24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 11, 2024

Contact us: [email protected]

JPM:TANESCO JIPANGENI KUSHUSHA BEI YA UMEME

ELIZABETH HOMBO Na NORA DAMIAN


RAIS Dk. John Magufuli, ameitaka Wizara ya Nishati kujiandaa kupunguza bei ya umeme kwa wananchi.

Alisema kwa sababu baada ya miradi yote ya umeme nchini kukamilika, Tanzania itakuwa na megawati 5,000 ambazo ni nyingi.

Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana  wakati akizindua kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi II chenye megawati 240 CCPP.

“Hivi sasa tuko pia kwenye utekelezaji wa mradi mkubwa wa umeme wa Stigliers George ambao utakuwa na megawati 2,100.

“Nina imani  wizara mtaendelea na majadiliano na mkandarasi ambao mtakuwa mmemteua kwa sababu nimeambiwa na Waziri wa Fedha (Dk. Philip Mpango) kuwa fedha za mradi huo zipo tayari.

“Miradi yote hii ikikamilika, itafika megawati 5,000, lazima tuwabane wizara waanze kupunguza bei ya umeme.

“Hatuwezi tukawa tunazalisha megawati zote hizo tena kwa malighafi za Watanzania halafu bei ya umeme iwe juu.

“Muanze sasa kupunguza bei ya umeme. Tumechoka kusindikiza, sasa  tunataka na wengine  watusindikize,”alisema Rais Magufuli.

KUGAWA WIZARA

Rais Dk. Magufuli pia alieleza sababu za kuigawa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, akisema lengo ni kuhakikisha kila waziri anawajibika vyake.

Hata hivyo alisema gharama kubwa ya umeme iliyopo  imetokana na baadhi ya mikataba ya nishati hiyo iliyoingiwa kuwa ni mibovu na ya ovyo.

“Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Ofisi ya Takwimu mwaka 2015/16, asilimia 36.6 ya Watanzania ndiyo wameunganishwa na umeme, asilimia 60 bado hawajaunganishwa na wanatumia mkaa, kuni, mafuta ya taa … na hali hii imechangiwa na bei ya umeme kuwa juu.

“Bei ya umeme bado iko juu ikilinganishwa na nchi zilizoendelea, ni ngumu hata kuwa na mashindano katika uwekezaji ndiyo maana nasisitiza umuhimu wa umeme.

“Na ndiyo sababu niliigawa wizara ya madini na nishati ili kila waziri awajibike  vyake, asitafute visingizio,”alisema Rais Magufuli.

Rais   pia aliagiza Wizara ya Nishati na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kuondoa changamoto za kuwaunganishia nishati hiyo wananchi.

Aliwataka wakuu wa taasisi mbalimbali za umma kufanya kazi kwa ushirikiano  kuepuka gharama wanazoisababishia Serikali na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.

Alisema yamekuwapo malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme hivyo hatua za haraka zinahitajika kuchukuliwa.

“Wizara ya Nishati na REA, hakikisheni mnaongeza kasi ya kuunganishiwa umeme, yapo malalamiko madogo madogo ya wafanyakazi kuomba rushwa, yamalizeni hayo  pamoja na kwamba wengi ni waaminifu,”alisema Rais Magufuli.

Kuhusu malalamiko ya taasisi kucheleweshewa baadhi ya huduma, Rais Dk. Magufuli alisema suala hilo linamkera na hataki kulisikia tena.

“Taasisi za Serikali zinatakiwa kufanya kazi kwa karibu hasa tunapotekeleza miradi mikubwa ya taifa  tusicheleweshane.

“Mawaziri, wakurugenzi, wenyeviti wa bodi msiache kuwasiliana ninyi kwa ninyi, kama unaona unakwamishwa na taasisi nyingine mambo kama haya nikisikia huwa yananiudhi…kwa lugha ya mitaani yananiboa kweli kweli. Shirikianeni kwani mnawacheleweshea wananchi maendeleo,” alisema Rais Magufuli.

Alisema  umeme wa uhakika unasaidia kutekeleza Tanzania ya viwanda  kwa sababu kwa sasa mahitaji ya nchi ni megawati karibu 1,40O.

“Hivi sasa uzalishaji umefikia megawati 1,515.3,  bado tunahitaji umeme wa kutosha na tuongeze uzalishaji,”alisema.

Rais Magufuli alisema ifikapo mwaka 2020/21, vijiji 873 ambavyo hazijafikiwa na umeme wa REA, vitakuwa vimefikiwa.

WAZIRI WA NISHATI

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alisema malengo   ni kuzalisha umeme megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

Alisema pia kuna miradi ya kusafirisha umeme kutoka Rufiji – Chalinze – Dodoma   utumike katika ujenzi wa reli ya kisasa.

Alisema miradi mingine ya kusafirisha umeme kutoka Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Malagarasi, utekelezaji wake utaanza rasmi mwaka huu na  utagharimu Dola za Marekani milioni 664.

Alisema ujenzi wa mradi wa kusafirisha umeme umbali wa kilomita 670 tayari umekamilika na unatarajiwa kuzinduliwa mapema mwakani.

Waziri alisema mradi wa kusafirisha umeme kutoka Makambako hadi Songea mkoani Ruvuma, unatarajiwa kukamilika Agosti  mwaka huu na  utapeleka umeme kwenye vijiji 120 katika mikoa husika.

“Mradi mwingine kutoka Singida hadi Namanga umbali wa kilomita 414, mkandarasi amepatikana na tunatarajia utaanza wakati wowote kuanzia sasa,” alisema Dk. Kalemani.

Alisema hadi sasa nguzo 20,000 zimepelekwa  maeneo mbalimbali nchini na   wateja wameongezeka kutoka milioni moja hadi kufikia zaidi ya milioni mbili, ikiwa ni ongezeko la asilimia 30.

MKURUGENZI TANESCO

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, alisema katika mradi wa Kinyerezi II utekelezaji uko mbele kwa wakati uliokusudiwa  kwa sababu  mitambo yote sita ya gesi imeanza kuzalisha umeme na kuingiza kwenye gridi megawati 167.82.

Alisema kazi inayoendelea ni kukamilisha kufunga mitambo inayotumia mvuke yenye uwezo wa kuzalisha megawati 80.4.

“Licha ya  mradi huu kufadhiliwa na Serikali, Tanesco inalazimika kulipa gharama nyingi ambazo tumekuwa tukipata ugumu kuzimudu kwa wakati,” alisema Dk. Mwinuka.

Alifafanua gharama hizo kuwa  ni   za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) Sh bilioni 186, tozo ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ya kupitisha mzigo mzito (Sh bilioni 5.6), gharama ya mchango wa njia ya reli (Sh milioni 186) na gharama za kutoa mizigo bandarini (Sh bilioni 12.23).

“Hali hii imesababisha shirika kushindwa kulipa fedha husika kwa wakati kutokana na mahitaji kuzidi mapato yetu. Baadhi ya mizigo imekuwa ikichelewa kutoka bandarini na hivyo kuongezeka kwa gharama za mradi ambazo zimefikia Sh bilioni 9.3,” alisema.

Alipendekeza VAT, tozo za Tanroads na michango ya njia ya reli kwa ajili vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya umeme zisamehewe  kulipunguzia shirika mzigo.

Alisema changamoto nyingine   ni ulipaji wa fidia kwa wakati hasa katika miradi ya kupitisha miundombinu ya njia za umeme ambako zinahitajika Sh bilioni 190.1.

Alisema kuna miradi ya njia kuu za umeme wa kilovoti 400 kutoka Kinyerezi – Chalinze – Segera – Tanga, msongo wa kilovoti 220 kutoka Bulyankulu – Geita – Nyakanazi – Lusumo na ule wa kilovoti 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga.

Mkurugenzi mkuu huyo aliiomba Serikali iangalie uwezekano wa kufidia serikali za vijiji kwa maeneo yasiyoendelezwa kwa kuyajengea miundombinu ya huduma za  jamii kama vile zahanati, shule, maji na barabara badala ya kuwalipa fedha taslimu.

JAPAN

Mwakilishi wa Balozi wa Japan, Hiroyuki Kubota, alisema nchi yake inaunga mkono sera ya Tanzania ya viwanda na Dira ya Tanzania ya mwaka 2025, ndiyo maana imekuwa ikishirikiana na serikali katika miradi mbalimbali katika sekta muhimu.

Alisema Japan inaamini kukiwa na uhakika wa umeme, utasaidia kutekeleza sera ya viwanda nchini na kuharakisha maendeleo ya uchumi katika kutoa huduma za  jamii.

“Mradi huu ni ishara ya ushirikiano kati ya Tanzania na Japan, umegharamiwa kwa ushirikiano wa nchi hizi, huku ukijumuisha wafadhili mbalimbali ikiwamo benki na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA),” alisema Kubota.

Alisema JICA  inashirikiana na Tanzania katika miradi muhimu kama vile kugharimia ujenzi wa barabara za juu katika eneo la Tazara na kujenga uwezo katika sekta mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles