28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango apongeza Stendi ya Nyamhongolo huku akitoa onyo…

Na Clara Matimo, Mwanza

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Stendi mpya ya mabasi na maegesho ya malori Nyamhongolo huku akitoa onyo kwa watumishi wa umma kutojilimbikizia vyumba vilivyotengwa kwa ajili ya wananchi kufanyia biashara na kuagiza kuondoa urasimu katika mchakato wa ugawaji vyumba hivyo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango (wa pili kulia) akizindua stendi mpya ya mabasi na maegesho ya malori Nyamhongolo katika halmashauri ya manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza. Wa pili kushoto ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela.

Dk. Mpango ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza alitoa agizo hilo Septemba 13, 2022 wakati akizungumza na wananchi waliofurika katika uwanja wa stendi hiyo baada ya kuizindua rasmi huku akiwataka wananchi watakaotumia stendi hiyo kutunza miundombinu iliyopo kituoni humo ikiwemo mifumo ya maji na umeme ili iweze kutumika kwa muda mrefu.

Amesema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya viongozi kutumia nyadhifa zao kushikilia maeneo mengi hali inayosababisha walengwa kukosa ama kuwekewa vikwazo kukosa vyumba hivyo wakati serikali inatekeleza miradi kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wake ili waitumie kupata kipato na kulipa kodi zitakazotumika katika miradi mingine ya maendeleo.

“Mkuu wa mkoa hakikisha kuna uwazi katika utaratibu utakaotumika kutoa vyumba  hivyo na kwa kuwa mimi ndiyo nimefungua rasmi kituo hiki cha mabasi nawambieni nitafuatilia na kuhakikisha hakuna upendeleo katika ugawaji wa vyumba vya biashara na utaratibu uwe jumuishi uzingatie makundi maalumu hususani watu wenye ulemavu, vijana na wanawake,”aliagiza Dk. Mpango na kuongeza:

 “Hakikisheni  uwepo wa huduma madhubuti za kukabiliana na majanga kama moto, pawepo huduma ya kwanza pamoja na utaratibu mzuri wa kukusanya taka ikiwemo vifaa na teknolojia zinazofaa katika kukusanya na udhibiti wa taka, wekeni ulinzi imara ili kuimarisha usalama wa watu na mali zao hususani wageni na wasafiri watakaotumia kituo hiki,”.

Pia Dk Mpango aliwaagiza viongozi wa halmashauri zote kuweka nguvu katika kukusanya mapato ya ndani huku akiwataka kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa kwani atakayejaribu kudokoa asije kunung’unika maana Rais Samia Suluhu Hassan alikwishasema anazungumza kwa kalamu.

Awali, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary akisoma taarifa ya mradi huo kwa mgeni rasmi Dk. Mpango alisema ulianza kutekelezwa Julai 30, 2017 na kukamilika Agosti 2022 ukigharimu Sh bilioni 26.645 ambapo utaongeza mapato ya halmamashauri ikikadiriwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 2.232 kwa mwaka.

Pia, utavutia wawekezaji, kuongeza idadi ya wafanyabiashara, kuboresha mazingira ya usafiri na usafirishaji kwa abiria na mizigo kwa wananchi wa mikoa mingine na nchi jirani na kuongeza fursa za ajira zaidi ya 1,300 kwa wakati mmoja.

“Mradi huu umesheheni miradi mbalimbali ikiwemo jengo la abiria lenye maduka makubwa 10, vibanda vya kukatia tiketi vya mabasi 46, benki mbili, supermarket mbili, migahawa mitatu, maduka madogo 72 na eneo la kuegesha mabasi 120 kwa wakati mmoja. Jengo la biashara lina maduka 32 na eneo la maegesho ya malori lina maghala manne ya kuhifadhia mizigo, gereji moja ya kisasa, sehemu ya kuegesha malori zaidi ya 80 kwa wakati mmoja na hosteli yenye vyumba vya kulala wageni 100,”alisema Apolinary.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima alisema kukamilika kwa mradi huo kutaisaidia halmashauri na taasisi za serikali kupunguza utegemezi wa bajeti ya serikali kuu pia kutawezesha mkoa kufikia malengo ya ukusanyaji mapato kutoka  Sh bilioni 45 hadi 53 ambazo ndiyo lengo kwa mwaka huu  na hatimaye 60 baada ya miaka mitatu.

“Kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Mwanza namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha nyingi katika mkoa wetu kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hadi hivi sasa mkoa umepokea kiasi cha zaidi ya Sh blioni 408 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati tunaahidi kuitunza miradi hiyo,”alisema  Malima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles