25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge ageuka mbogo kwa wanaomhujumu Rais

Na Gustafu Haule, Pwani

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini mkoani Pwani, Michael Mwakamo (CCM) amewaijia juu baadhi ya watendaji na wataalamu wa Halmashauri hiyo wanaofanya makusudi ya kuhujumu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano chini ya  Rais Dk. John Magufuli.

Mwakamo amesema kwa sasa mtendaji atakayebainika kufanya hivyo atakula nae sahani moja kwa kuwa hatoweza kumvumilia mtendaji wa aina hiyo.

Mwakamo aliyasema hayo juzi Mlandizi mkoani Kibaha wakati akizungumza na watendaji hao mara baada ya kumalizika kwa zoezi  la kuapishwa kwa madiwani wa Halmashauri hiyo.

Mwakamo amesema Rais Magufuli anaendesha nchi akiwa na dhamira ya dhati ya kutaka kuifikisha nchi katika hatua nzuri ya kimaendeleo lakini wapo watu wachache ambao wanakwamisha malengo hayo.

Amesema miongoni mwa watu hao ni baadhi ya watendaji na wataalamu waliopo katika Halmashauri hiyo ambao wamekuwa wakishindwa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo jambo ambalo linakatisha tamaa.

Amesema Jimbo la Kibaha vijijini limepata madiwani makini na hata yeye mwenyewe hawezi kukubali kuona miradi hiyo inakwama na kwamba watashirikiana na madiwani kuhakikisha Kibaha vijijini inabadilika.

“Mimi pamoja na madiwani wangu tupo pamoja na tumejipanga kuhakikisha hakuna mradi utakaokwamishwa  kizembe na kama tutabaini kuna mtendaji au mtaalamu wa namna hiyo basi tutakula nae sahani moja,”amesema Mwakamo.

Aidha amesema kuwa haiwezekani Rais Magufuli afanye mambo makubwa ya kitaifa halafu akae na kuwaza kusimamia miradi ya Jimbo la Kibaha Vijijini wakati mbunge yupo, madiwani wapo na watendaji wapo.

Amesema kazi alizofanya rais kwa sasa anapaswa kutulia na badala yake watendaji na wataalamu wawe mstari wa mbele kumsaidia kuliko kumpa majukumu ambayo yapo ndani ya uwezo wa viongozi wa ngazi za chini.

“Rais Magufuli anaendesha nchi hii kwa dhamira ya dhati na anataka kuifikisha nchi mbele zaidi kwahiyo tusimpe wakati mgumu wa kuja kufanya mambo ya Jimbo letu wakati kuna madiwani ,mbunge na watendaji ,”amesema Mwakamo.

Mwakamo amesema kuanzia sasa wakibaini mtendaji au mtaalamu anakwamisha miradi ya maendeleo kamwe hatovumilika na kwamba lazima watahakikisha anaondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo.

Aidha, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha Vijijini,  Butamo Ndalahwa kuanza maramoja kuitangaza miradi inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ili wananchi wapate kuelewa namna ambavyo serikali yao inavyofanyakazi.

“Mimi nashangaa kuona katika Halmashauri nyingi nchini zikitangaza miradi inayotekelezwa kupitia Rais Magufuli lakini kwa Halmashauri hii sijaona mkifanya hilo au Kibaha Vijijini hakuna miradi? nawaambia kama nyinyi mnashindwa mimi nitafanya hilo,” amesema Mwakamo.

Nae diwani wa viti maalum (CCM), Josephine Gunda amesema umefika wakati lazima watendaji watambue wajibu wao na kwamba wao wamewekwa ili waweze kumsaidia rais kuwaletea wananchi maendeleo.

Upande wake Ndalahwa amesema kuwa kupitia kikao hicho amepokea maelekezo yote na atakwenda kuyafanyia kazi na kikao kijacho atapeleka taarifa zote za utekelezaji wa maagizo hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles