Na Masyaga Matinyi- Manyara |
MIEZI mitatu ikiwa imepita tangu Rais Dk. John Magufuli azindue ukuta kuzunguka migodi ya madini ya vito ya tanzanite, hakuna udhibiti makini wakati wa kuingia na kutoka ndani ya eneo hilo hasa kwa wale wanaoingia kwa kutumia magari ambao wengi wao ni wamiliki wa migodi (matajiri), wanunuzi wa madini na watendaji wa Serikali.
Ukuta huo wenye urefu wa kilomita za mraba 24.5 na urefu wa mita tatu kwenda juu, umegharimu takribani Sh bilioni sita na umezunguka eneo hilo maarufu la machimbo ya Mirerani mkoani Manyara na hutembelewa na wamiliki wa migodi, wachimbaji wakubwa na wadogo, maofisa wa Serikali, wafanyabiashara wanaouza bidhaa tofauti na wageni mbalimbali.
Ukuta huo una geti moja kubwa ambalo hutumika kwa ajili ya kuingia na kutoka na getini kuna polisi wenye silaha na maofisa wengine wa Serikali wenye nguo za kiraia.
MTANZANIA Jumapili ambalo limekuwapo katika eneo hilo na kufanikiwa kuingia na kutoka ndani ya ukuta zaidi ya mara nane, limebaini upungufu mkubwa na hali hiyo inarahisisha utoroshaji wa tanzanite na tatizo hilo limekuwapo kwa muda mrefu na kuliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya fedha.
Tatizo hilo ndilo lililosababisha Septemba 20, mwaka jana, Magufuli achukue uamuzi wa kuagiza ukuta huo kujengwa ili kudhibiti vitendo hivyo na baada ya ujenzi wake kukamilika, mapato ya Serikali yatokanayo na mrabaha katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu yameongezeka na kufikia Sh milioni 714.6 na kuyapiku mapato ya miaka mitatu mfululizo (mwaka 2015 (Sh milioni 166.8), mwaka 2016 (Sh milioni 71.8) na mwaka 2017 Sh milioni 147.1) na pengine kama vitendo hivyo visingekuwepo bila shaka yangeongezeka zaidi.
Kabla ya kuingia ndani ya ukuta huo, kuna kitabu ambacho wanaoingia huandika majina yao na wakati mwingine hutakiwa kuonyesha vitambulisho na hatua hiyo hufanyika zaidi kwa wanaoingia kwa kutumia pikipiki na waenda kwa miguu.
Hata hivyo, kwa wale wanaoingia kwa kutumia magari ambao wengi wao ni wamiliki wa migodi (matajiri), wanunuzi wa madini na watendaji wa Serikali, hakuna anayewauliza kitu zaidi ya kusalimiana na kuingia ndani ya ukuta.
HALI ILIVYO WAKATI WA KUTOKA
Kwa kawaida wakati wa kutoka kuna ukaguzi ambao hufanyika kwa baadhi ya watu wanaotoka, ingawaje aina ya ukaguzi unaofanyika hauwezi kumzuia mtu mwenye nia ya kutorosha jiwe au mawe kushindwa kufanikisha azma yake.
Siku zote wakaguzi huwa ni maofisa wa Serikali waliovaa nguo za kiraia na wakati mwingine husaidiana na polisi.
Lakini mara kadhaa ukaguzi hufanyika wakiwa wamekaa kwenye viti na humkagua mtu anayetoka migodini kwa kumpapasa katika mifuko ya suruali, shati au koti kisha kumruhusu na hakuna vifaa vyovyote vinavyotumika.
Kwa wamiliki wa migodi maarufu kama matajiri na wanunuzi wakubwa wa mawe, wao hawakaguliwi kabisa na hubaki ndani ya magari yao na wanaoshuka na kukaguliwa ni madereva na watu walioambatana nao.
Pia ukaguzi ndani ya magari haufanyiki kabisa kwa baadhi ya magari, jambo linalotoa mwanya kwa mawe kutoroshwa, hasa kwa kuzingatia baadhi ya wachimbaji na wafanyabiashara wameshajenga urafiki na wenye dhamana ya kulinda geti hilo.
Magari yenye namba za Serikali yanayoingia eneo hilo pamoja na abiria waliomo ndani hayafanyiwi ukaguzi kabisa wakati wa kuingia na kutoka.
JICHO LA SERIKALI NDANI YA MIGODI
Katika mahojiano na baadhi ya wamiliki wa migodi na wachimbaji wanaozama chini ya ardhi (majina tunayahifadhi), walisema bado kuna udanganyifu mkubwa unaondelea kuhusu madini halisi yanayopatikana katika migodi.
“Wakati mwingine ni vizuri ukweli ukafahamika, hawa maofisa wa madini na wale wa mapato ya Serikali ambao wanazama migodini wakati wa uzalishaji, huwa hawapati taarifa sahihi.
“Kuna baadhi ya miundombinu ya migodi kule chini inahitaji uzoefu na ujasiri kufika, sasa utakuta inapigwa baruti eneo fulani chini ardhini na tanzanite kutoka, lakini katika eneo hilo unakuta vijana hao wa Serikali hawafiki.
“Mara nyingine huishia eneo fulani na kusubiri, sasa baadhi ya wenye migodi na wachimbaji hufika tanzanite ile nzuri na kupandisha ile ya kiwango cha chini, ambayo ndiyo hufanyiwa makadirio kwa ajili ya mapato ya Serikali.
“Kwa sababu hawa wachimbaji wazoefu hapa migodini ni ma-geologist wazuri sana, wanayajua haya mawe (tanzanite) kuliko unavyofikiria, kwa hiyo bado kuna ujanja mwingi unafanyika chini ardhini.
“Hivyo wakishamalizana na maofisa wa Serikali, huchukuwa mawe mazuri na kuyapitisha pale getini kwa urahisi kabisa na wale ambao wanakuwa na mawe mengi husubiri nyakati za usiku,” alisema mmoja wa wamiliki wa migodi.
KAMISHNA MSAIDIZI WA MADINI
Akizungumza hali hiyo, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma, alikiri kuwapo kwa upungufu kadhaa katika usimamizi wa ukuta huo.
Alisema ukaguzi kwa wanaoingia na kutoka hauridhishi pamoja na ujenzi wa ukuta huo kukamilika, lakini bado vifaa vya ukaguzi kama vile kamera na skana bado havijafungwa.
“Ni kweli kuna upungufu lakini tunayafanyia kazi, hata sasa hivi tunavyoongea nipo huku Mirerani na wajumbe wa Tume ya Madini tukifanyia kazi changamoto hizo.
“Ukaguzi pale getini hauridhishi, kwa mfano ni kosa kutokagua magari ya Serikali na ni kweli matajiri hawakaguliwi wanapoingia na kutoka.
“Pia ni vizuri kufahamu kuwa bado jeshi halijaanza ulinzi kwa asilimia 100, lakini kila kitu kitakapokuwa kimekamilika, hali iliyopo sasa itakwisha,” alisema.