Na ELIZABETH HOMBO – DODOMA
MBUNGE wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hillary (CCM), ameitaka Serikali iwalipe fidia wafanyabiashara wa viroba kwa sababu utaratibu wa kuzuia ulikuwa wa ghafla.
Aeshi alitoa kauli hiyo jana jioni wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Makamu wa Rais (Mazingira) kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Alisema kabla ya operesheni ya kuondoa viroba ni vyema serikali ingetoa muda kwa wafanyabishara hao kujipanga na kuuza bidhaa hizo kwa kuwa wengine walikopa mikopo benki.
"Binafsi ninajua uchungu wa mtu kufilisika, Serikali iwalipe fidia hawa wafanyabiashara kwa sababu wamepata hasara kubwa na tulisikia kuna mfanyabishara alijiua kwa sababu alikuwa amechukua mkopo benki.
"Inakuwaje biashara ilikuwa halali halafu ghafla serikali inazuia ni bora tungewapa nafasi,'alisema Aeshi.
Kutokana na hilo, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alitoa taarifa kwa mwenyekiti wa Bunge, akisema: "Mheshimiwa mwenyekiti anachokisema Aeshi ni sahihi kabisa ninamuunga mkono,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Muungano na Mazingira, January Makamba, alisema taarifa za kupiga marufuku viroba ilitolewa Mei mwaka jana, mpaka hatua zinachukuliwa ilikuwa ni miezi 10 imepita.
Alisema mbali na marufuku hiyo baadhi ya watu waliendelea kuingiza mitambo ya kutengeneza bidhaa hiyo kwa mazoea kwamba, Serikali hutoa tamko bila kuchukua hatua.
“Ukiwa na taarifa alafu ukaingiza mzigo ni kujitakia mwenyewe,” alisema Makamba.
Pamoja na hatua hiyo alisema, Serikali itazidi kufanya mazungumzo na wafanyabiashara ili kuona namna nzuri ya kutatua jambo hilo.