KHARTOUM, SUDAN
MKATABA wa mwisho wa amani nchini Sudan Kusini, unatarajiwa kutiwa saini wiki ijayo, jijini Khartoum nchini Sudan.
Pande zote tatu zimesema kuwa mkataba huu unahusisha kuachiliwa huru kwa wafungwa, utoaji wa misaada ya kibinadamu na kuundwa kwa Serikali ya mpito ndani ya miezi minne.
Waziri wa Habari, Michael Makuei, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kuwa mazungumzo yanayoendelea kwa sasa yanakwenda vizuri.
Michael Makuei, amesema pande hasimu nchini humo zimefikia mwafaka kuhusu muswada wa mkataba wa mwisho wa amani, ambao unatarajiwa kusainiwa Agosti 27, jijini Khartoum.
Amesema mazungumzo ya sasa yanahusu masuala ambayo hayajatatuliwa ya kugawana madaraka na mipango ya usalama.
Naye Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Nicholas Haysom, ametaka pande zote kushughulikia kwa kikamilifu suala la usalama katika mkataba huo.