29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

KENYA KINARA UTENGENEZAJI DAWA ZA BINADAMU AFRIKA MASHARIKI

Na Said Ameir, MAELEZO


KUWAPATIA wananchi dawa zenye viwango bora, salama na ufanisi ni moja kati ya malengo makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuimarisha afya za watu.

Pamoja na lengo hilo, utekelezaji wake mbali ya kukabiliwa na chagamoto za kibajeti, changamoto nyingine kubwa ni upungufu wa wataalamu wa ukaguzi na kudhibiti ubora na usalama wa dawa.

Kwa mujibu wa takwimu za miaka ya hivi karibuni, soko la dawa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki linategemea bidhaa hiyo kutoka nje kwa kati ya asilimia 70 na 75 hivyo uzalishaji wa ndani ni kati ya asilimia 30 na 25.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Ulisubisya Mpoki anasema Tanzania huagiza nje ya nchi asilimia 80 ya mahitaji yake ya dawa.

Nchi nyingine zinazoagiza dawa nje ya nchi ni Rwanda asilimia 90, Uganda asilimia 90, Burundi asilimia 100, Zanzibar asilimia 100 na Sudan Kusini asilimia 100.

Katika nchi wanachama wa Jumuiya hii, ni Kenya pekee ambayo imepiga hatua katika utengenezaji dawa ambapo takwimu zinaonesha kuwa inatengeneza karibu asilimia 25 ya mahitaji ya soko la nchi wanachama.

Mbali ya Jumuiya kuwa na mpango maalumu wa muda mrefu kuwezesha nchi wanachama kutengeneza zaidi dawa kuliko kutegemea watengenezaji wa nchi za nje, lakini pia imeweka mkazo katika kuwapatia uwezo na ujuzi  wa udhibiti na ukaguzi wa viwango vya ubora na usalama wa dawa wataalamu wa nchi wanachama.

Mkakati wa Jumuiya katika kujenga uwezo wa wataalamu wa nchi wanachama umejikita katika kuhakikisha dawa zinazotengenezwa katika nchi wanachama na zile zinazoingizwa toka nchi za nje zinakidhi viwango vya ubora unaotakiwa.

Nchi hizo zimekubaliana kuwianisha viwango vya dawa ili dawa zinazotengenezwa na kuingizwa katika Jumuiya ziwe na viwango vinavyofanana ubora, usalama na ufanisi.

Hivi karibuni, Jumuiya hiyo kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shule ya Famasi ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi za Afya Muhimbili (MUHAS) waliendesha mafunzo maalumu kwa wataalamu wa udhibiti na ukaguzi wa dawa kutoka nchi wanachama.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Kituo Mahsusi cha Kanda cha Ukaguzi na Udhibiti wa Dawa kwa Afrika Mashariki, kilichopo Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi ya Afya, Muhimbili yaliendeshwa kwa pamoja na wataalamu wa TFDA, MUHAS, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na mtaalamu mbobefu kutoka Bodi ya Dawa ya Uholanzi.

Kituo hicho kilianzishwa mwaka 2014 na kuanza shughuli zake mwaka 2015 na kinaendeshwa kwa pamoja kati Jumuiya ya Afrika Mashariki, TFDA na Shule ya Phamasi ya Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili.

Mafunzo hayo ni ya pili tangu kuanzishwa kwa kituo hicho ambapo mafunzo ya kwanza yalifanyika mara tu kilipoanza kufanya kazi mwaka 2015.

Ni vyema kubainisha kuwa katika programu ya uwianishaji wa dawa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, TFDA ndio taasisi kiongozi ya uratibu na usajili dawa. Hii inadhihirisha uwezo mkubwa wa kitaalamu na kitaasisi ilionao TFDA katika masuala hayo katika nchi wanachama wa jumuiya.

Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo anaeleza kuwa moja ya majukumu ya mamlaka za udhibiti wa dawa katika nchi wanachama ni kufanya tathmini ya dawa kabla hazijaingia katika soko kuhakikisha kuwa zinakidhi viwango vya ubora, usalama na ufanisi vilivyokubalika kisheria.

“Mafunzo haya ni sehemu ya uwezeshaji wa utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka za Udhibiti na Usimamizi wa Dawa katika nchi zetu, pia ni sehemu ya mpango wa uwianishaji  wa dawa wa jumuiya ili kujenga uwezo kwenye ngazi ya nchi za ukanda huu  kwa kufanya tathmini ya maombi ya usajili wa bidhaa za dawa,” anafafanua Sillo.

Akizungumzia tathmini ya mafunzo hayo, Mratibu wa Mafunzo Mhadhiri Mwandamizi na Meneja wa Maabara ya Utafiti na Maendeleo, Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili, Profesa Eliangiringa Kaale anasema yana umuhimu mkubwa katika kulinda afya ya wananchi wa Jumuia ya Afrika Mashariki.

Kama takwimu za uingizaji dawa katika nchi wanachama zinavyoonesha, ni vyema kueleza kuwa kiwango hicho kikubwa cha dawa kinachoagizwa kutoka nje kinalazimu nchi wanachama kushirikiana kwa karibu kwa sheria, kanuni na viwango vinavyofanana ili ukanda wote uwe salama katika suala la dawa.

Kama inavyoeleweka biashara ya dawa na vifaa tiba ni moja kati ya biashara inayonyemelewa na kushamiri kwa udanganyifu, hivyo ushirikiano wa karibu ni kitu muhimu katika udhibiti. Ukaguzi wa mipakani na ukaguzi wa mara kwa mara kwenye soko ndio utakaowalinda wananchi.

Zaidi, uwezo mkubwa wa kitaalamu, rasilimali na kimiundombinu ndio silaha madhubuti kukabiliana na udanganyifu huo ambao Jumiya imekuwa ikichukua hatua kuimarisha uwezo wa wananchama wake wa usimamizi, ukaguzi na kudhibiti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles