwanawe, Benjamin, ambaye aliuambia umma kuwa dakika chache kabla ya baba yake kupumua pumzi yake ya mwisho, alisema neno fupi tu: ‘That is life’.

Alilisema hilo baada ya kuambiwa waziwazi kuwa ugonjwa wa tezi dume uliokuwa ukimtesa hauponi, naye kwa kujua wazi kauli ya kutopona inaashiria kifo, alikikubali.

Huo ni ujasiri wa hali ya juu unaonilazimisha nimtenganishe na wanasiasa wengi wa kizazi chake.

Sitta, Spika wa Bunge la Tisa, Bunge lililorejesha heshima, hadhi na maana ya mhimili unaojitegemea, hatutamwona tena, zaidi tutasalia na kumbukumbu ya historia yake iliyotukuka.

Nenda Sitta, tangulia Mzee wa Kasi na Viwango, umeacha alama ya mafanikio katika siasa na uongozi. Usiache kumweleza Mwalimu Julius Nyerere hali ya mambo ilivyo nchini.

Ikiwezekana mkumbushe namna alivyokuchapa viboko ulipokuwa ukipigania haki za wanafunzi pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Ndiyo. Ulichapwa, inawezekana ulichapwa kwa haki au kwa kuonewa, lakini Mwalimu alikuadhibu.

Hivyo ndivyo ilivyo, alikuwa na makosa kama binadamu wengine, hakuwa mkamilifu kwa sababu aliishi katika dunia hii ya mchwa, mende  na kizazi cha panya kinachong’ata na kupuliza.

Hata hivyo, ukweli unasalia pale pale, mazuri yake ni mengi kuliko mabaya. Na hapo ndipo ninapopata jeuri ya kufikiri bila haya kuwa itachukua miongo sita kumpata Sitta II.

Kwanini nafikiri hivyo? Nafikiri hivyo kwa sababu kadha wa kadha, zikiwemo za kupambana bila kuchoka katika kusaka haki na harakati zake za kisiasa.

Mapambano, Sitta anatajwa kuwa mpambanaji na mtu asiyechoka wala kuona haya katika kudai haki yake. Alikuwa hivyo kabla na hata baada ya kujiingiza kwenye siasa.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, mwaka 1966 akiwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliongoza mgomo na maandamano ya wanafunzi wa chuo hicho wakipinga baadhi ya mambo ambayo kwa wakati huo hayakuwa na tija kwa wanafunzi.

Wanafunzi, wakiongozwa na Sitta, walihoji sababu ya vigogo wa Serikali kulipwa mishahara na marupurupu makubwa. Lakini pia alionyesha kutetea haki za wakulima na wafanyakazi.

Bila hofu, Sitta akiwa na wenzake walithubutu kumwambia Mwalimu kuwa ni heri wakati wa ukoloni kuliko utawala wake.

Wanafunzi wote 400 walirudishwa makwao ili kwenda kufunzwa adabu na familia zao, hata hivyo miezi 10 baadaye wanafunzi 392 walirejeshwa chuoni, isipokuwa Sitta na wenzake saba.

Ingawa Mwalimu alikuja kumsamehe baadaye, lakini alilazimika kutandikwa viboko na Mwalimu Nyerere, ikiwa ni sehemu ya msamaha huo.

Huu ni ujasiri wa hali ya juu, kwani haikuwa rahisi kwa mtu kumsema Mwalimu, ilihitaji ushupavu na ujemadari uliotukuka ambao Sitta alikuwa nao.

Kisiasa. Sitta alikuwa mwanasiasa mbobezi, aliyebobea kwenye siasa za hoja na urari katika masuala muhimu yaliyogusa masilahi ya wananchi.

Sitta ameweza kuhudumu kwenye aina zote mbili za kisiasa nchini, siasa ya chama kimoja na hata hizi za vyama vingi.

Historia yake ya kisiasa inaanzia mbali, hakuibuka kama uyoga mwituni, bila shaka alilelewa katika misingi bora na imara ya siasa za kukosoa na kukosolewa na ndiyo maana alifanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali za kiuongozi ndani na nje ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwa ni pamoja na nafasi ya ukuu wa mkoa na baadaye uwaziri katika wizara mbalimbali.

Hata hivyo, utofauti wa Sitta na wanasiasa wengine ulianza kujidhihirisha wakati wa Bunge la tisa, ambalo ndilo lilikuwa Bunge la kwanza la Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Sitta alifungua maana mpya ya Bunge, alitimiza kwa vitendo ahadi yake ya kulifanya Bunge la tisa kuwa la kasi na viwango.

Sitta aliweza kulifanya hilo, alilisimamia Bunge lake kwa haki, hakuwa mwoga mbele ya serikali, aliikosoa na kuirekebisha pale palipokuwa na haja hiyo.

Kamwe hakuona haya kusema wazi wazi makosa ya Serikali, hakuogopa kutengwa na watawala hata pale walipoonyesha kumtenga. Kwake aliamini katika kutenda kile ambacho Bunge lilipaswa kutenda.

Uwezo wake huo ndio unaomtofautisha na maspika wote wanaokuja mbele yake na labda anaweza kupatikana wa aina yake au wa kukaribiana naye baada ya miaka 60 kutoka sasa.

Tangu afanyiwe hiyana za kuenguliwa kwenye mbio za Uspika wa Bunge la 10, jamii imeshuhudia warithi wake kwenye kiti hicho cha juu ndani ya Bunge wakishindwa angalau hata kuyakaribia yale aliyokuwa akiyafanya yeye.

Katika kipindi cha uongozi wake bungeni ndipo jamii iliposhuhudia serikali ikilaumiwa kwa mengi, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mali za umma, idara ya mahakama ikilaumiwa kwa kushindwa kuwatia hatiani watuhumiwa waliofikishwa mahakamani na serikali kwa tuhuma mbalimbali, labda kwa wakati ule ni Bunge pekee ambalo lilifanya kazi sahihi ya kuwapigania wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles