Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
BARAZA la Mtihani la Taifa (NECTA), limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika Novemba mwaka jana, ambapo safari hii mchuano kati ya wasichana na wavulana umekuwa mkali, huku ufaulu ukipanda kwa asilimia 70.09 tofauti na mwaka 2015 ambapo ulikuwa asilimia 67.53.
Kutokana na matokeo hayo ufaulu kwa wanafunzi kuanzia daraja la I-III umepanda kwa asilimia 27.6 na daraja la nne asilimia 42.75.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alisema katika matokeo hayo wanafunzi waliofeli mwaka jana ni asilimia 29.65.
Alisema watahiniwa 408,372 walisajiliwa kufanya mtihani huo ambapo wasichana walikuwa 209,456 sawa na asilimia 51.29 na wavulana 198,916 asilimia 48.71.
Mchuano mkali
Katika matokeo hayo mchuano mkali umeonekana katika matokeo hayo, ambapo wasichana watano wameingia katika 10 bora huku wakitoshana nguvu sawa na wavulana ambao nao wameingia watano.
Pamoja na hali hiyo Dk. Msonde, alisema katika ufaulu wa jumla, wasichana na wavulana wamekaribiana ambapo kwa watahiniwa wa shule kati ya 244,762 waliofaulu mtihani huo, wasichana ni 119,896 sawa na asilimia 67.34 na wavulana 124,866 sawa na asilimia 73.5.
Licha ya matokeo hayo shule za Mkoa wa Dar es Salaam zimeingia kwenye rekodi ya aina yake kwa kutoa shule tatu ambazo zimeingia katika 10 bora, pamoja na kutoa shule sita ambazo zimeshika mkia katika shule 10 za mwisho jambo ambalo halikuwahi kutokea.
Ubora wa ufaulu
Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa wa shule waliopata ufaulu mzuri (daraja la I-III) ni 96,018 sawa na asilimia 27.60, ambapo daraja la kwanza ni 9,458 sawa na asilimia 2.72, kati yao wavulana ni 5,723 sawa na asilimia 3.37 wasichana 3,735 sawa na asilimia 2.1.
Waliopata daraja la pili ni 32,391 sawa na asilimia 9.31 kati yao wavulana ni 19,959 sawa na asilimia 11.75 na wasichana 12,432 sawa na asilim8ia 6.98.
Watahiniwa waliopata daraja la tatu ni 54,169 sawa na asilimia 15.57 wavulana wakiwa 31,054 sawa na asilimia 18.28 na wasichana 23,115 sawa na asilimia 12.98.
Matokeo yanaonyesha pia watahiniwa walipata daraja la nne ni 148,744 sawa na asilimia 42.75 wavulana wakiwa 68,130 sawa na asilimia 40.1 na wasichana 80,614 sawa na asilimia 45.28.
Waliofeli mtihani huo ni watahiniwa 103,164 sawa na asilimia 29.65 wavulana wakiwa 45,024 sawa na asilimia 26.5 na wasichana wakiwa 58,140 sawa na asilimia 32.66.
Katika Mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015, watahiniwa wa shule waliopata daraja la kwanza walikuwa 5,973 sawa na asilimia 2.77 tu, hivyo ikilinganishwa na mwaka 2016, ufaulu kwenye eneo hili umeshuka.
Kwa daraja la pili mwaka 2015 walikuwa 19,791 (asilimia 9.01), daraja la tatu 27,749 (asilimia 13,56) na daraja la tatu la juu ni watahiniwa 53,513 (asilimia 25.34).
Waliopata daraja la nne ni watahiniwa 71.358 sawa na asilimia 67.91 na waliofeli ni 47,812 sawa na asilimia 32.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Msonde alisema. “Juhudi za makusudi zinahitajika kuendelea kufanyika ili kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo yote ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watahiniwa kwenye madaraja ya juu ya ufaulu,” alisema
Katibu Mtendaji huyo wa NECTA, alisema baraza hilo litafanya uchambuzi wa kina wa matokeo hayo kwa kila somo na kutoa machapisho yatakayowasilishwa kwa wadau wa elimu nchini.
Alisema kati ya wadau hao ni shule zote za sekondari nchini lengo likiwa ni kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.
Ufaulu kwa masomo
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa, somo la hisabati watahiniwa hawakufanya vizuri ambapo ni asilimia 18.12 pekee waliofanya vizuri ingawa mwaka 2015 hali ilikuwa mbaya zaidi kwa asilimia 16.76 pekee kufanya vizuri.
Masomo mengine na asilimia za ufaulu wake kwenye mabano ni biashara (40.89), Book Keeping (49.7), Fizikia ( 44.77), Uraia (48.9), Historia (48.06), Jografia (51.4), Baiolojia 55.69, Kemia (59.22), Kingereza (64.27) na Kiswahili (77.75).
Matokeo yaliyofutwa
Kwa mujibu wa matokeo hayo watahiniwa 126 wamefutiwa matokeo kutokana na kubainika kufanya udanganyifu.
Kati ya watahiniwa hao 58 ni wa kujitegemea, 58 wa shule na 10 wa Mtihani wa Maarifa (QT), huku mtahiniwa mwingine mmoja akifutiwa mtihani wake kutokana na kuandika matusi kwenye karatasi ya majibu.
Dk. Msonde alisema baraza limezuia matokeo ya watahiniwa 33 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa baadhi ya masomo.
“Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2017,” alisema Dk. Msonde.
Alisema pia watahiniwa 124 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote matokeo yao yamezuiliwa na wamepewa nafasi ya kurudia mtihani huo mwaka huu.
Watahiniwa wengine 40 matokeo yao yamezuilikuwa kutokana na shule kutopeleka matokeo ya maendeleo ya wanafunzi shuleni (Continues Assessment-CA).
Mwaka 2015, watahiniwa 87 waliobainika kufanya udanganyifu walifutiwa matokeo kati yao 25 wakiwa ni wa kujitegemea, 52 wa shule na 10 QT.
Alisema pamoja na hali hiyo watahiniwa 23 walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani ambapo walishindwa kufanya mitihani kwa baadhi ya masomo, matokeo yao yalizuiwa na wengine 98 walishindwa kufanya mtihani yote.
Waliofanya mtihani
Katika mtihani huo ambao watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 408,372, wasichana wakiwa 209,456 sawa na asilimia 51.29 na wavulana 198,916 sawa na asilimia 48.71, kati yao washule walikuwa 355,822 na wakujitegema 52,550.
Alisema watahiniwa wa shule waliosajiliwa kufanya mtihani huo, 349,524 sawa na asilimia 98.23 ndio walioufanya, wasichana wakiwa 178,775 sawa na asilimia 97.97 na wavulana 170,749 sawa na asilimia 98.5 huku watahiniwa 6,298 wakiacha kufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, kati ya 52,550 waliosajiliwa, waliofanya ni 47,751 sawa na asilimia 90.87 wengine 4,799 sawa na asilimia 9.13 wakishindwa kuufanya.
Kwa upande wa wale wa QT , waliosajiliwa walikuwa 20,655 lakini waliofanya ni 17,347 sawa na asilimia 83.98 na wengine 3,308 sawa na asilimia 16.02 walishindwa kuufanya kwa sababu mbalimbali.
Shule kumi bora kitaifa
Matokeo hayo yanaonyesha shule 10 bora kitaifa, zinaongozwa na Feza Boys (Dar es Salaam), Shule ya wasichana ya St. Francis (Mbeya), Kaizerege Junior (Kagera) Shule ya wasichana ya Marian na ile ya Wavulana (Pwani).
Nyingine ni Shule ya wavulana Shamsiye (Dar es Salaam), Shule ya wasichana Anwarite (Kilimanjaro), Shule ya wasichana ya Kifungilo (Tanga) na Thomas More Machrina (Dar es Salaam).
Shule kumi za mwisho
Shule zilizoshika kumi za mwisho ni pamoja na Kitonga, Nyeburu zote za Dar es Salaam, Masaki (Pwani), Mbopo, Mbondole, Somangila Day zote kutoka Dar es Salaam.
Nyingine ni Dahani (Kilimanjaro), Ruponda (Lindi), Makiba (Arusha) na Kidete (Dar es Salaam).
Wanafunzi kumi bora
Wanafunzi waliongoza kumi bora ni pamoja na Alfred Shauri (Feza Boys), Cynthia Nehemiah Mchechu (St Francis Girls), Erick Mamuya (Marian Boys), Jigna Chavda (St Mary Goreti).
Wengine ni Naomi Tundui (Marian Girls), Victor Chang’a (St Francis Girls), Brian Johnson (Marian Boys), Esther Mndeme (St Mary’s Mazinde Juu), Ally Koti (Alcp Kilasara) na Emmanuel Kajege (Marian Boys).