Na BENJAMIN MASESE
MBUNGE wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema), ametoboa siri ya kilimo cha bangi wilayani humo hususan eneo la Nkongore Kata ya Kitare.
Amesema zao hilo lilikuwa likilimwa na raia kutoka Kenya ambao walikuwa wakikodi ardhi Tanzania.
Pia aliitaka Serikali kufanya utafiti kuhusiana bangi na tumbaku iwapo kuna athari kubwa na kupendekeza kuangalia uwezekano wa kulifanya zao hilo kuwa la biashara.
Alisema baada ya jeshi la polisi kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Glorius Luoga, kuteketeza zao hilo. alikwenda kutembelea wakazi hao.
Matiko alisema kwa mujibu wa maelezo ya wakazi wa eneo hilo la Nkongore, raia kutoka Kenya ndiyo walikuwa wakikodi ardhi hiyo kwa ajili ya kilimo cha bangi kwa vile zao hilo lina soko kubwa Kenya na mataifa mengine jirani.
“Raia wa Kenya wanakuja Tarime kwa sababu ya ardhi ipo na ina rutuba nzuri lakini jambo ambalo nimekuwa nikilipigia kelele hata bungeni ni kwamba hilo zao linapaswa kuruhusiwa kulimwa kwa sababu lina soko kubwa nje ya nchi.
“Nilisema katika Bunge la 10 nikaiomba Serikali ifanye utafiti au ilete ushahidi kati ya bangi na tumbaku kipi kina madhara makubwa.
“Leo ukiitaka Serikali ilete mtu mmoja tu ambaye alitumia bangi na kuwa teja hawezi kupatikana, naishauri Serikali iruhusu bangi ilimwe kwa lengo la kuuzwa nje ya nchi,”alisema.
Matiko alisema ikiwa zao hilo litaruhusiwa na kuweka mipango namna ya ulimaji na usafirishaji litaweza kuliingizia kipato taifa kuliko baadhi ya mazao yanayopewa kipaumbele.
Alisema siyo kwamba anapingana na Serikali juu ya mapambano ya dawa za kulevya nchini, bali anataka uwepo mpango madhubuti wa kuangalia zao la bangi ambalo madhara yake ni kidogo kuliko ilivyo kwa tumbaku.
Alisema Tarime haina vyanzo vingi vya mapato na ndiyo maana kuna baadhi ya maeneo maendeleo yamekwema.
Mbunge huyo aliiomba Serikali kufungua mnada wa ng’ombe wa Magena mpakani na Kenya.
Alisema mnada huo ulifungwa kisiasa kutokana na kile kilichodai unatumika kurahisisha vitendo vya wizi wa ng’ombe kutoka Tanzania kwenda Kenya.
Hata hivyo, alisema baada ya kupiga kelele hivi karibuni bungeni, viongozi wa Serikali walifika eneo hilo mwishoni mwa mwaka jana na kuahidi kuufungua.
Alisema soko la kimataifa la Lemagwe lilipo wilayani humo nalo limeshindwa kufanya kazi na kusababisha ajira kupotea huku miundombinu yake ikianza kuharibika.