Â
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali, amehoji bungeni uhalali wa raia kutoka nchini Msumbiji na Tanzania ambao wamekuwa kushiriki katika uchaguzi katika nchi zote mbili.
“Kumekuwa na raia wengi kutoka Msumbiji katika Jimbo la Mchinga hasa vijiji vya Kilangala B, Butamba na Mvuleni Kilombwani, wamekuwa wakishiriki uchaguzi katika nchi zote mbili, je, raia hao ni Watanzania au wa Msumbiji, na je, Serikali imepitisha utaratibu wa raia pacha na kuwapa watu maalumu,” amehoji Bobali.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde, amesema sheria hazijaruhusu uraia wa nchi pacha wala hakuna watu maalumu waliopewa uraia wa aina hiyo.
“Ibara ya 5 (2) (a) ya katiba hairuhusu mtu mwenye uraia wa nchi nyingine kushiriki shughuli za uchaguzi ikiwamo kupiga kura, hata hivyo, ili mtu aweze kupiga kura lazima awe ameandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura lililoanzishwa chini ya Ibara ya 5 (3) (a) ya Katiba,” amesema Mavunde.