Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
MWENYEKITI wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia, ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha haki inatendeka katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa wakati akizungumza na watia nia 113 wa nafasi za ubunge kwa tiketi ya NCCR Mageuzi.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wabunge waliojiunga na chama hicho hivi karibuni wakitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao ni Joseph Selasini, Mbunge wa Rombo, Anthony Komu, Moshi Vijijini pamoja na wabunge wa viti naalum, Susan Massele na Joyce Sokombi.
“Tunahitaji Tume ya Uchaguzi itakayotenda haki, tunajua kuna wakurugenzi ambao ni makada, sisi kilio chetu ni haki itendeke, wahakikishe wanasimamia sheria na kanuni, hapa hatuzungumzii kijani tunazungumzia haki,” alisema.
Pia, alisema vyama vya siasa vinatakiwa kushindana kwa hoja na sio siasa za propaganda.
“Niombe sana vyama vishindane kwa hoja na sio propaganda za kuchafuana, hakuna siasa za kumtoa mtu ngeu wala propaganda. NCCR Mageuzi tumezaliwa upya,”alisema.
Vilevile Mbatia alitoa rai kwa Watanzania, kwamba wachagua wabunge na madiwani wanaotokana na NCCR Mageuzi kwani hakuna chama chenye haki miliki ya kuongoza.
“Tanzania ni yetu sote, hakuna mwenye haki miliki ya kuongoza. Ni zamu yetu kuongoza,”alisema.
Alisema kwa wananchi kuchagua wabunge na madiwani wanatoka NCCR, ana uhakika kilio chao cha kupata Katiba mpya kitasikilizwa.
“Niwapongeze wabunge kwa kuona NCCR Mageuzi ndio sehemu sahihi, nawaomba Rombo wamrudishe Selasin (Joseph) na mimi nitakuwepo katika kampeni.
“Kuna minong’ono ya ukabila, hili halipo kwetu na kuna kauli kwamba tunataka kufungua kanisa sio kweli, hakuna chama ambacho ni kiranja wa mwenzake hapa kwetu ndio kuna mageuzi ya ukweli na tunamtanguliza Mungu mbele,”alisema.
Alisema chama chake kimeamua kujenga jamii inayozingatia haki huku akidai kila Mtanzania ana wajibu wa kupata haki.