25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE ALIYEMWAPISHA RAILA AKAMATWA

NAIROBI, KENYA


MBUNGE wa Ruaraka, Tom J Kajwang’, ambaye aliongoza shughuli ya kumwapisha kiongozi wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, katika viwanja vya Uhuru Park jijini hapa juzi, amekamatwa na polisi jana.

Kajwang’ alikamatwa jana alasiri na askari kanzu nje ya Mahakama ya Sheria Milimani jijini Nairobi, ambako alikuwa ametoka kusimama mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, George Odunga kwa uamuzi wa kesi, ambayo alikuwa akiwakilisha wabunge wanaopinga kupunguzwa kwa mishahara na posho zao.

Awali kabla ya tukio hilo, Kajwang’ ambaye pamoja na mwanasheria mwingine Miguna Miguna, walikuwa katikati ya tukio la kumwapisha Raila kuwa ‘rais wa watu’, alisema kwamba haogopi lolote kumtokea na kwa uzoefu wake wa miaka 28 kama wakili wa mahakama kuu, amejifunza mengi.

Wakati wa hafla hiyo, Kajwang’ aliyewasili Uhuru Park mapema, alivalia joho la uwakili na wigi kichwani na kukaribishwa na kelele za shangwe na wafuasi wa NASA.

Haijafahamika mara moja sababu ya kukamatwa kwa mbunge huyo na iwapo zinahusu tukio la kuapishwa kwa Raila, ambalo Serikali ilishaonya kuwa ni uhaini na adhabu yake ni kifo.

Tayari Jeshi la Polisi juzi lilitangaza kuanza kukamata wafuasi wa vuguvugu la upinzani la NASA (NRM) ikiliita la kigaidi sambamba na makundi kama al-Shabaab.

Katika hatua nyingine, kinara mwenza wa NASA, Kalonzo Musyoka, amedai kutoonekana kwake katika viwanja vya Uhuru Park wakati wa kuapishwa kwa Raila, kulitokana na kunyang’anywa walinzi wake.

Kalonzo ambaye pia alikuwa aapishwe, alidai kuwa vinara wengine wa NASA, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula pia walizuiwa na polisi kuhudhuria tukio hilo.

Hata hivyo, maelezo yake yaliyorekodiwa na kusambazwa katika mtandao wa WhatsApp usiku wa kuamkia jana, yanaweza kuleta mkanganyiko zaidi.

Katika maelezo hayo ya sauti yanayosikika kwa Kiswahili, Musyoka anasema: “Wakati tulipokutana usiku uliopita (Jumatatu), Mheshimiwa Raila aliona vyema kutoutumikia usiku nyumbani kwake. Mimi niliamua kubaki nyumbani na huo ni mpango tuliofikia.”

Aliongeza askari polisi waliohusisha walinzi wake katika nyumba zake za Karen na Tseikuru na yule anayeambatana naye, waliondolewa asubuhi na waliambiwa watafukuzwa kazi iwapo watamsindikiza kuelekea Uhuru Park.

“Niliachwa peke yangu. Nilikaa nyumbani hadi saa tano asubuhi na huo ni wakati waandishi walikuja nyumbani kwangu. Niliondoka. Tulizungumza kwa njia ya simu na Mheshimiwa Raila, Wetang’ula na Mudavadi kupanga safari yetu kwenda Uhuru Park. Hatukuweza kufika. Tulijikuta mimi, Wetang’ula na Mudavadi katika mkwamo, kwa sababu hatukuwa na walinzi kuweza kutoka chumbani. Hicho ndicho kilichotokea,” alidai.

Hata hivyo, haikuweza kujulikana wapi watatu hao walijichimbia wakati Raila akiapishwa Uhuru Park, huku wabunge wa chama anachokiongoza, Wiper pia wakiwa wameingia mitini.

Kalonzo alidai kuwa alidhamiria kuapishwa kama ilivyopangwa.

“Kwa sasa nawataka wale wanaosambaza taarifa katika mitandao kutoleta mvurugano ndani ya Nasa. Sisi vinara wanne bado tu imara na wamoja,” alisema.

Awali baada ya hafla ya kuapishwa, vinara hao watatu walisema kwamba hawakuweza kuungana na Odinga kama ilivyopangwa kutokana na hali zilizo nje ya uwezo wao na kwamba wako pamoja na watakutana ndani ya siku mbili kujadili changamoto zinazoikumba nchi.

Hilo limekuja huku nyumba ya Kalonzo ya Karen ikiwa imejaa maofisa wa polisi wanaochunguza tukio la bomu na risasi zinazodaiwa kurushwa katika makazi hayo usiku wa kuamkia jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles