30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE CHADEMA AWEKWA NDANI  

 

Na Mwandishi Wetu-MBEYA


MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Chadema), amepelekwa mahabusu kwa kile kilichoelezwa makahamani kuwa ni kwa usalama wake.

Hatua ya kupelekwa mahabusu mbunge huyo, imetokana na ubishani mkali wa kisheria ulioibuka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mbeya, baina ya mwanasheria wa Serikali, Joseph Pande na wakili wa upande wa utetezi, Sabina Yongo.

Sugu alifikishwa mahakamani hapo jana na mwenzake, Katibu wa Chadema Kanda, Emmanuel Masonga wakidaiwa kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Baada ya Sugu na mwenzake kusomewa mashtaka, Wakili Yongo, aliiomba mahakama iwape dhamana wateja wake jambo ambalo lilipingwa na Mwanasheria wa Serikali, Pande ambaye alidai kwamba licha ya kosa hilo kuwa na dhamana, aliomba mahakama isiwape kutokana na hali ya usalama wao.

Kutokana na mabishano ya kisheria, mahakama kupitia Hakimu Mkazi, Michael Mteite, ilikubaliana na hoja za mwanasheria wa Serikali kutowapa dhamana washtakiwa hao na uamuzi utatolewa Januari 19, mwaka huu kama watapewa ama la.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili Pande kuwa watuhumiwa wote wawili wanashtakiwa kwa kosa moja la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli kinyume cha sheria.

Pande alidai kuwa Desemba 30, mwaka jana, mtuhumiwa wa kwanza, Sugu, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge, alidaiwa kutoa maneno ya fedheha yakiwamo: “Kama Rais anataka kupendwa, asingemshuti Lissu, asingemfunga Lema miezi minne gerezani, asingemzuia Sugu asiongee hili au lile, kwa kuteka watu.

“Umemteka Roma, Ben Saanane mtoto wa watu hadi leo hatujui alipo.”

Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, Emmanuel Masonga, alidaiwa katika mkutano huo alitoa kauli kuwa “hali ya maisha imekuwa ngumu, kila kona mambo yamekaza, watu wanatekwa mchana kweupe, watu wanauawa na kufungwa kwenye viroba mchana kweupe.

“Rais Magufuli ameamua kubadilisha namna ya kutawala, yeye anaamini njia ya kutawala Watanzania ni kuwaua, kuwazuia wasiongee.

“Leo hii wanazuiwa, viongozi wa dini ndio wanaokwenda kuhakikisha nchi inakuwa na amani, lakini utawala huu wa awamu ya tano unawazuia viongozi wa dini wasizungumze na kuwaonya.”

Kwamba alidai katika mkutano huo kuwa wana bahati mbaya kuwa na rais ambaye hapendi kukoselewa, hapendi kuambiwa ukweli, hivyo wanahitaji kuona namna ya kutoka wanakoelekea.

Baada ya maelezo hayo, washtakiwa hao walikana kutenda kosa hilo na Wakili Pande aliiomba mahakama hiyo isiwape dhamana kwa usalama wao kwani kosa walilofanya linahatarisha maisha yao.

“Mheshimiwa hakimu, licha ya kwamba hili ni kosa linalodhaminika na kwamba washtakiwa wana haki ya kupata dhamana, lakini si katika mazingira yote.

“Kwa mazingira ya mashtaka yaliyopo mbele yako, upande wa Jamhuri unaomba washtakiwa wasipewe dhamana kutokana na hali ya usalama wao.

“Kosa limejionyesha kwamba ni matumizi ya lugha ya fedheha dhidi ya rais ambaye amechaguliwa na Watanzania wakiwemo wakazi wa Mbeya, sehemu ambayo kosa limetendeka, hivyo wapo ambao hawajapendezwa na kauli hizo, wanaweza kufanya jambo lolote lile kwa washtakiwa.

“Katika kipindi chote ambacho washtakiwa walikuwa mikononi mwa Jeshi la Polisi, yalitokea matukio mengi ambayo yalikuwa yana viashiria vibaya vya kiusalama kwa washtakiwa, hivyo kusababisha jeshi kutumia muda mwingi kulinda usalama wao bila wao kujua.

“Hivyo basi, leo wapo mbele ya mahakama yako na awali wasingeweza kupelekwa mahabusu kwa mujibu wa sheria za Jeshi la Polisi, lakini kwa mujibu wa sheria za mahakama kifungu cha sheria namba 148 kifungu kidogo (5) d cha sheria ya mwenendo wa jinai, kimeeleza kwamba mahakama inaweza kumuweka mshtakiwa mahabusu kwa usalama wake,” alidai Wakili Pande.

Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na Wakili Yongo na kudai mahakamani hapo kuwa usalama wa watuhumiwa hao haupo shakani na kwamba wao ni viongozi, hawawezi kuruka dhamana na kosa waliloshtakiwa nalo linadhaminika.

“Tunapingana na pingamizi hili kwani haki ya dhamana kwa mshtakiwa ipo kikatiba na kwamba kosa waliloshtakiwa wateja wangu linadhaminika na kwamba wakili wa serikali hajawasilisha mahakamani hapo vielelezo vinavyoonyesha wateja wake kwamba hawapo salama,” alidai Wakili Yongo.

Baada ya kusikiliza hoja za kila upande, Hakimu Mteite aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 19, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi.

 

POLISI NA MWANDISHI

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, askari kanzu sita wa Jeshi la Polisi, walivamia katika kituo cha kutoa huduma za intaneti jijini hapa na kuhoji pamoja na kutaka kukagua kazi iliyokuwa ikiandikwa na mwandishi wetu.

Tukio hilo lilitokea jana saa nane mchana wakati mwandishi huyo akiwa na wanahabari wenzake, ghafla alijikuta amezungukwa na askari hao wakitaka kusoma kazi aliyokuwa akiandika.

Wakati mwandishi akiendelea na utekelezaji wa majukumu yake, ghafla lilitokea kundi la askari hao wakiwa wamevalia nguo za kiraia na kumtaka kutoendelea na shughuli aliyokuwa anaifanya hadi kwanza waione.

“Tunakutaka utulie hivyo hivyo, usifanye kitu chochote hadi pale tutakapokueleza nini cha kufanya,” alisikika mmoja wa askari hao.

Baada ya kutolewa kwa agizo hilo, mwandishi alimtaka askari huyo kuonyesha kitambulisho chake na kuhoji tangu lini polisi wamegeuka kuwa wahariri wa kazi za waandishi wa habari.

Hata hivyo, mtu huyo anayedhaniwa kuwa ni ofisa wa polisi ambaye alikuwa na wenzake wengine, alimtaka mwandishi kutambua kwamba wao wapo kazini na pia wanahitaji kukagua na kitabu alichokuwa akichukua kumbukumbu za matukio.

Mwandishi aliwapa note book yake askari kanzu hao, huku wakimtaka kutopiga kelele wakati wote wakiendelea na kazi yao.

Baada ya muda, kiongozi huyo alitoka nje akiwa ameambatana na ofisa mwengine wa kike na baada ya muda walirejea ndani ya kituo hicho kinachomiliwa na Kampuni ya Simu ya TCCL na kumtaka mwandishi huyo aendelee na majukumu yake.

“Tulipata taarifa kwamba wewe unahusika na usambazaji wa vipeperushi, hivyo tulifika ili tujiridhishe na kubaini kwamba taarifa tulizozipata hazina ukweli, pia tumebaini kwamba wewe ni mwandishi wa habari, hivyo endelea na majukumu yako,” alisema kiongozi huyo wa askari hao polisi.

Kwa muda sasa kumekuwa na manyanyaso kwa waandishi wa habari, ikiwamo kupata vipigo na hata wengine kupotea katika mazingira ya kutatanisha, likiwamo tukio la mwandishi wa Azory Gwanda ambaye sasa ni zaidi ya siku 50 haijulikani alipo.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles