MILTON KEYNES, UINGEREZA
WANASAYANSI nchini Uingereza na Gambia wamesema wana ushahidi wa awali unaoonesha kuwa mbwa wanaweza kunusa malaria.
Wanasayansi hao wamewafunza mbwa kutambua harufu ya malaria kwa kutumia nguo za watu wenye maambukizi.
Kuna matumaini makubwa kuwa wanyama hao watatumika katika mapambano dhidi ya malaria na hatimaye kuutokomeza ugonjwa huo.
Japokuwa utafiti huo upo katika hatua za awali, wanasayansi wanaamini matokeo yake yanaweza kubadili namna ya kutumia vipimo vya malaria.
Kwa mujibu wa tafiti za hapo awali, mtu ambaye ana vimelea vya malaria mwilini anakuwa na harufu tofauti ambayo inawavutia mbu kuendelea kumshambulia. Na kwa sababu hiyo, mbwa wapo kazini kuinusa harufu hiyo.
Soksi zilizovaliwa na watoto usiku kucha katika jimbo moja nchini Gambia, zilisafirishwa hadi Uingereza kufanyiwa uchunguzi.
Kati ya jozi 175 zilizotumwa katika Wakfu wa Mbwa wa Ugunduzi wa Tiba mjini Milton Keynes, 30 zilikuwa zimevaliwa na watoto wenye vimelea vya malaria.
Mbwa hao wenye uwezo mkubwa wa kunusa pia wapo kwenye mafunzo ya kunusa harufu ya saratani na ugonjwa hatari wa kukakamaa (Parkinson’s disease).
Matokeo ya jumla, ambayo yalitolewa katika Mkutano wa Mwaka wa Jumuiya ya Amerika ya Magonjwa ya Kitropiki na Usafi yanaonesha kuwa kati ya watoto 10 walioathirika, mbwa wana uwezo wa kutambua watoto saba.
Lakini pia walifanya makosa kwa kudhani kuwa mtoto mmoja ana maambukizi kati ya 10 ambao wapo salama.
Mtafiti Mkuu Profesa Steve Lindsay kutoka Chuo Kikuu cha Durham, alisema wana furaha kubwa juu ya matokeo hayo, lakini mbwa hao bado hawajawa tayari kutumika kila siku.
Watafiti bado wanahitaji muda zaidi kuboresha umakini wa mbwa na kuanza kunusa watu badala ya soksi.
Pia wanata kujiridhisha kama mbwa wanaweza kutambua aina tofauti za malaria.
Lengo ni kutumia mbwa hao siku moja katika viwanja vikubwa vya ndege ili kuzuia maambukizi.
Utumiaji wa wanyama hao pia utakuwa ni hatua kubwa katika kutokomeza ugonjwa huo sababu haitasubiriwa hadi mtu aoneshe dalili ndipo afanyiwe vipimo kama ilivyo kwa sasa.