ALIYEKUWA Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Simiyu, Gimbi Masaba (Chadema), wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka.
Mwingine aliyekuwamo katika gari hilo lenye namba za usajili T 397 ASB Toyota Pick Up, ni mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima mkoani Mwanza, Sitta Tuma.
Ajali hiyo, ilitokea jana saa 3 asubuhi katika eneo la Magereza nje kidogo ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu.
Watu hao walikuwa wakitoka jijini Mwanza kwenda mjini Bariadi kwenye shughuli zao za kawaida. Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Wenje.
Akizungumza na MTANZANIA, Wenje alisema licha ya gari walilokuwa wakisafiria kuharibika vibaya, hakuna mtu aliyeumia.
“Tunamshukuru Mungu kwa mapenzi yake ametuokoa, ilikuwa ajali mbaya na imetokea tunaiona hivi. Gari imeharibika mbele tumenusurika.
“Chanzo cha ajali ni barabara ya lami kuwa na kokoto nyingi zilizosababisha gari kuyumba ghafla, baadaye likanishinda,”alisema Wenje.
Naye Gimbi alishauri kokoto zilizomwagwa kwenye barabara hiyo kutoka Lamadi kwenda Bariadi mjini ziondolewe, ili kuepusha uwezekano wa ajali za aina hiyo kutokea.
Alisema kokoto hizo zimekuwa zikisababisha ajali kutokana na magari kuyumba na kuseleleka mitaroni.
Kwa upande wake, Sitta alisema baada ya ajali hiyo aliendelea na majukumu yake.
“Unajua kokoto hizi ukikata kona kidogo tu, lazima uhame na kuteleza kama goroli. Wenje alijitahidi sana kuicontrol (kuidhibiti) gari, lakini iliyumba barabara nzima karibu mara tatu, kisha ikaparamia mtaro ikaviringika,”alisema Sitta.