MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora, Munde Tambwe (CCM), amerusha vijembe kwa vyama vya upinzani, akisema viongozi wake wamegeuza vyama hivyo kuwa saccos.
Tambwe alitoa kauli hiyo juzi mjini hapa, wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ilisusiwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Naipongeza Serikali ya CCM kwa kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji… hao wanaotaka kuitoa madarakani watakesha sana.
“Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vyama vya siasa vimekuwa saccos, vinahitaji kutumbuliwa kwa sababu pamoja na kwamba vinapokea ruzuku, havijawahi kutoa hata dawati,” alisema huku akishangiliwa na wabunge wa CCM.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema), aliomba kutoa taarifa akimwambia Tambwe Serikali ndiyo inayotoa fedha na si CCM, na kwamba chama hicho kinaongoza kwa ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma na hati chafu.
Kutokana na hilo, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) naye aliomba kutoa taarifa akisema: “Hatuelewi huyu Matiko anachangia au anafanyaje kwa sababu wamesusia sasa anaongea nini hapa.”
Lakini Tambwe alisema hawezi kupokea taarifa hiyo ya Matiko kwa sababu haina msingi wowote.
“Wameweka nini kwenye ruzuku hata hawajawahi kujenga choo. Wamegeuza vyama NGO’s zao na familia, lazima itungwe sheria ili vitumbuliwe tu,” alisema Tambwe huku Mbunge wa Kilombero, Peter Lijuakali (Chadema) akipaza sauti kwamba kama ni uwaziri hapati.
Awali wakati akichangia hotuba hiyo, Tambwe alisema tatizo la ajira kwa Mkoa wa Tabora ni kubwa pamoja na kwamba wanalima tumbaku na kuchangia pato la Taifa, lakini watu wake hawana faida na kilimo hicho.
Naye Asha Abdalah Juma (Viti Maalumu), alivishambulia vyama vya upinzani kwa kususia bajeti hiyo ya Waziri Mkuu, akisema wanachokifanya ni kutaka kuikwamisha.