Dk Fredirick L Mashili, MD, PhD.
TUNAPOKARIBIA maadhimisho ya siku ya kisukari duniani, ni muhimu kujikumbusha vitu rahisi kabisa ambavyo kiukweli hupuuzwa. Mojawapo ya vitu hivyo ni mazoezi. Licha ya ukweli kwamba wengi wetu hatupendi kufanya mazoezi, tafiti zinaonesha kuwa kufanya mazoezi mara kwa mara kunaweza kukukinga na magonjwa zaidi ya kumi ikiwamo ugonjwa wa kisukari.
Katika makala hii tutajadili magonjwa, aina ya mazoezi na shahidi za kisayansi zinazoonyesha ukweli huo.
SARATANI, KISUKARI NA MAGONJWA MBALIMBALI YA MOYO
Mkusanyiko wa tafiti zaidi ya 40 zilizohusisha watu na nchi mbalimbali, ulibaini kwamba mazoezi huweza kuzuia magonjwa kama vile kisukari, magonjwa ya moyo na baadhi ya saratani. Imeonekana pia kwamba, tofauti na kutokuvuta sigara, kuwa mkakamavu kwa kufanya mazoezi mara kwa mara ni mtindo wa maisha wenye faida lukuki kwa afya zetu. Leo hii tunafahamu fika kwamba, mazoezi ni sehemu muhimu ya mpango mzima wa kujikinga na ugonjwa wa kisukari.
Hakikisha unafanya mazoezi ya aerobics (kutemba, kukimbia, kuogelea au kuruka kamba) kwa muda usiopungua nusu saa kwa siku, angalau mara tano kwa wiki. Usisahau pia kufanya mazoezi ya nguvu (kuvuta na kusukuma uzito) angalau mara mbili kwa wiki. Ni muhimu pia kufanya mazoezi ya kunyoosha na kulainisha viungo kila siku.
UGONJWA WA SONONA (DEPRESSION)
Katika utafiti uliojumuisha tafiti nyingi zilizofanyika katika pande mbalimbali duniani, ilionekana kwamba mazoezi huweza kuzuia na hata kutibu tatizo la sonona. Tafiti hizi zimebaini kwamba, pamoja na kuongeza vichocheo vya kibailojia vya furaha mwilini, kufanya mazoezi humpa mtu fursa ya kujumuika, hivyo kupata wasaa wa kushirikiana na wengine, kitu ambacho ni muhimu katika kutibu tatizo hili. Mazoezi pia husaidia katika kuzuia magonjwa ya kusahau (dementia) na kiharusi.
Hakikisha unafanya mazoezi katika vikundi au clubs. Jiunge na kikundi cha mchaka mchaka (jogging club) mtaani au katika mahali pako pa kazi. Mazozi ya aerobics yanapokuwa kama tabia, husaidia kuzuia na kutibu tatizo hili. Kumbuka kwamba, kufanya mazoezi kuwa tabia ni nguzo madhubuti katika kupambana na tatizo la sonona.
MADHARA YA AFYA YATOKANAYO NA UMRI MKUBWA
Inafahamika kisayansi kwamba umri unapoongezeka, uwezekano wa kupata magonjwa pia huongezeka. Hii husababisha watu wengi hata kuuchukulia uzee kama ugonjwa. Matatizo ya kiafya yanayotokana na umri mkubwa ni pamoja na kuumwa mgongo na magoti, mifupa kuvunjika kiurahisi na hata magonjwa ya kisukari, moyo na saratani.
Tafiti zimethibitisha kisayansi uwezo wa mazoezi kupunguza kasi ya kuzeeka, na kuonyesha kwamba, watu waliowakakamavu huishi maisha marefu kuliko wale wanaoishi kibwanyeye. Kiukweli, kama kuna kipindi ambacho mazoezi ni muhimu, ni pale ambapo umri wetu unaposogea. Katika kipindi hiki mazoezi yanatakiwa kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku.
Zingatia kufanya mazoezi ya aerobics na yale ya nguvu kwa pamoja. Mazoezi ya kunyoosha na kulainisha viungo pia ni muhimu kama yalivyo mazoezi yakuimarisha uwiano wa mwili au body balance. Mazoezi ya kuimarisha balance ni muhimu sana katika kipindi cha uzee, kwani wazee huathirika sana na tatizo la kuanguka mara kwa mara ambalo husababishwa na kukosa uwiano (balance). Mazoezi ya nguvu (resistance exercises) ni muhimu sana katika kipindi hiki. Hii inatokana na ukweli kwamba aina hii ya mazoezi huimarisha nguvu ya misuli na mifupa na kuzuia kuanguka anguka ambako huwapata wazee wengi.
SARATANI YA UKUTA WA MJI WA UZAZI (ENDOMETRIAL CANCER)
Katika utafiti uliohusisha takribani wanawake 1400 ilibanika kwamba, kufanya mazoezi kwa saa 150 kwa wiki (wastani wa nusu saa kwa siku) kuliweza kuzuia uwezekano wa kupata saratani ya ukuta wa mji wa uzazi kwa zaidi ya asilimia 30.
Kutokana na faida zake katika kudhibiti tatizo la unene uliokithiri (obesity), mazoezi yanaweza pia kuzuia saratani ya matiti na ile ya utumbo mkubwa. Kwa ujumla mazoezi yanayo sehemu kubwa katika kuzuia saratani mbalimbali.
Kama ilivyoshauriwa hapo juu, fanya mazoezi ya aerobics angalau mara tano kwa wiki, kwa muda usiopungua dakika 30 kwa siku. Usisahau kufanya mazoezi ya nguvu angalau mara mbili kwa wiki. Kumbuka, mazoezi si kwenda gym au kushiriki michezo pekee. Kutembea, kukimbia kupanda ngazi na hata kuendesha baiskeli ni mazoezi tosha.