27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

MCL YATAKA VYOMBO VYA DOLA KUMSAKA MWANDISHI ALIYETOWEKA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


KAMPUNI ya Magazeti ya Mwananchi Communication Limited (MCL), imeiomba serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kusaidia kumtafuta Mwandishi wa Habari wa Gazeti ma Mwananchi, Azory Gwanda (42), aliyetekwa na watu wasiojulikana hivi karibuni.

Gwanda alitoweka katika mazingira ya kutatanisha Novemba 21, mwaka huu, akiwa katika kituo chake cha kazi wilayani Kibiti, Mkoa wa Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai alisema hadi sasa hawajapata taarifa zozote kutoka Jeshi la Polisi kuhusu kupotea kwa mwandishi huyo.

“Gwanda alianza kuliandikia Mwananchi Septemba, mwaka 2015 na hatukuwahi kupata taarifa zozote kutoka kwake juu ya kutishiwa maisha.

“Kwa hali tuliyonayo, hatuwezi kusema kazi yake ya mwisho aliyoifanya ni ipi, lakini tunaomba kama ameshikiliwa kwa kosa lolote apelekwe kwenye vyombo vya sheria ili haki itendeke,” alisema Nanai.

Kwa mujibu wa Nanai, MCL wanatarajia kuandika barua kwa taasisi mbalimbali kuonyesha jinsi gani wasivyoridhishwa na utekwaji wa mwandishi wao wa habari.

Barua hizo zitakwenda kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Spika wa Bunge, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MisaTan) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).

ALIVYOTOWEKA

Akizungumzia jinsi tukio lilivyotokea, Nanai alisema kwa mara ya mwisho mwandishi huyo aliwasiliana na ofisi za Mwananchi, Novemba 20 mwaka huu kwa majukumu ya kikazi.

“Kwa mujibu wa mkewe, Anna Pinoni (35) asubuhi ya Novemba 21, mwaka huu watu wanaokadiriwa kuwa wanne wakiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye rangi nyeupe, walifika katikati ya mji wa Kibiti sehemu ambayo Gwanda hupatikana mara kwa mara na kumchukua.

“Baadaye gari hilo lilielekea shambani kwake saa nne asubuhi na kumkuta mkewe huyo akiwa huko.

“Kwa hiyo, Gwanda aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma kwenye gari hilo alimuita mkewe huyo na kumuuliza alikokuwa ameweka ufunguo wa nyumba yao.

“Mkewe alilisogelea gari na kuzungumza naye kutokea dirishani na kumwelekeza alipoficha ufunguo. Baadaye, Gwanda alimwambia mkewe huyo kwamba amepata safari ya dharura na kama asingerudi siku hiyo angerudi siku inayofuata kwa maana ya Novemba 22.

“Tangu siku hiyo, Gwanda hajaonekana tena na namba zake za simu za mkononi hazipatikani.

JUKWAA LA WAHARIRI

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Theophil Makunga, jana alilisema tukio la kutoweka kwa mwandishi huyo linatishia uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Kuna nia ovu katika kukamatwa kwa Gwanda kwa sababu kama alifanya kosa la jinai, sheria ingechukua mkondo wake.” alisema Makunga.

UTPC YALAANI

Nao Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UPTC), umeviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa haraka ili kufanikisha kupatikana kwa mwandishi huyo.

Rais wa UTPC, Deogratious Nsokolo, alisema jana, kuwa wamepokea taarifa hiyo kwa mshtuko na wanalaani kitendo hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles