22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 29, 2022

MASTAA HAWA NYOTA ZAO ZINAWAKA HATARI

Na JOSEPH SHALUWA


MTU anaweza kufanya kazi au biashara fulani kwa muda mrefu asifanikiwe, lakini akija mwingine kwenye mazingira yaleyale akatusua! Hapo sasa ndipo kitu kinachoitwa nyota au mvuto hutambulika.

Katika tasnia ya burudani Bongo napo kuna wasanii ambao wameonekana kuwa na nyota kali kuliko wengine. Wakati mwingine, uwezo wa sanaa yao unawabeba huku wengine wakiwa na viwango vya kawaida kabisa lakini wanabebwa na nyota.

Mifano ipo mingi. Kuna wasanii wapo miaka nenda rudi kwenye game, lakini wapo vilevile, lakini kuna wengine wanaingia kama chipukizi na wanampita na kumuacha palepale.

Kuna wasanii ni wa muda mrefu, lakini hawachuji. Hata kama wakipotea kwenye game kwa muda mrefu, akirudi na kufanya kazi moja tu, anarudi juu tena kama vile alikuwa ulingoni siku zote.

Hiyo ni kwa sababu moja tu; nyota kung’aa. Wapo wasanii wengi wa aina hiyo Bongo. Lakini leo Swaggaz linakudondoshea mastaa wafuatao ambao wapo juu zaidi.

WEMA SEPETU

Alitambulika kwa kofia ya Miss Tanzania 2006 ambapo ushindi wake ulikuwa wa kishindo kikuu akiwa kwenye ushindani mkubwa na Jokate Mwegelo, Lisa Jensen na Irene Uwoya. Hawa walikuwa warembo moto kuwemo katika Top 5 ya Miss Tanzania ya mwaka huo.

Hata hivyo Wema amekuja kupata heshima kubwa zaidi alipoingia kwenye uigizaji. Nyota ya Wema ilianza kuonekana tangu aliposhiriki filamu yake ya kwanza kabisa, A Point of No Return akiwa na marehemu Steven Kanumba.

Baada ya hapo Wema ameendelea kufanya vizuri kwenye filamu za Kibongo, huku akitajwa kama miongoni mwa mastaa 10 Bora wanaotamba kwenye tasnia hiyo. Ukitazama Filamu ya DJ Ben, White Maria, 14 Days, Red Valentine utaelewa kwa nini anapewa sifa hizo.

Nje ya game, Wema ametokea kuwa na mashabiki wengi wanaomfuata kwenye kurasa zake katika mitandao ya kijamii. Anao wafuasi wake (Team Wema) ambao wamejenga umoja wa kumsapoti kwenye kila jambo. Hata kama akifanya jambo baya, Team Wema wamekuwa mstari wa mbele kumtetea.

IRENE UWOYA

Ni Miss Tanzania no. 5 mwaka 2006. Ametoka wakati mmoja na Wema. Naye aliamua kuingia kwenye filamu na akafanya vizuri. Pamoja na kuwakuta wakongwe kwenye tasnia hiyo, lakini yeye amekuwa miongoni mwa wasanii wa kutegemewa na wanaolipwa ghali zaidi kwenye tasnia hiyo.

Siku za karibuni, Uwoya amekuwa haishi vituko katika mitandao ya kijamii, lakini kutokana na nyota na kukubalika kulikopitiliza kwa mashabiki wake, wengi wanamtetea.

Ikiwa atatumia fursa hiyo vizuri, ana uwezo wa kutengeneza fedha nyingi kutokana na kipaji chake, lakini pia kwa sababu ana wafuasi wengi wanaomuunga mkono.

Uwoya ameshiriki filamu nyingi, akivaa uhusika tofautitofauti, lakini sinema mbili – O’prah na Off-Side zinaendelea kulinda heshima yake siku zote.

Sinema hizo ni chemistry ya aina yake, ikiwashirikisha wasanii wakali kama Jacob Stephen ‘JB’, Vincent Kigosi ‘Ray’, Emmanuel Myamba na marehemu Steven Kanumba.

MILLAD AYO

Historia yake inaonyesha alianza kazi ya utangazaji kwa msoto mkubwa, lakini hakukata tamaa. Wadau walianza kumwelewa Millard baada ya kuanza kutangaza Kipindi cha Milazo 101 ndani ya Radio One.

Baadaye mwaka 2010 alipojiunga na Clouds Media Group ndipo moto wake ulipozidi kwenye Vipindi vya Amplifaya na Clouds Fm Top 20. Juhudi za Millard hazikuishia kwenye kituo chake cha kazi pekee, alijiongeza na kufungua website na TV ya mtandaoni iitwayo Ayo TV.

Anayo team kubwa, ukijaribu kumsema vibaya utapambana na team yake inayomsapoti na kumfuata kwenye kurasa zake katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

DIAMOND PLATNUMZ

Stadi wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ anafahamika kwa uwezo wake jukwaani, lakini pamoja na hilo, siyo siri kuwa nyota yake ndiyo inayombeba.

Mbali na muziki, Diamond ana miradi kadhaa ikiwemo manukato ya Chibu, Diamond Karanga, Wasafi TV, Wasafi Record na mtandao wa wasafi.com.

Ingawa nyota yake inaonekana kung’ara lakini Diamond ni msanii wa kujiongeza, anajua kuwaweka karibu mashabiki wake, ambao ndiyo wanamsapoti kwenye kazi zake.

Tukio la hivi karibuni kugawa fedha kama mkono wa Idd katika Sikukuu ya Eid Elfitri, nyumbani kwao Tandale, Dar ni kati ya matukio yanayomuunganisha na jamii na kumfanya azidi kukubalika kwenye jamii yake.

ALI KIBA

Ni msanii wa kitambo, amewaacha wenzake wengi pembeni, lakini yeye ameendelea kung’ara. Hata alipoamua kupumzika kwa muda masuala ya muziki, aliporejea alikuwa na kishindo kikubwa kiasi cha kuwekwa levo moja na Diamond ambaye alikuwa juu peke yake.

Mpaka sasa Kiba ndiye msanii pekee ambaye anapimana ubavu na Diamond. Achana na vibao vyake Aje, Dushelele kwa sasa Mvumo wa Radi unazidi kumuweka pazuri.

Kwa upande wa biashara, anacho kinywaji kiitwacho Mofaya Energy, ikiwa ni ushirikiano na Dj maarufu kutoka nchini Afrika Kusini, Dj Sbu.

JOKATE MWEGELO

Mbali na urembo ana vipaji vingi, ikiwemo ujasiriamali. Ni miongoni mwa wasanii wachache walioshtuka mapema na kuacha kutegemea sanaa.

Jokate ambaye mwaka 2017 alitajwa na Jarida la Fobers Afrika, ameweza kubadilisha jina lake la utani na kuwa bidhaa na sasa ana Kidoti Company ambayo inajihusisha na utengenezaji wa nywele, viatu, mikoba, vifaa vya shule nk.

Mbali na yote hayo amejikita katika kusaidia watoto wa kike kujiamini katika kutimiza ndoto zao. Kama ni umisi walikuwa wengi, kama ni filamu aliwakuta wengi, lakini kutokana na nyota yake kuwaka, mpaka sasa bado ni lulu katika anga la burudani.

STEVE NYERERE

Komediani huyu wa kitambo ambaye jina lake halisi ni Steven Mengele, kukubalika kwake si tu kwa mashabiki bali hata wasanii wenzake. Ushawishi wake katika kuratibu mambo kunamfanya aendelee kuwa juu licha ya wachekeshaji wengine wengi kuingia kwenye fani hiyo miaka ya hivi karibuni.

Amekuwa kiongozi wa Bongo Movie kwa muda mrefu, wasanii wenzake humpa nafasi ya kupanga mambo shughuli mbalimbali ikiwemo sherehe au misiba inayowahusu ndugu au wasani wenyewe.

WENGINE

Mastaa wengine na fani zao kwenye mabano ni Lucas Mhuvile ‘Joti’ (komediani), Masoud Kipanya (mtangazaji), Rose Muhando (mwimbaji wa Injili), Judith Wambura ‘Jide’ (mwanamuziki), Jacob Stephen ‘JB’ (mwigizaji) na Amri Athumani ‘King Majuto’ (komediani).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,204FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles