26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

MASHINE ZA EFD’S ZALETA HITILAFU, MBUNGE AHOJI

Na MAREGESI PAUL-DODOMA


MASHINE za kielektroniki za kukusanya mapato (EFDs), hazifanyi kazi nchi nzima.

Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM).

Akijibu mwongozo huo, Dk. Kijaji, alisema Serikali inatambua uwepo wa tatizo hilo na kwamba imeshachukua hatua kwa kupeleka wataalamu wa habari na mawasiliano (ICT) katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutatua tatizo hilo.

“Ni kweli mheshimiwa mwenyekiti tatizo hilo lipo na lilianza Mei 11, mwaka huu na bado tunaendelea kulishughulikia.

“Lakini, baada ya kuwapo kwa tatizo hilo, tulilishughulikia na kulimaliza na mambo yakawa sawa kwa wiki moja, lakini baadaye lilijirudia.

“Kwa sasa wataalamu wetu wa e-government na ICT wanaendelea kulishughulikia na tunatarajia kulitatua mapema. Wataalamu wote wa ICT wako pale Mamlaka ya Mapato na tunaamini tatizo hilo litatatuliwa ndani ya muda mfupi kwa sababu tunajua kutokuwapo kwa mfumo huo Serikali inapoteza mapato,” alisema Dk. Kijaji.

Awali, Ndassa alisimama na kuomba mwongozo akitumia kanuni ya 68 (7), akieleza jinsi alivyopata taarifa za kutofanya kazi kwa mashine hizo na kusema tatizo hilo linaweza kuwa ni hujuma dhidi ya Serikali.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, huko mitaani na maeneo mbalimbali nchini, ni wiki ya tatu sasa ukinunua bidhaa kama mafuta hupewi risiti kwa sababu mashine zote za EFDs hazifanyi kazi.

“Hata leo asubuhi nimepigiwa simu kutoka Mwanza, wananieleza juu ya tatizo hilo na naamini Serikali sasa inapoteza mapato.

“Kwahiyo, Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua Serikali inasemaje juu ya jambo hilo, kwa sababu linaweza kuwa ni hujuma dhidi ya Serikali ili ipoteze mapato na kulifanya liwe janga la taifa,” alisema Ndassa.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, aliitaka Serikali iwe makini na utatuzi wa jambo hilo kwa sababu linapoteza mapato mengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles