ANDREW MSECHU -DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) amemuomba radhi Katibu Mkuu mstaafu wa CCM , Abdulrahman Kinana kutokana na tuhuma dhidi yake alizowahi kuzitoa bungeni kwa kuwa hazikuwa na ukweli wowote.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, Msigwa alisema anakiri mbele ya Watanzania, kwamba tuhuma hizoalizowahi kuzitoa mara kadhaa dhidi ya Kinana hazikuwa na ukweli wala ushahidi wowote.
“Taarifa nilizopewa na kuzitumia hazikuwa na ukweli bail zilikuwa na malengo potofu ya kisiasa na kizandiki. Nasikitika kwamba taarifa hizo nilipewa na watu waliokuwa na malengo maovu.
“Mambo kama haya hutokea katika jamii na maishani. Nasi kama binadamu inapotokea kuwakosea wenzetu busara hututuma kuomba radhi na kwa waliokosewa kuwa tayari kusamehe.
“Ni dhahiri kwamba kupitia kauli zangu za huko nyuma dhidi yake, nimemkosea, nimemdhalilisha na kumkashifu ndugu yangu Kinana. Nafurahi kuwaambia hapa kwamba nimekutana na kaka yangu Kinana na kumuomba radhi yeye binafsi na amekubali kunisamehe. Baada ya msamaha huo wa Kinana, sasa shauri hili la kimahakama sasa litakuwa limemalizika rasmi,” alisema.
Alisema itakumbukwa kwamba kutokana na tuhuma hizo alikuwa na kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania iliyofunguliwa na Kinana dhidi yake kwa sababu ya matamshi aliyowahi kuyatoa dhidi yake ndani na Bunge, akimhusisha na biashara ya ujangili na uuzaji wa nyara za Serikali.
Msigwa alieleza kuwa katika hotuba yake akiwa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni akiwasilisha maoni yao wakati wa mjadala wa makadirio ya matumizi ya
Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2013/2014, alitoa maelezo marefu ya kumhusisha Kinana na biashara hizo.
Alisema kutokana na tuhuma zakeu hizo kwake, Kinana alinifungulia mashitaka katika Mahakama Kuu ya Tanzania kwa shauri namba 108 ya mwaka 2013.
“Nimekuja hapa hadharani kuomba radhi kwa sababu nafahamu aliyeumizwa si Kinana peke yake, bali familia yake, ndugu zake, marafiki zake na Watanzania kwa ujumla wao,” alisisitiza.
Kabla ya kupeleka suala hilo mahakamani, Kinana kupitia kwa wakili wake, Erick Sikujua Ng’maryo, alimtaka Msigwa kufuta kauli zake hizo na kuomba radhi hadharani kwa kuwa kauli zake hizo hazikuwa na ukweli wowote. Msigwa alikataa kufanya hivyo na kusema yuko tayari kujitetea mahakamani.
Jaji Zainab Muruke aliyesikiliza na kuamua kesi hiyo, alieleza kitendo cha wanasiasa kutoa kauli za kudhalilisha wenzao pasipo kuwa na ushahidi wala ukweli wowote kama “tabia mbaya” inayopaswa kukemewa.