Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Mdhamini wa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, Robert Katula, katika kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge huyo na wahariri wa gazeti la Mawio, amedai mshtakiwa huyo hana ushirikiano hivyo anaomba kujitoa.
Katula ametoa madai hayo leo Jumatatu Machi 25, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya mahakama kutaka maelezo yake kuhusu mshtakiwa Lissu.
“Mheshimiwa sina la kusema, sina taarifa naye, hana ushirikiano kwa kweli, ikiwezekana nijitoe,”alidai.
Hata hivyo, Hakimu Simba alisema hawezi kujitoa wakati mshtakiwa hayupo mahakamani hivyo alimtaka ahakikishe amefika ndiyo ajitoe.
Kesi hiyo ilikuja kwa kutajwa leo, imeahirishwa hadi Aprili 25 mwaka huu.
Mbali na Lissu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uchochezi ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.