25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MBOWE ATOKA NA MSIMAMO MKALI SEGEREA

Na KULWA MZEE -DAR ES SALAAM


MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake sita wametimiza masharti ya dhamana na kuachiwa na mahakama lakini wametoka gerezani na msimamo mkali.

Viongozi hao walidhaminiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, baada ya kukaa gerezani Segerea kwa siku saba.

Mbowe baada ya kutoka nje ya mahakama alisema siku za nyuma kulikuwa na ukandamizaji wa haki, lakini sasa umetimia kwamba  ataulotea ufafanuzi wakati mwingine.

Mbowe na wenzake watano, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Machi 25, mwaka huu na kusomewa mashtaka nane lakini jana mashtaka hayo yalibadilishwa na kusomewa upya mashtaka tisa baada ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee  kuunganishwa kwenye kesi hiyo.

Jana hali ya ulinzi iliimarishwa ndani na nje ya mahakama huku wafuasi wa Chadema wakizuiliwa kuingia katika viwanja vya mahakama na wale waliofanikiwa kuingia, baadhi walizuiwa kuingia katika ukumbi wa mahakama.

Wana Chadema hao walikwaruzana na polisi hadi Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye alikuwa  mahakamani alitoka nje ya kwenda kuwasihi wawe watulivu.

Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa,  Frederick Sumaye na Wakili Mabere Marando, walifika mahakamani hapo mapema kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.

 

Wasomewa mashtaka upya:

Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai anaiomba mahakama kuwasomea upya washtakiwa mashtaka yanayowakabili ambapo alimuongeza Mdee katika orodha ya washtakiwa.

 

Nchimbi aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Mbowe,  Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vicent Mashinji, Salum Mwalimu, Peter Msigwa, John Mnyika, Ester Matiko na Mdee.

Washtakiwa wote wanadaiwa  kufanya mkusanyiko au maandamano yasiyo halali, kuendelea na mkusanyiko usio halali wenye vurugu baada ya kutolewa tamko la wao kutawanyika.

Mbowe peke yake alisomewa mashtaka ya kuhamasisha chuki miongoni mwa wanajamii isivyo halali, uchochezi na kusababisha chuki miongoni mwa wanajamii, uchochezi wa uasi, ushawishi utendekaji wa kosa huku Msigwa akisomewa shtaka la kushawishi raia kutenda kosa.

Nchimbi alidai washtakiwa wote mnamo Februari 16, mwaka huu, wakiwa katika barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa wamekusanyika kutekeleza lengo la pamoja kinyume cha sheria, waliendelea na mkusanyiko katika namna iliyowafanya watu waliokuwa kwenye eneo hilo waogope watakwenda kwenye uvunjifu wa amani.

Alidai washtakiwa wote, katika tarehe hiyo, wakiwa kwenye barabara hiyo kwa pamoja katika ujumla wao wakiwa wamekusanyika wao sita na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani, wakiwa katika maandamano au mkusanyiko wenye vurugu na kutozingatia amri ya kusitisha maandamano iliyotolewa na askari, waligoma kutawanyika na kuendelea na mkusanyiko huo wa vurugu uliosababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeraha kwa askari wawili kutokana na mkusanyiko wa vurumai walizozisababisha.

Mbowe, anadaiwa siku hiyo katika viwanja vya Buibui, vilivyoko wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, akiwa anahutubia wakazi wa jimbo la uchaguzi la Kinondoni alitoa matamshi ambayo kwa hali ya kawaida yanaleta hisia za chuki miongoni mwa wanajamii na wakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anadaiwa kusema ‘ninapozungumza hapa kiongozi wetu wa Kata ya Kinondoni Hananasif yupo mochwari… amekamatwa na makada wa CCM kwa msaada wa vyombo vya ulinzi na usalama… Wamemnyonga, wamemwua halafu sisi tunaona ni jambo la kawaida… Tunacheka na polisi na CCM.

Katika mashtaka ya uchochezi wa uasi, Mbowe anadaiwa siku hiyo kwenye viwanja hivyo alitoa maneno kwa nia ya kupandikiza chuki na dharau kwa upande wa wakazi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania dhidi ya mamlaka halali ya serikali iliyoko madarakani.

Anadaiwa kusema ‘Tumejipa kibali cha kutangulia mbele ya haki… Haiwezekani wanaume wazima na akili zetu,wake zetu na watoto wetu tukafanywa ndondocha…hii ni nchi ya ajabu mimi leo nipo hapa kuliandaa Taifa.. Kule Afrika Kusini juzi, jana aliyekuwa Rais Jacob Zuma amelazimishwa kujiuzulu, Mugabe (Robert) kang’olewa…. Magufuli ni mwepesi kama karatasi.

Mbowe pia anadaiwa siku hiyo kwenye viwanja hivyo akiwa amejumuika na wengine ambao hawapo mahakamani aliwashawishi wakazi wa Kinondoni kutenda kosa la kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali.

Msigwa yeye anadaiwa siku hiyo kwenye viwanja hivyo aliwashawishi wakazi wa Kinondoni kutenda kosa la kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.

Mdee anashtakiwa kwa uchochezi wa chuki akidaiwa kusema’ Sihitaji kusimulia madhila yanayomkuta kila mmoja, naombeni kesho tukamchinje Magufuli kama mbwai na iwe mbwai’.

Washtakiwa wote walikana mashtaka na upande wa utetezi ukiongozwa na Peter Kibatala, uliomba mshtakiwa Mdee apewe dhamana kwa masharti kama ambayo walipewa kina Mbowe na wengine.

Hoja hiyo ilipingwa na Wakili Nchimbi ambaye alidai wanapinga dhamana ya Mdee na kwamba kila mtuhumiwa atabeba mzigo wake mwenyewe.

Akitoa sababu za kupinga dhamana, Wakili wa Serikali Dk. Zainabu Mango alidai Mdee alipewa dhamana ya polisi na alitakiwa kuripoti mara moja kwa wiki lakini aliruka dhamana hiyo.

Alidai Mdee hakufika polisi Machi 15, 22 na 29, mwaka huu alipotakiwa kuripoti, hivyo wanapata hofu endapo atapewa dhamana mahakamani hataweza kutimiza wajibu wake wa kufika mahakamani.

Akijibu, wakili Kibatala alidai hoja za Jamhuri za kufikirika na mahakama haiwezi kuongozwa kumnyima dhamana mshtakiwa kwa hoja kama hizo.

Kibatala alidai mahakama ilitakiwa kupokea taarifa kutoka kwa aliyempa dhamana Polisi na si kwa mawakili wa Serikali kwani wao si wapelelezi wala si wakamataji.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mashauri alisema polisi ni taasisi inayojitegemea hakuna sheria inayoweza kuiruhusu mahakama kumnyima dhamana mshtakiwa kwa sababu aliruka dhamana yao.

“Kutokana na sababu hizo, mahakama inakubali kumpa dhamana mshtakiwa kwa masharti kama ya washtakiwa wengine. unatakiwa kuwa na wadhamini wawili, watakaosaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 20, wawe na barua na vitambulisho na washtakiwa wanatakiwa kuripoti Polisi mara moja kila wiki,”alisema.

 

Kesi kusikilizwa haraka:

Wakili Nchimbi alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, asilimia kubwa ya watuhumiwa ni wabunge, wanawawakilisha wananchi katika majimbo yao.

“Kwa haiba ya watuhumiwa wanapokuwa mahakamani wanaleta umati mkubwa kwa maslahi ya haki na uchumi shauri hili liendeshwe haraka mfululizo, washtakiwa wajitetee , tunaomba kama mahakama itaridhia turuhusiwe kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali kesho,”alidai nchimbi.

Kibatala alijibu hoja hizo akidai kwamba Machi 28 jamhuri walipotaka kuwasilisha nia ya kukata rufaa hawakuona uharaka huo lakini hilo analiacha kwa mahakama.

Alidai katika tarehe hizo, atakuwa na kesi katika mahakama mbalimbali na ataenda Arusha katika Mkutanao wa TLS hivyo aliomba kesi hiyo ipangwe Aprili 16 au 19.

Hakimu Mashauri, alikubaliana na hoja za Kibatala na kuipanga kesi hiyo Aprili 16 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles