28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

MWANASHERI MKUU WA SERIKALI, UPINZANI WAVUTANA

Na Fredy Azzah – Dodoma    


      

MSEMAJI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Ally Saleh (CUF), jana alilazimika kutomaliza kusoma hotuba yake akisema Bunge halina uhuru.

Saleh alifikia uamuzi huo baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu kumtaka kuruka kurasa kadhaa kwa madai zinazungumzia mambo yaliyopo mahakamani.

Kabla ya uamuzi huo, Saleh alikatishwa mara kadhaa kusoma hotuba yake na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, aliyekuwa akipinga baadhi ya maneno yaliyokuwamo ambayo yalionekana kumkera.

 

MVUTANO ULIVYOANZA

AG alianza kusimama mwazoni mwa hotuba ya Saleh, wakati mbunge huyo akiwa ukurasa wa pili alipokuwa akizungumzia kutotekelezeka kwa bajeti.

Akisoma eneo hilo, alisema: “Hii ni bajeti ya pili tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ambapo Rais John Magufuli, ameshika uongozi wa nchi.

“Imekuwa ni bajeti ngumu kutekelezeka kwa ushahidi wa fedha zilizotolewa, ikilinganishwa na zile zilizotengwa. Kila wizara imekiona cha moto, maana wamebanwa mpaka wamevunjwa mbavu.”

Baada ya maelezo hayo, Masaju alisimama na kumwomba mwenyekiti utaratibu akisema msemaji anasema uongo na kutumia lugha isiyofaa, hivyo kutaka maneno ‘wamebanwa mpaka wamevunjwa mbavu’ yasiingie kwenye kumbukumbu za Bunge.

Kabla ya kukaa, alianza pia kuzungumzia nia yake ya kutaka maneno yaliyo katika ukurasa wa tatu wa hotuba hiyo, yanayozungumzia Rais Dk. Ali Mohamed Shein kukalia kiti kisicho chake yaondolewe.

Kabla hajafika mwisho, Zungu alimtaka kuketi, kisha kumpa nafasi Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), aliyesema Masaju anavunja kanuni za Bunge kwa kuwahisha shughuli za Bunge kwa kuzungumzia mambo ambayo bado hayajafikiwa.

Baada ya maelezo hayo, Zungu alisimama na kuamuru maneno ‘wamebanwa mpaka wamevunjwa mbavu’, yasiingizwe kwenye kumbukumbu za Bunge kisha aliruhusu Saleh kuendelea na hotuba yake.

Aliporuhusiwa kuendelea na hotuba yaje, Saleh alisema katika kutokutolewa kwa fedha za bajeti zilizotengwa na Bunge, eneo la miradi ya maendeleo ndilo lililoumia zaidi.

“Eneo la miradi ya maendeleo limeumia zaidi, maana huko asilimia zilizopelekwa mpaka zinatia aibu kutajwa hadharani, au tunaweza kusema haijawahi kutokea.

“Na kama kuna watu wanasema kuna hatua iliyopigwa katika miradi, basi itakuwa ni ile iliyopendelewa na kiongozi wa nchi, lakini sio ile ambayo Bunge ilipangia kutekelezwa na ile ambayo inagusa maisha ya kila siku ya mwananchi.

“Katika hali hii, ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa mwathirika mkubwa wa kisu cha ngariba. Fedha ilizoweza kushushiwa hazifanani na hadhi ya ofisi hii, au hata kukatiwa fedha au kupunguziwa, haipendezi,” alisema Saleh.

Baada ya maelezo hayo, Majasu alisimama tena na kutaka maneno “kisu cha ngariba” yaondolewe kwa maelezo kwamba ni uongo, kwani ngariba hatoi fedha.

Baada ya kukaa, Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msingwa (Chadema), alisimama na kuomba kupewa utaratibu, akisema mfumo wa mabunge ya Jumuiya ya Madola, ambao ndio unaofuatwa na Tanzania, unataka wachache wasikilizwe na walio wengi waamue.

“Sasa sisi hapa tunatumia utaratibu upi kwa sababu hata maoni yetu hayasikilizwi,” alisema Msigwa.

Baada ya maelezo hayo, Zungu alisimama na kukubaliana na hoja ya AG ya kufuta maneno “kisu cha ngariba” katika kumbukumbu za Bunge.

Pia aliagiza maneno yaliyo katika ukurasa wa tatu na wa nne yanayohusu uhalali wa Dk. Shein kuwa Rais wa Zanzibar na yale ya ukurasa wa sita na saba, ya kile walichosema ni mbinu chafu za Msajili wa Vyama vya Siasa kuivuruga CUF, yote yarukwe na aanze kusoma kuanzia ukurasa wa 8.

Baada ya maelezo hayo, Saleh alipewa nafasi ya kuendelea na hotuba yake, lakini alikataa kwa kusema: “Kumbe freedom of parliament (uhuru wa Bunge) haipo tu that extent (kwa kiwango hicho).”

Alisema wakati anasimama kusoma hotuba yake, aliona namna mawaziri walivyokuwa wakiwasiliana, na akawaambia wabunge wenzake kwa hali hiyo lazima watamzuia.

“Naomba kuikabidhi (hotuba yake), aichane anavyotaka,” alisema Saleh na kwenda kukaa bila kumaliza kusoma hotuba yake hiyo yenye kurasa 59.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles