31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge Ngara aomba kuondolewa kazini DMO, Mfamasia

Na Allan Vicent, Ngara

Mbunge wa Jimbo la Ngara wilayani Ngara Mkoani Kagera, Ndaisaba Ruhoro, ameomba serikali kuwaondoa kazini Mganga Mkuu wa Hosipitali ya Wilaya (DMO), Mfamasia na Mtunza Stoo ya dawa kutokana na tuhuma za kuhusika na upotevu wa dawa za mamilioni ya fedha yaliyoletwa na serikali.

Akizungumza na vyombo vya habari jimboni humo leo Jumatatu, Machi 1, amesema kuwa Maofisa hao walikamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi kufuatia tume maalumu iliyoundwa na Wizara ya Afya kuja kuchunguza upotevu mkubwa wa madawa yanayoletwa na MSD kwa ajili ya wananchi.

Amesema kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, watumishi hao walipaswa kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi lakini cha kusikitisha hadi sasa watumishi hao bado wapo kazini.

“Kama Mbunge nimeshapokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakitaka kujua hatma ya suala hilo na wametishia kuchukua hatua dhidi ya maofisa hao kama wataendelea kuachwa hivi hivi na mimi na waunga mkono,” alibainisha.

Aidha, amefafanua kuwa wananchi wa Jimbo hilo wanaumia sana wanapoona zahanati, vituo vya afya na hospitali ya wilaya vinakosa madawa ya kutosha wakati serikali imekuwa ikileta dawa hizo kwa wingi.

“Wananchi wanaumia sana wanapoenda katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuambiwa dawa hakuna na hivyo kutumia gharama kubwa kununua dawa katika maduka binafsi,” amesema mbunge huyo.

Mbunge ameongeza kuwa kitendo cha watumishi hao kuendelea kuwepo kazini wakati suala hilo likisubiri maamuzi ya ngazi za kisheria kunaibua hali ya sintofahamu miongoni mwa jamii na viongozi wa wilaya.

Amemuomba Waziri wa Afya kuwaondoa kazini watumisha hao mara moja vinginevyo hasira za wananchi zitaendelea kuongezeka jambo linaloweza kupelekea kupigwa mawe watumishi hao.

Aidha, ameomba Mamlaka ya Famasia nchini kumfutia kibali Mfamasia huyo ikiwa ni pamoja na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kukiuka maadili ya utumishi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo, Luteni Kanali Michael Mntenjele amesema kuwa suala hilo ni la kiuchunguzi na liko mahakamani hivyo wanaiachia sheria ichukue mkondo wake.  

“Hili suala liko kwenye uchunguzi, siwezi kulizungumzia, tuviachie vyombo vya sheria vifanye kazi yake, kuhusu kuwaondoa kazini wahusika, waliotuma timu ya wataalamu kuja kuchunguza suala hilo ndiyo wenye maamuzi,” amesema. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles