25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mchango wa NMB ujenzi wa taifa waikosha serikali

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

Serikali inaridhishwa na jinsi Benki ya NMB inavyozihudumia tawala za mikoa na serikali za mitaa pamoja na taifa kwa ujumla huku ikiipongeza taasisi hiyo kiongozi ya fedha nchini kwa mchango wake katika ujenzi wa taifa.

Hiyo ni kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, na viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT)-Tanzania ambao wamesema nafasi ya NMB kwenye maendeleo ya nchi ni nyeti na ya kimkakati.

Akiwa kwenye banda la benki hiyo kabla ya kuufungua rasmi mkutano mkuu wa mwaka wa ALAT, Dk. Mpango alisema huduma za NMB kwa halmashauri zimekuwa na manufaa makubwa hasa mikopo.

Hata hivyo kiongozi huyo ameshauri ukopeshaji huo uwe ni wa tija ili kuepuka uwezekano wa kuwepo mikopo chechefu ambayo mwisho wa siku itakuwa mzigo kwa serikali.

“Mnafanya vizuri na tunafurahia mnavyozihudumia halmashauri zote nchini ila umakini unahitajika mnapozikopesha ili kuepuka mikopo chechefu,” alisema Dk. Mpango baada ya kumsikiliza, Vicky Bishubo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Biashara za Serikali.

Afisa huyo alimwambia Dk. Mpango kuwa NMB imeunganishwa kidijitali na halmashauri zote na taasisi zaidi 1,100 katika swala zima la kuzisaidia kukusanya mapato. Alisema pamoja na kuwa na mahusiano makubwa na halmashauri hizo pia NMB ni mshirika mkubwa wa serikali na mdau wake muhimu wa maendeleo.

“Kama kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu wa ALAT inavyochagiza, sisi tumejipanga kushirikiana na Tamisemi kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato,” Bi Bishubo alibainisha.Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa ALAT Taifa 2020 ni:

“Kuongeza Tija Katika Ukusanyaji na Matumizi Bora ya Mapato Katika Halmashauri ni Msingi wa Maendeleo Endelevu kwa Wananchi,” amesema.

Akihutubia mkutano huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema wana mifumo bora na rahisi ya kusaidia ngazi zote za Serikali kukusanya mapato.

Na kati ya mwaka 2018 na 2021 benki hiyo imefanikisha makusanyo yenye thamani ya Sh trilioni 9.6.Bi Zaipuna alisema NMB pia ni mlipa kodi mzuri ikichangia zaidi ya Sh trilioni 1.2 kwenye eneo hilo ndani ya miaka saba. Kwa upande wa gawio, kiasi ilichopata Serikali katika kipindi hicho ni TZS bilioni 121.5 ambapo TZS bilioni 30.7 zilitolewa mwaka huu.

“Tunajivunia kuwa mshirika mkubwa wa maendeleo ya taifa letu na tunaahidi kuendelea kujitoa zaidi kwa maslahi makubwa ya taifa letu. Siku zote tupo tayari kuihudumia serikali, tupo tayari kuwahudumiwa watumishi wa umma na tupo tayari kuwahudumia Watanzania wenzetu,” amesema Zaipuna.

Mbali na kusaidia kukusanya mapato ya Serikali, Bi Zaipuna alisema NMB inashiriki kwenye maeneo mengine ya ujenzi wa taifa ikiwemo kusaidia jamii kwa kurejesha sehemu ya faida yake kwa jamii kupitia hasa uwekezaji kwenye elimu na afya.Pia benki hiyo ni kinara wa kuwakopesha watumishi wa umma ambapo mwaka jana mikopo iliyotolewa ni ya kiasi cha Sh trilioni 2.94. Wakulima na wafugaji pamoja na mnyororo mzima wa nyanja hizo wanafaidi mikopo ya riba ya asilimia tisa tu.

Zaipuna alisema mwaka huu tayari wameshatoa zaidi ya Sh 509 kama mikopo katika sekta hii muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.

Wanufaika wengine wa mikopo ya NMB ni wakandarasi wanaosaidia kuboresha miundombinu kwenye halmashauri ambao 564 kati yao wamekopeshwa zaidi ya Sh bilioni 45.Mkuu huyo alisema pia NMB imekuwa mshiriki mkubwa katika miradi ya kimkakati ambako imechangia kiasi cha Sh trilioni 1.14 kupitia mikopo na dhamana mbalimbali.

Miradi hiyo ni kama ule wa maji Tabora, Igunga na Nzega, ujenzi wa reli wa SGR na vipuri vya mradi wa umeme wa Kinyerezi I.

Pia ipo miradi ya REA, ule wa Mabasi ya Mwendokasi, vipuri vya gati bandarini na ukarabati wa mtambo wa maji wa DAWASA.“Kuna pia kusaidia makundi maalum kama wamachinga, bodaboda na mama na baba lishe. Tunatambua makundi ya wafanyabiashara wadogo katika halmashauri zetu na hivyo Benki ya NMB imebuni masuluhishi bora kwa makundi haya na tayari tumetenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya mikopo rafiki kwa sekta hii,” amesema Zaipuna.

Eneo jingine ambalo NMB imekuwa mstari wa mbele katika kulihudumia taifa ni utoaji wa elimu ya fedha. Aidha, benki hiyo imeanzisha asasi maalum ya kiraia ya NMB Foundation itakayosaidia kwenye sekta za Elimu, Afya, Ujasiriamali na Mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles