KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
Mcheza Video, Rutyfiya Abubakary maarufu kama Amber Rutty na mpenzi wake Said Bakari Mtopali wanaoshtakiwa kwa makosa mawili likiwemo la kufanya mapenzi kinyume na maumbile wamedhaminiwa leo Novemba 27 saa nne asubuhi.
Washtakiwa hao waliokosa wadhamini kwa takribani mara tatu, leo wamepata dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili, wenye vitambulisho vya Taifa na wamesaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 15.
Mmoja wa wadhamini wa Saidi Bakari ni Mchungaji wa Kanisa la Pentekosti Mbezi Mwisho, mchungaji Daudi Mashimo. Washtakiwa hao na mwenzao James Delicious alikuwa ametimiza masharti ya dhamana tangu Novemba 2 mwaka huu wamepanda kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Rwizire wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Awali Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga alidai katika kosa la kwanza washtakiwa hao wanadaiwa kufanya mapenzi kinyume na maumbile kosa ambalo linamkabili, Amber Rutty.
Inadaiwa ametenda kosa hilo kati ama baada ya Oktoba 25, 2018 ambapo alimruhusu, Said Bakari Mtopali kumuingilia kinyume na maumbile. Shtaka lingine linalowakabili washitakiwa hao ni la kufanya mapenzi kinyume na maumbile, linamkabili mshtakiwa wa pili, Said Bakari Mtopali ambapo anadaiwa kati ama baada ya Oktoba 25, 2018 jijini Dar es Salaam alifanya mapenzi na Amber Rutty kinyume na maumbile.
Kosa la tatu linalowakabili washitakiwa hao ni kuchapisha video ama picha za ngono, ambapo linamkabili James Charles ama James Delicious anayedaiwa Oktoba 25, 2018 kusambaza video za ngono kupitia magroup ya Whatsapp. Kosa la nne ni kusababisha kusambaa picha za ngono kosa ambalo linamkabili, Amber Rutty na Said Abubakari Mtopali ambapo wanadaiwa Oktoba 25, 2018 walisababisha kusambaza picha za ngono kupitia makundi ya Whatsapp.
Washtakiwa walipewa masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili kila mmoja na kusaini dhamana ya maandishi ya Sh. Milioni 15. Pia wadhamini wawe na vitambulisho vya taifa pamoja na kuwasilisha hati za kusafiria na wasitoke nje ya Dar es Salaam bila kibali.