Na MAREGESI PAUL-DODOMA
MBUNGE wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba (CCM), amelieleza Bunge jinsi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alivyodanganywa baada ya kutembelea Manispaa ya Morogoro hivi karibuni.
Mgumba alitoboa siri hiyo bungeni jana alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2018/19 iliyowasilishwa na Lukuvi juzi.
“Leo nataka nikwambie kitu walichokufanyia siku ulipokuja kufanya ziara Morogoro Manispaa. Kuna watu walikuwa wamejiandaa kuja kukueleza migogoro ya ardhi, lakini hukuonana nao kwa sababu waliwekwa kwenye chumba kingine na wewe ukapelekwa chumba walimokuwa watumishi wa manispaa ambao ndio ulizungumza nao.
“Kwahiyo nakuomba uje tena Morogoro uonane na wananchi wenye migogoro na miongoni mwao ni mimi, mjomba wangu na wananchi wengine wengi,” alisema Mgumba.
Pamoja na hayo, Mgumba alisema katika Manispaa ya Morogoro, baadhi ya watumishi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wana kawaida ya kuchoma mafaili ya wamiliki wa ardhi na kuandaa mapya kwa manufaa yao.
Wakati huo huo, Mgumba alilalamikia uwepo wa migogoro ya ardhi, huku akitaka gharama za kupima ardhi zipunguzwe ili wananchi wengi waweze kupimiwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Anne Kilango (CCM), alilalamikia mashamba ya mkonge yaliyoko katika kata za Makanya na Ndungu wilayani Same, kwa kile alichosema hayana faida kwa vijana na wananchi wa wilaya hiyo.
Aliitaka Serikali iangalie jinsi ya kuwafanya wananchi wa Same waweze kupata ardhi kuendesha maisha yao.
“Kwanza kabisa nampongeza Waziri Lukuvi kwa jinsi alivyofanikiwa kutatua migogoro ya ardhi nchini.
“Pamoja na hayo, naiomba Serikali ifanye kila inaloweza kuwafanya wananchi wa Same wanufaike na ardhi, kwa sababu sehemu kubwa ya ardhi yao ni milima na nyingine ni mashamba ya mkonge ambayo hayawasaidii kitu,” alisema Kilango.
Kwa upande wake, Waziri Lukuvi alipokuwa akihitimisha mjadala huo, alisema mtumishi yeyote wa wizara yake atakayefanya kazi kinyume cha sheria, hatahamishwa na badala yake atachukuliwa hatua akiwa kituoni kwake.
“Kuna migogoro mingine ya ardhi tunaisababisha sisi viongozi, lakini nawaambia kwamba kitendawili cha mtumishi kufanya kazi kwa mazoea kimeshateguliwa na Serikali ya awamu ya tano.
“Yeyote atakayevunja sheria, hatahamishwa bali atachukuliwa hatua akiwa hapo hapo kituoni kwake.
“Kuhusu migogoro ya ardhi ambacho ndicho kilio cha waheshimiwa wabunge, nawahakikishia tutaendelea kuitatua na maeneo yenye watumishi wachache, tutawapeleka wengine ili kazi za upimaji wa ardhi zifanyike kwa haraka, kwa sababu tutawapa mafunzo ya namna ya kutumia vifaa vipya vya upimaji wa ardhi.
“Kuhusu changa la macho nililopigwa kule Morogoro, naahidi nitakuja tena, lakini kabla ya kuja, nitaonana na mheshimiwa Mgumba,” alisema Waziri Lukuvi.