30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mbowe awasilisha hoja tatu kwa JPM

Andrew Msechu – Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema chama chake kimemwandikia rasmi barua maalumu Rais Dk. John Magufuli, kikitoa mapendekazo muhimu ya kiushauri, kuhusu mambo ya msingi ya kufanya ili kuleta utangamano wa kitaifa.

Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Mbowe alisema barua hiyo maalumu ilipelekwa na kupokewa Ofisi ya Rais Dodoma Januari 29, mwaka huu ikiwa inalenga ushauri na mapendekezo matatu muhimu ya kushughulikiwa.

“Barua hiyo inatoa mapendekezo ya umuhimu wa marekebisho muhimu ya Katiba ili kuruhusu Uchaguzi Mkuu wa 2020 kuwa huru na wa haki, hasa kulingana na kauli ya hivi karibuni ya Rais akiwa na mabalozi, alipoahidi kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na wa haki.

“Kauli hiyo ilipokelewa kama ukiri wa yeye kutambua umuhimu wa uchaguzi huru na wa haki. Kuna hatari kubwa ya kutengwa na jumuiya ya kimataifa iwapo ahadi za namna hii zisipotekelezwa, kwa hiyo ni vyema Rais akichukua hatua kuhakikisha anatimiza maneno ya kinywa chake,” alisema Mbowe.

Alisema barua hiyo imeeleza kuwa Chadema kama chama kikuu cha upinzani kinaamini kuna kila sababu sasa kuanza kuchukua hatua za makusudi na shirikishi kukabiliana na changamoto zilizopo na kwamba Rais ana mamlaka yote ya kuanzisha mchakato wa kurudisha utengemano wa nchi.

Mbowe alisema katika barua hiyo, Chadema imepeleka mapendekezo ya awali yaliyojikita katika kuanza kulikwamua taifa katika sintofahamu inayolinyemelea ambayo yamejikita kwenye maeneo makuu matatu.

Alieleza kuwa maeneo hayo ni marekebisho madogo ya Katiba na sheria mbalimbali za uchaguzi ili kuwezesha upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi, kufutwa na kurudiwa kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 2019 na Kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi. Kama ujuavyo, mwaka wa uchaguzi huhitaji busara, uelewa na uvumilivu ili kuivusha nchi salama. Kwa hali ilivyo sasa, kuna kila aina ya kiashiria cha uwepo wa machafuko ya kisiasa kabla, wakati na baada ya uchaguzi, kama hatutazika ‘viburi’ vyetu vya kiitikadi na badala yake kusimama pamoja kama taifa kuruhusu haki na demokrasia ya kweli kutamalaki,” alisema Mbowe.

Alisema katika barua hiyo, wameeleza kuwa wana uhakika kuwa kwa sasa taifa linahitaji maridhiano ya kitaifa na viongozi wana wajibu huo mbele ya wananchi na hata mbele ya Mungu, na Rais akiwa kama kiongozi mkuu wa nchi, ana turufu na wajibu wa kipekee kuwezesha matamanio hayo ya haki kupatikana.

Mbowe alisema kuwa pamoja na barua hiyo, ameambatanisha maelezo ya kina ya vifungu mbalimbali vya Katiba na sheria ambavyo wanashauri kurekebishwa.

“Nina hakika wadau wengine katika taifa letu nao watakuwa na mawazo ya kuchangia katika kuutafuta mustakabali mwema,” alisema Mbowe akinukuu sehemu ya barua hiyo.

Alisema wameeleza kuhusu maeneo yanayohitaji kufanyiwa marekebisho kuhusu sifa na masharti ya kugombea, na mchakato wa kuweka na kuamua mapingamizi dhidi ya uteuzi wa wagombea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles