NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kwamba mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe anayekabiliwa na kesi ya uchochezi na wenzake nane, yu mahututi na amesafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya moyo na presha.
Taarifa hizo ziliwasilishwa leo mahakamani hapo na wakili, Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Wakili Kibatala alidai kwamba alimuhoji mdhamini wa Mbowe, Grayson Celestine na akamueleza kuwa Mbowe amesafirishwa nchini Afrika Kusini akiwa mahututi na alimueleza nyaraka za usafiri na matibabu zitawasilishwa kwa barua mahakamani.
Kwa upande wa wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliiomba Mahakama kutoa amri ya kumkamata mara moja Mbowe, ili ajieleze kwanini dhamana aliyopewa na mahakama isifutwe kwa kushindwa kuiheshimu.
Hakimu Mashauri alimuuliza mdhamini kuwa ana nini cha kuithibitishia mahakama kuwa Mbowe amesafiri nje ya nchi kwa matibabu na kumuhoji kama ana nyaraka yoyote.
Mdhamini huyo alidai kuwa mshtakiwa akirejea atawasilisha nyaraka za safari na matibabu kwa mahakama na upande wa mashtaka, alidai anafanya mawasiliano ili aweze kutumia kwa Fax.
Nchimbi alidai Jamhuri wanaona ni muendelezo wa dharau ya mshtakiwa namba moja Mbowe kwa mahakama na kwa kuwa alikwisha pewa onyo mara mbili.
“Upande wa mashtaka tunapenda kusema kwamba mshtakiwa huyu kutofika kwake mahakamani, ameamua kwa utashi wake kukiuka amri ya mahakama,” alidai Nchimbi.
Nchimbi aliiomba Mahakama kutoa amri ya kutaka mshtakiwa aletwe mahakamani mara moja ili ajieleze kwanini dhamana yake isifutwe kwa kushindwa kuheshimu dhamana yake aliyopewa.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mashauri alisemaa kutokuwepo kwa mshtakiwa wa kwanza mahakamani anakubaliana na upande wa mashtaka kwamba mshtakiwa huyo aje mahakamani kueleza kwa nini dhamana yake isifutwe.
Hata hivyo Hakimu Mashauri alisema iwapo mshtakiwa hatopeleka vielelezo atatoa amri ya kukamatwa ili ajieleze kwanini asifutiwe dhamana kwa kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa na mahakama.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ambao wanatetewa na wakili, Peter Kibatala ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na mbunge wa kibamba, John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, mbunge wa Kawe Halima Mdee, mbunge wa bunda, Esther Bulaya, mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji. Huku Peter Msigwa akitetewa na wakili Jamuhuri Johnson.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, likiwemo la kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari mosi na 16, mwaka huu jijini Dar es Salaam.