32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 1, 2023

Contact us: [email protected]

Wito watolewa kukabili vifo vya wajawazito Afrika

NAIROBI, KENYASERIKALI za mataifa ya Afrika zimetakiwa kujitolea kwa hali na mali ili kukabili vifo vya wajawazito na watoto ifikapo mwaka 2030.

Hayo yalisemwa katika Kongamano la Pili la Kimataifa la Afrika lililoanza mjini hapa juzi na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa 25 na washirika wapatao 1,000.

Kongamano hilo linajadili njia bora na salama za kina mama kujifungua.

Akifungua kongamano hilo, Margaret Kenyatta ambaye ni mke wa Rais Uhuru Kenyatta, alisema upo uwezekeno mkubwa wa kukabili vifo vya wajawazito na watoto ifikapo mwaka 2030 iwapo njia mbadala zitachangiwa na Waafrika wenyewe.

Kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa nchini Kenya, 22 hufariki dunia kabla ya kufikisha mwezi mmoja huku 193,000 wakizaliwa kabla ya siku zao.

“Kaulimbiu ya leo inakwenda sambamba na mikakati yangu ya kupunguza idadi ya vifo kwa wanawake wanaojifungua na kila mtoto anastahili kuishi zaidi ya miaka mitano.

“Ni vita ambavyo nimekuwa nikipigana navyo kwa muda wa miaka mitano sasa, na leo naongezea sauti yangu kwenye vita hivi, naamini kuwa kila mama na kila mtoto anastahili kuishi na kushamiri,” alisema Margaret.

Serikali ya Uingereza imetoa dola milioni 15 kwa mpango wa kupunguza vifo vya kina mama wanaojifungua nchini hapa.

Kongamano hilo linafuatia lile ambalo lilifanyika Afrika Kusini miaka mitano iliyopita, huku wanawake 550 wakiripotiwa kufa kila siku kutokana na matatizo ya ujauzito katika mataifa yaliyoko chini ya jangwa la Sahara.

Kenya imetajwa kuwa mfano kwa mataifa mengine ya Afrika huku mfumo wa ugatuzi ukichangia kuboresha sekta ya afya mashinani, hasa katika majimbo yaliyoko kaskazini ambayo yalikuwa na viwango vikubwa vya vifo vya wajawazito na watoto kutokana na uhaba wa vifaa.

Tume ya ya Umoja wa Afrika ambayo inafadhili kongamano hilo pamoja na Serikali ya Kenya imesema inashirikiana na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo Afrika na Shirika la Chakula Duniani pamoja na wake wa marais wa bara la Afrika kuhamasisha wananchi wa mataifa husika ili kupunguza vifo hivyo.

Kongamano hilo la siku tatu litajadili masuala mengine yakiwemo uongozi, uwajibikaji, virusi visababishavyo Ukimwi miongoni mwa watoto pamoja na ndoa na mimba za mapema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles