Aveline Kitomary -Dar es salaam
WIZARA ya Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekanusha tetesi za kuwepo kwa mtu anayeshukiwa kuwa na ugonjwa wa virusi vya corona nchini.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo –Idara kuu ya Afya, Catherine Sungura alisema kuwa timu ya wataalamu wa afya ilifika eneo aliko mshukiwa huyo aliyetokea nchini China Februari 2 mwaka huu na kuingia jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo baada ya kufanikiwa kumfanyia uchunguzi wataalamu hao walibaini kuwa raia huyo mwenye asili ya China hana dalili za kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Aidha Wizara hiyo ilitoa rai kwa wananchi kutokuwanyanyapaa raia wa kigeni hasa raia wenye asili ya China pamoja na watu wanaovaa ‘mask’ kwa nia ya kujikinga njia ya hewa kwa kuwa ni utaratibu wa kawaida duniani ambao hutumika kwenye msongamano wa watu.
“Pamoja na hayo Wizara imeimarisha ukaguzi wa afya mipakani na katika viwanja vya ndege kwa kuhakiksha watu wote wanaotoka na kuingia wanakaguliwa kikamilifu,” inasomeka taarifa hiyo.
Mlipuko wa virusi vya corona ulioanzia katika jiji la Wuhan nchini China mbali na kusababisha vifo vya watu 637 na maambukizi kwa watu 31,198 umesababisha hofu kubwa duniani.
Ugonjwa huo unaambukizwa kwa njia ya hewa kwa kuingia na majimaji yenye virusi kutoka kwa mtu mmoja kwa kukohoa au kupiga chafya au kwa kugusa majimaji au makamasi kutoka kwa mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo.
Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa na mafua makali, kuumwa kichwa, mwili kuchoka, kikohozi, kubanwa mbavu, maumivu ya misuli, vidonda vya koo, kuathiri mapafu, kupumua kwa shida na hadi kifo.