25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

KILI STARS MTEJA KWA ZANZIBAR HEROES

Na MWANDISHI WETU, MACHAKOS-KENYA


TIMU ya Zanzibar Heroes imeendeleza ubabe mbele ya ndugu zao wa Kilimanjaro Stars, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, mchezo wa kundi A Kombe la Chalenji uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos, nchini Kenya.

Katika mchezo huo ulioanza saa nane mchana, Kilimanjaro ilijikuta ikipoteza pointi tatu licha ya kutangulia kufunga bao la kuongoza.

Kipigo hicho kinaifanya Kilimanjaro Stars kuendeleza unyonge dhidi ya Zanzibar Heroes, baada ya kushindwa  kulipa kisasi cha kuchapwa kwa mikwaju ya penalti 6-5 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa michuano hiyo ilipofanyika nchini Uganda mwaka 2012.

Ushindi huo unaifanya Zanzibar Heroes kufikisha pointi sita na kuongoza kundi A, ikiiacha Kilimanjaro Stars ikipambana na hali yake ikiwa na pointi moja baada ya kushuka dimbani mara mbili.

Mabao ya Zanzibar Heroes katika mchezo huo yalifungwa na Kassim Khamis dakika ya 66 na Ibrahim Ahmada dakika ya 77, wakati bao pekee la Kilimanjaro Stars likifungwa na Himid Mao dakika ya 28.

Mchezo huo ulianza kwa kasi, ambapo dakika ya tano, Mudathir Yahaya, alimtoka beki wa Kilimanjaro Stars, Gadiel Michael na kuachia shuti kali lililopaa juu kidogo ya lango.

Dakika ya nane, kocha wa Kilimanajaro Stars, Ammy Ninje, alifanya mabadiliko kwa kumtoa Kelvin Yondani aliyeumia na kumwingiza Boniface Maganga.

Dakika ya 13, Ibrahim Hamad, nusura aipatie bao la kuongoza Zanzibar Heroes, baada ya mkwaju wake kutoka nje kidogo ya lango la Kilimanjaro Stars.

Dakika ya 28, Himid Mao, aliwainua mashabiki wa Kilimanjaro Stars baada ya kufunga bao la kuongoza kwa kugongeana vema na Dany Lyanga.

Dakika ya 38, kocha wa Zanzibar, Hemed Suleiman, alifanya mabadiliko, alimtoa, Hamad Mshamata na kumwingiza Selemani Kassim ‘Selembe’.

Kilimanjaro Stars ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao moja.

Kipindi cha pili kilipoanza, Kilimanjaro ilizindua mashambulizi mapya ambapo dakika ya 46, Mzamiru Yassin alipokea pande safi la Elias Maguli lakini mkwaju wake ulitoka nje ya lango la Zanzibar Heroes.

Mashambulizi ya kupokezana yaliendelea na dakika ya 57, Mudathir alipokea pasi murua ya Ibrahim Hamad, lakini alishindwa kufunga bao baada ya kupiga shuti lililotoka nje ya lango la Kilimanjaro Stars.

Dakika 58, Zanzibar Heroes ilifanya mabadiliko, alitoka, Mudathir na nafasi yake kuchukuliwa na Kassim Khamis.

Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kwa upande wa Zanzibar Heroes, kwani dakika ya 66, Kassim aliifungia bao la kusawazisha baada ya kutumia vema makosa ya mabeki wa Kilimanajro Heroes waliozembea kuondoa mpira wa hatari uliokuwa ukizagaa langoni mwao.

Dakika ya 68, Feisal Abdallah, alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Mzamiru Yassin wa Kilimanjaro Stars.

Dakika ya 70, mlinda mlango wa Zanzibar Heroes, Mohamed Abrahman, alifanya kazi ya ziada kuokoa mchomo mkali wa Maguli aliyewazidi maarifa mabeki wake.

Dakika ya 74, Haji Mwinyi wa Zanzibar Heroes alilimwa kadi ya njano kwa kosa la kumchezea rafu Kennedy Juma wa Kilimanjaro Stars.

Dakika ya 76, Kilimanjaro Stars ilifanya mabadiliko, alitoka Maguli na nafasi yake kuchukuliwa na  Yahya Zayd.

Dakika ya 77, Ibrahim Ahmada, aliiandikia bao la pili Zanzibar Heroes, baada ya kuunganisha pasi ya Selembe

Dakika ya 87, Zanzibar Heroes ilifanya mabadiliko, alitoka Kassim baada ya kuumia na kuingia Ibrahim Abdallah.

Mabadiliko hayo hayakuweza kubadili matokeo ya mchezo huo kwani hadi dakika 90 za mchezo huo zinamazilika, Kilimanjaro Stars ilitoka kichwa chini baada ya kuchapwa mabao 2-1.

Kili Stars: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Kelvin Yondani, Abdallah Hamis, Shiza Kichuya, Himid Mao. Elias Maguli. Daniel Lyanga na Mzamiru Yassin.

Zanzibar Heroes: Mohamed Abrahman, Ibrahim Mohamed, Haji Mwinyi Ngwali, Abdulla KheriIssa Haidar Dau, Abdul Azizi Makame, Mohamed Issa, Mudathir Yahaya, Ibrahim Hamad Hilika, Feisal Salum na  Hamad Mshamata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles