24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Burundi kumkamata Buyoya kwa mauaji ya Ndadaye

BUNJUMBURA, BURUNDIMAMLAKA ya Burundi imewakamata maafisa wanne wastaafu wa jeshi na kutoa hati ya kukamatwa kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Pierre Buyoya kwa tuhuma za kushiriki mauaji ya Rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia, Melchoir Ndadaye mwaka 1993.

Uamuzi huo ulitangazwa siku ya Jumamosi na Mwanasheria Mkuu, Sylvestre Nyandwi.

Mwanasheria huyo alisema kukamatwa kwao kunalenga kukomesha tabia ya  kutowaadhibu wahalifu kama inavyodaiwa na raia na jamii ya kimataifa.

Katika mahojiano na waandishi wa habari, Nyandwi alisema licha ya kuwa kesi juu ya mauaji ya Ndadaye ilikuwa tayari mahakamani na hukumu kutangazwa lakini  taasisi yake ilikuwa tayari imeitaka Mahakama Kuu isikilize upya kesi hiyo.

“Mahakama Kuu ilitakiwa kubainisha msimamo wake baada ya kudhihirika kuwa kesi hiyo bado haijakamilika. Kwani ilitambulika baadaye kuwa kuna watu waliohusika kwa kiasi kikubwa na ukatili bado hawajaguswa na sheria,” alisema Nyandwi.

Waliokwisha kamatwa ni pamoja na Kanali Gabriel Gunungu, Kanali Anicet Nahigombeye, Kanali Niyonkuru na Jemedari Celestin Ndayisaba, wote wakiwa maafisa wastaafu wa jeshi waliohudumu wakati wa utawala wa Buyoya.

Waliotolewa hati ya kukamatwa mbali ya Buyoya, ambaye ni mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Mali na katika Ukanda wa Sahel, ni maafisa wengine 18 wa jeshi waliostaafu.

Miongoni mwao ni pamoja na Kanali Bernard Busokoza aliyewahi kuwa Makamu wa Rais chini ya utawala wa Rais Pierre Nkurunziza.

Chama cha Sahwanya Frodebu cha Marehemu Ndadaye, mbali na kukaribisha hatua hiyo, kilisema lazima izingatie mpango mzima wa utangamano wa kitaifa na kuwa walikubaliana kwenye mikataba ya usitishwaji mapigano kesi kama hiyo ishughulikiwe kwenye Tume ya Ukweli na Maridhiano.

Tume hiyo iliongezewa muda wake na kupatiwa wajumbe wapya wiki iliyopita  ambapo sasa inaongozwa na Pierre Claver Ndayicariye, mkuu wa zamani wa Tume ya Uchaguzi (CENI) na Karenga Ramadhani akiwa miongoni mwa wajumbe 15 wa tume hiyo.

Familia za maafisa hao wastaafu jeshini waliokamatwa, na ambao wote ni kutoka jamii ya Watutsi, zinasema zinahofia usalama wa wastaafu hao wanaoelemewa na umri mkubwa na baadhi wakikabiliwa na matatizo ya afya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,208FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles