Na FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM
UANZISHAJI wa Mwalimu Commercial Bank mwaka mmoja na nusu uliopita, ni uamuzi uliokuwa unasubiriwa na tasnia ya ualimu kwa muda mrefu ili kuondokana na matatizo mbalimbali ya kiuchumi yanayowakabili walimu wengi mijini na vijijini.
Hali hiyo ni kutokana na kilio cha walimu kufanya kazi kwenye mazingira magumu kwa muda mrefu, huku mishahara na masilahi mengine kuwa madogo, jambo ambalo limekuwa likiwafanya kuishi maisha duni kuliko wafanyakazi wengine wa Serikali na taasisi nyinginezo za umma.
Ni ukweli usiopingika kwamba, licha ya walimu kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi hasa wafanyao kazi vijijini, bado wameshindwa kupata muda na mtaji ili kupata mapato ya ziada na waweze kujikimu au kufanya maendeleo ya taaluma yao.
Wazo la kuanzishwa Benki hii ni walimu wenyewe walioona umuhimu wa kuanzisha chombo hicho, baada ya baadhi yao kuzidiwa na mzigo wa madeni yaliyotokana na mikopo kutoka benki mengine ili kujiendeleza kimaisha, hivyo pamoja na huduma hizo lakini zimewaongezea mzigo wa madeni.
Kuanza kwa MCB kumeleta matumaini mapya kwa vile itawasaidia waalimu kuwa na maisha bora, kwani licha ya kuwa wateja wa benki pia ni wanahisa wa benki hiyo. Hivyo uongozi wa benki kuhakikisha wanatengeneza faida na pia ina bidhaa zinazowanufaisha wateja wao mahsusi, walimu ambao wengi wao wapo vijijini.
Itakumbukwa kuwa walimu wengi hapo zamani hasa wa vijijini walilazimika kusafiri hadi mijini kufuata huduma za fedha ikiwemo mishahara. Lakini hivi sasa huduma jumuishi za fedha zimeweza kusogeza huduma hadi ngazi za chini na hivyo kupata huduma hiyo.
MCB imeanza wakati huduma hii imezagaa nchini nzima na pia ina wateja wake kila pembe ya nchi hadi mipakani. Huu ni mtaji mkubwa na mhimili wa benki kujenga mazingira bora ya kutengeneza faida ya benki hiyo na kuinua hali ya uchumi ya wanahisa wake.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu, Ronald Manongi, anasema mtaji uliotumika kuanzisha Benki hiyo ni Sh bilioni 31.
Anasema mtaji huu ni mkubwa, ni karibu mara mbili ya kiwango cha chini kinachotakiwa ili Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iweze kutoa leseni.
“Uhitaji wa uanzishwaji benki ulionekana tangu awali hasa baada ya Uongozi wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kuisajili kwenye Soko la Hisa na kwa muda mfupi kukusanya mtaji haraka,” anasema Manongi.
Anasema wanahisa wengi wa benki hiyo ni mwalimu mmoja mmoja na kwamba ni dhahiri MCB ilianza shughuli zake sambamba na mfumo wa kisasa wa kimataifa wa kutoa huduma za kifedha jumuishi.
Mwalimu mmoja mmoja anamiliki hisa za benki asilimia 35.28; wakifuatiwa na wananchi kwa ujumla, 16.19, mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF na NHIF, asilimia 16.17 kila mmoja; Chama cha Walimu (CWT) asilimia (12.94 na Kampuni ya Maendeleo ya Walimu (Teachers’ Development Company Ltd) ina asilimia 3.23.
Huduma jumuishi ni ile inayowaunganisha watu wa kipato cha chini katika mfumo wa kibenki na kunufaika na matumizi rafiki ya mtandao wa kidigitali kwa gharama nafuu na usalama wa miamala hiyo.
Mkurugenzi Mkuu huyo anasema wakati menejementi ya MCB inajitahidi kuwa na mikakati ya kuikuza benki hiyo ili kuwafikia walimu wengi waliotapakaa kila kona ya Tanzania, bado inakabiliwa na ushindani wa vyombo vya fedha vilivyowakopesha walimu hao kuendelea kuwashikilia ili waendelee kuwa wateja wao kwa hofu ya kupunguza wateja wao.
“Ni wajibu wa Serikali kuwa karibu na Benki hii ili kuunga mkono juhudi za uwekezaji wa ndani uliofanywa na waajiriwa wao. Kwa kufanya hivyo itaweza kuwasaidia wananchi wake kuboresha maisha ya wananchi wake na faida itokanayo na benki hiyo itaweza kusaidia jamii kwa kuelekea uchumi wa kati,” anasema Manongi.
Anasema maamuzi mengi yanayoweza kufanywa na Serikali kuisaidia benki hiyo kukua haraka likiwemo lile la kupitishia mishahara ya walimu kwenye benki yao.
Manongi anasema mbali na njia hiyo, pia malipo mengine yakiwemo madeni wanayoidai Serikali yangeweza kuwapa morali walimu ili
kuendelea kuitumikia nchi yao kwa moyo mmoja.
Anatoa pongezi kwa manejimenti ya MCB kwa kufikia makubaliano ya kufanya kazi pamoja na Benki ya Posta (TPB) kwa kile anachodai hizi ni benki za kizalendo, hivyo lazima tukubali kuwa benki zinazoanzishwa na Watanzania kwa manufaa ya Watanzania lazima zikidhi haja ya Watanzania.
“Ushuhuda kutoka kwa wateja, wanasema wanapotaka kuongeza amana kwenye akaunti zao, huenda tawi la Benki ya Posta lililoko jirani na kujaza fomu. Mara karani wa benki anapomaliza kuingiza taarifa za mteja kwenye kompyuta, hapo kwa hapo muamala umekuwa umekamilika kupitia kwenye mtandao,” anasema mkurugenzi huyo.
Anazitaja huduma zinazotolewa na MCB kuwa mikopo kwa mtu mmoja mmoja na makundi madogo madogo, jambo ambalo anasema linawavutia wateja wengi ni masharti rahisi ya upatikanaji wa mikopo ili kukidhi mahitaji ya mwombaji.
“Mikopo inaambatana na masharti rahisi na inaweza kulipwa kwa kipindi cha miezi 72,” anasema Manongi.
Akizungumzia mipango ya baadaye ya benki hiyo, Manongi anasema wamedhamiria kuwafikia wananchi wenye kipato cha chini ambao ndio tegemeo la ukuaji wa benki hiyo.
Anasema kwa sasa maombi ni mengi na kinachosubiriwa ni kibali cha Benki Kuu ya Tanzania kutekeleza mikakati hiyo kutokana na kuwa benki ipo imara.
“MCB si benki pekee ya walimu duniani, kuna mabenki mengine kama hayo nchi nyinginezo zikiwemo zile zilizoendelea. Ni vyema menejementi ya Benki ikaangalia namna ya kujifunza kutoka huko ili kuboresha benki hii na ikiwezekana kuhamisha teknolojia na mifumo ili ziweze kuijenga MCB kuwa ya kisasa zaidi,” anasema mkurugenzi huyo.
Anasema jukumu jingine la Menejimenti ya MCB ni kutayarisha mkakati wa mawasiliano na kujitangaza hasa kwa wananchi wa vijijini, ambapo kuna mahitaji makubwa ya huduma za benki ili kwenda sambamba na mfumo uliozinduliwa na Benki Kuu hivi karibuni wa mpango wa huduma jumuishi za fedha kufika vijijini.
Anatoa wito kwa wanahisa ambao ni walimu kwani wamekuwa wakitumika katika kampeni mbalimbali za kitaifa, hivyo ni vyema kama wanahisa wakaunga mkono na kuwasiliana na menejimenti ya benki kuhamasisha wananchi kujiunga na benki yao ili kuinua hali za maisha yao.
Manongi anasema ni vyema MCB ikaangalia huduma za kifedha ambazo zinalenga kuwekeza kwenye elimu ili kuinua viwango vya elimu ya wanahisa na familia zao ambapo mara nyingi tunashuhudia baadhi yao wakihangaika kutafuta mikopo kwa ajili ya kugharamia ada za mafunzo ya familia za wanahisa katika ngazi mabalimbali za elimu.