RAMADHAN HASSAN,
MBUNGE wa Viti Maalumu, Salma Mwasa (CUF), amehoji ni lini Serikali itatekeleza miradi ya maji Dar es Salaam.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Mwasa alidai miradi mingi ya maji Dar es Salaam imekuwa haitekelezwi, je ni lini Serikali itaanza kuitekeleza.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM), alihoji ni lini Serikali itahakikisha kuwa wananchi wa Nyamagana wanapata maji ya uhakika hasa ikizingatiwa wamezungukwa na Ziwa Victoria.
‘’Jimbo la Nyamagana lina ukubwa wa kilomita za miraba 256, kati ya hizo kilomita za mraba 71.56 ni eneo la maji ya Ziwa Victoria.
“Lakini bado wananchi wake hawapati maji ya uhakika ya bomba, sasa ni lini Serikali itahakikisha wananchi hao wanapata maji?” alihoji Mabula,
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isaack Kamwelwe alisema Serikali imekwisha kukamilisha miradi ya maji katika Mto Ruvu chini na juu.
Alisema kufanya hivyo huduma ya maji itakuwa ya uhakika Dar es Salaam.
Kamwelwe alisema huduma ya maji katika Wilaya ya Nyamagana Mwanza inatolewa kwa asilimia 90 ya wakazi wote na wilaya hiyo.
‘’Hata hivyo baadhi ya wakazi ambao wanaishi katika sehemu za mwinuko na wanaoishi pembezoni mwa Jiji wanakosa ya maji,’’ alisema.
Alisema kwa kutambua hilo imepata mkopo wa masharti nafuu kutoka European Investment Bank (EIB) Euro milioni 54 (Sh bilioni 110).