24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 26, 2022

JPM AMPA MAAGIZO 10 MKUU MPYA JESHI LA MAGEREZA


Na AGATHA CHARLES        |

RAIS Dk. John Magufuli, amempa maagizo 10 Kamishna Jenerali mpya wa Magereza, Phaustine Kasike, huku akimwonya kuwa asipochukua hatua atamchukia.

Maagizo hayo aliyatoa jana Ikulu, Dar es Salaam, wakati akiwaapisha Kamishna Jenerali Kasike na Balozi Joseph Sokoine ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

Kamishna Jenerali Kasike ametakiwa kushughulikia promosheni za askari wa jeshi hilo, kuhakikisha mashine ya ukaguzi inafungwa, wafungwa wanajilisha wenyewe, wanafanya kazi ikiwamo ujenzi, kufanya ufugaji na kujenga nyumba za askari.

Pia alimtaka kuhakikisha mfungwa hafanyi mambo asiyotakiwa kama simu, bangi, kujamiiana lakini pia mfungwa kuhukumiwa kisha anakutwa na hatia nje ya gereza.

Akifafanua agizo moja baada ya jingine, Rais Dk. Magufuli ambaye alianza kwa kutoa pole nyingi kwa Kamishna Jenerali Kasike kuliko pongezi, alisema askari wako nyuma katika kupandishwa vyeo.

“Naanza kwa kukupongeza na kukupa pole. Mategemeo yangu nataka yakawe makubwa ya kuleta mabadiliko magerezani. Sio siri Jeshi la Magereza na maaskari wenyewe wamekaa kama wameachwa hivi, hata katika promosheni zao imekuwa ni tatizo.

“Wakati nampromoti Kamishna Jenerali aliyestaafu, palikuwa na makamishna wawili tu, si kwamba hawana sifa, waliachwa aidha kwa makusudi au kuhofia waliojuu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hadi Kamishna Kasike anashika kijiti hicho mtangulizi wake alikuwa ameanza kutekeleza agizo la Rais na kufanikiwa kuwapandisha Makamishna na Manaibu Kamishna zaidi ya 10, hivyo aendeleze hilo hadi kwa askari wa chini waliokaa muda mrefu.

Mbali na hilo, Rais Dk. Magufuli alirudia kauli yake aliyopata kuizungumza siku za nyuma kwamba ni jambo la aibu kwa nchi kulisha wafungwa kwa kuwa mashamba yapo.

Alisema wafungwa wanapaswa kufanya kazi na si kuomba msaada wa tofali wala chakula.

“Maeneo ya Magereza ni mengi, ukienda Mbeya eneo linalolimwa ni robo tu. Kila mwaka kuna maombi ya bajeti kulisha wafungwa, kufungwa maana yake ni ukamenyeke kwa kazi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema si sahihi watumishi wa magereza kukosa nyumba za kuishi na kuomba fedha serikalini wakati wafungwa wanaweza kufyatua tofali na kuzichoma.

Mbali na hilo, Rais Dk. Magufuli, alisema hataki kuona mtu akipangiwa majukumu kutokana na kufahamiana na mtu fulani.

“Sitaki niyasikie yale ya Mbeya, mfungwa amehukumiwa kufungwa ni jambazi halafu baadaye anashikwa akishirikiana kuwinda tembo porini na anakamatiwa huko wakati huku amehukumiwa kufungwa, sitaki nisikie mfungwa aliyeacha familia yake kule nyumbani anakuja mke wake gerezani, anakaribishwa na askari wa magereza akafanye yule mfungwa mambo ambayo hakutakiwa kuyafanya akiwa gerezani,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hataki kusikia wafungwa wakiwasiliana na familia au jamaa zao kupitia simu ambazo zimejaa magerezani na kusababisha kuwa kitu cha kawaida.

Katika hilo, Rais alikwenda mbali na kusema kuwa jambo hilo linafanyika hata katika magereza ya Dar es Salaam ambako wapo wanaopiga simu hadi nje ya nchi wakiwa gerezani.

“Sitaki kwenye magereza wafungwa wakapate nguvu ya kuvuta bangi na saa nyingine kujamiiana, kwa sababu hawafanyishwi kazi za kutosha. Sitaki mfungwa akafungwe, baadaye akiwa huko akaanze kufuga mbuzi na ng’ombe anapeleka hadi mnadani, anakuwa tajiri hata kuliko askari. Nina mifano ya kila gereza,” alisema Rais Magufuli.

Akisisitiza Rais Magufuli alisema: “Nakupongeza kidogo, pole ndio nyingi. Najua wapo maaskari watakaochukia kwa hatua utakazochukua na usipozichukua mimi utanichukia, nataka magereza ikafanye kazi askari wafaidike.”

Rais Magufuli pia alisema haoni sababu ya Jeshi la Magereza kukosa vitendea kazi kama trekta wakati Jeshi la Kujenga Taifa liliwahi kukopesha vitu hivyo.

Changamoto nyingine aliyotakiwa kuishughulikia ni fedha alizotoa kiasi cha takribani Sh bilioni 10 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba za maaskari katika eneo ya Ukonga ambazo hazijakamilika.

“Kama malori yamepungua, nitayatoa mengine yaliyokuwa ya polisi, nitawapa ninyi. Serikali ni moja, fedha ni za wananchi, kaeni mjadili namna mtakavyogawana. Ni wizara moja. Nataka Jeshi la Magereza likawe mfano,” alisema Rais Magufuli.

Alimtaka Kamishna huyo kupanga vizuri safu yake ikiwamo kushirikiana na makamishna wenzake katika kufanya kazi ili kupata mwelekeo.

“Kuna watu wana rekodi nzuri, mfano Mwakijungu alipelekwa Makete kila mtu alikuwa akipakataa, akapelekwa Iringa akafanya vizuri, mtu wa operesheni kama huyo mnampeleka akawe store keeper? (mtunza stoo), sina hakika kama wamepangwa vizuri. Sikufundishi kazi,” alisema Rais Magufuli.

Ili kukabiliana na tatizo la kupitisha simu kwa wafungwa, Rais Magufuli alishauri kifungwe kifaa cha utambuzi ili kuwabaini wahusika.

Zaidi alimtaka Kamishna huyo kutembelea magereza pamoja na kukutana na majeshi mengine nchini ili kupata mikakati ya kujiimarisha.

Awali Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ambaye alianza kwa kumwamkia Rais Magufuli kwa kusema; “Shikamoo Mheshimiwa Rais,” alisema mambo ambayo alimwagiza wakati akimwapisha alikwishaanza kuyafanyia kazi likiwamo suala la ajali za barabarani pamoja na mikataba.

Alisema baada ya kuingia kuongoza Wizara hiyo aliitisha mkutano na wakuu wa vyombo vilivyo chini yake kujitafakari huku akitoa siku 21 kila chombo kuwasilisha kwake taarifa ya mwelekeo.

“Zimebaki siku saba, hakika tutachukuwa hatua bila kutazama usoni,” alisema Lugola.

Alisema kwa sasa wanaelekea kufanya mikakati ya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika mwakani ili kuweka hali ya utulivu na usalama.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba, akizungumza katika hafla hiyo alisema walipata maelekezo ya Rais kuhusu ucheleweshaji wa vyeti vya tathmini ya athari kwa mazingira kwenye ujenzi wa viwanda.

“Wiki mbili zijazo nitasaini kanuni mpya za kufanya tathmini ya athari kwa mazingira ambazo zitawezesha ndani ya siku tatu tangu mtu atakapoleta ombi la kujenga kiwanda tutakuwa tumetazama na tutatoa ruhusa ya awali ili aanze kujenga halafu mchakato mwingine uendelee,” alisema January.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,051FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles