Na ALOYCE NDELEIO
MBIO za kuonesha ukubwa katika Afrika zinafanyika kati ya mataifa mawili ya Asia yenye nguvu, China na India na kwa kiwango kikubwa Marekani haionekani popote.
Hali hiyo imeleta hamaki kwa Marekani ambapo Mwanazuoni David Andelman aliandika hivi karibuni akimtahadharisha Rais wa Marekani Donald Trump akisema, “Donald Trump chunga, wakati ukiwa huangalii China inaliiba hili bara kutoka kwako; India nayo haipo nyuma,”
Rais wa China, Xi Jinping na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi wote hivi karibuni wamefanya ziara Afrika kila mmoja akiipitia, katika ziara ‘binafsi ya kirafiki’.
Rais Trump hajaitembelea Afrika, wala hajatangaza mpango wa kufanya hivyo na hapo ndipo Andelman anasema, “Kwanini hatujali? China na India zinajali mno.”
Hata hivyo hivi karibuni Trump alimwalika Rais wa Kenya, Uhuru Kenyetta ambaye alizuru Marekani ambapo wawili hao walisaini mikataba baina ya nchi zao ukiwamo wa safari za anga za moja kwa moja kutoka New York hadi Nairobi.
Andelman akabainisha, “Kwa ujumla Afrika ndiyo makazi ya Nigeria na inatarajiwa kuwa nchi ya tatu duniani kwa idadi ya watu na changamoto zipo katika masuala ya ajira zaidi kwa idadi ya vijana inayoongezeka achilia mbali chakula na miundombinu.
“Lakini pia ni sehemu muhimu kimkakati kwani ndiko yalipo madini ya lanthanum, cerium and neodymium, ambayo ni muhimu kwa magari ya umeme ya baadaye.” |
Anasema alielezwa na Rais wa Benki ya Afrika, Akinwumi Adesina kwamba “kuna hektari milioni 400 za ardhi inayofaa kwa kilimo katika maeneo ya ukanda wa Savanna” ambayo “itapima hali ya baadaye ya chakula duniani”.
Haikushangaza Modi alitangaza katika hotuba yake katika Bunge la Uganda ikiwa ya kwanza kwa Waziri Mkuu wa India aliyepo madarakani, kwamba India itafungua balozi 18 mpya, “Kuimarisha ushirikiano wetu na kujikita katika upanuzi mkubwa Afrika”
Xi alikuja na pendekezo ambalo ni kubwa – ushiriki wa China katika mradi mkubwa wa maendeleo: mkakati wa Ukanda na Barabara, awali ukijumuisha eneo kubwa la ardhi na mkondo wa biashara kuvuka Ulaya na Asia na kupanua mtazamo kwa mapana zaidi. Tayari imeshatoa mkopo wa dola bilioni 94 kwa serikali za Afrika na makampuni yanayomilikiwa na serikali.
Lakini mikakati hii inayoongozwa na Wachina na msukumo huu katika Afrika umekuwa unaambatana na hatari na changamoto kubwa kwa Marekani na maslahi yake Afrika.
Kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), deni la umma kwa eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara limepanda kutoka asilimia 28.5 ya pato Ghafi la Ndani (GDP) kwa mwaka 2012 hadi asilimia 48 mwaka huu 2018, na kumaanisha sehemu kubwa ya kipato kitatumiwa kulipa madeni yake.
Kwa ujumla madai kwa deni hili ni rasilimali za asili kuanzia katika mafuta Nigeria na Angola hadi madini kadhaa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kimsingi ni muhimu kwa maeneo ya kimkakati-kijiografia kama Djibouti.
Papo hapo njia mbili za biashara kati ya Marekani na Afrika zimeporomoka kutoka takribani dola milioni 142 mwaka 2008 hadi dola milioni 55 mwaka jana 2017, ambapo kwa kiwango kikubwa inatokana na Marekani kuongeza kujitegemea katika nishati, kwa kuondoa hitaji la mafuta ghafi kutoka Afrika.
Wakati China na Marekani zinaendelea na vita kubwa kbiashara kuvuka Pasifiki, China inajikita yenyewe katika nchi moja baada ya nyingine Afrika hususani kwa faida na ikiwa kimya.