Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD.
INAFAHAMIKA kwamba mazoezi ni mojawapo ya vitu muhimu kwa afya zetu. Na njia mojawapo ambayo mazoezi hutusaidia kulinda afya zetu ni kwa kuzuia magonjwa mbalimbali kama vile kiharusi (stroke). Leo tutajadili matokeo ya tafiti mbalimbali zilizothibitisha uwezo wa mazoezi kuzuia tatizo la kiharusi.
Katika utafiti mkubwa uliofanyika nchini Marekani, ambapo watu 27,000 wasiokuwa na kiharusi walifuatiliwa kwa muda wa takribani miaka sita, ilionekana wazi kwamba mazoezi yana uwezo mkubwa wa kupunguza uwezekano wa kupata tatizo la kiharusi.
Washiriki katika utafiti huu waliripoti kiasi cha mazoezi ambayo hufanya katika maisha yao ya kawaida na kuwekwa katika makundi matatu. Kundi la kwanza ni wale wasiofanya mazoezi kabisa, la pili ni wale waliofanya mazoezi kidogo mpaka ya wastani (mara moja mpaka tatu kwa wiki) na kundi la tatu ni wale waliofanya mazoezi sana (mara nne na zaidi kwa wiki). Watu hawa walifuatiliwa kwa muda wa miaka sita.
Matokeo ya utafiti huu mkubwa yalionyesha kwamba asilimia 33 (wastani wa watu wa tatu katika kila watu kumi, au watu 30 katika kila watu 100) ya washiriki, hawakuwa wanafanya mazoezi, na kundi hili ndilo lililoathirika na tatizo la kiharusi zaidi. Utafiti huu ulionyesha pia kwamba, wanaume waliofanya mazoezi sana (zaidi ya mara nne kwa wiki) ndiyo walionusurika zaidi na kupata kiharusi.
Hii inamaanisha kwamba kama wewe ni mwanamume unatakiwa kufanya mazoezi sana (zaidi ya mara nne kwa wiki) ili kujikinga zaidi na kiharusi. Uhusiano huu kati ya kufanya mazoezi sana na kiharusi haukuonekana kwa wanawake–ikimaanisha kwamba hata mazoezi kiasi cha wastani yanaweza kumkinga mwanamke na tatizo la kiharusi.
Utafiti huu ni mojawapo tu ya tafiti chungunzima zilizoonyesha uwezo wa mazoezi katika kuzuia tatizo la kiharusi. Ziko tafiti zingine zilizofanyika nchini Denmark, Canada na uchina ambazo pia zimeonyesha faida hizo za mazoezi. Tafiti nyingine zilizofanyika katika makundi madogo ya watu zimeonyesha kwamba mazoezi yanayohusisha kupumzika kidogo wakati wa mazoezi (interval training) yanafaida zaidi katika kuzuia tatizo hili la kiharusi. Interval training (IT) huruhusu moyo, mapafu na misuli kufanyakazi kubwa kwa muda mfupi na kasha kupata ahueni kidogo kabla ya kuendelea na zoezi.
Fuata utaratibu ufuatao kufanya interval training
- Pasha mwili moto kwa kutembea, kuruka au kukimbia mchakamchaka kwa dakika kama tatu
- Fanya mazoezi kwa kasi kubwa (iwe kukimbia au kuruka kamba) kiasi cha kufanya kasi ya kupumua na mapigo ya moyo kuongezeka sana. Fanya hivi kwa sekunde 30. Unatakiwa kufanya kwa kasi kiasi kwamba usingeweza kuendelea zaidi ya hizo sekunde 30.
- Punguza kasi kwa sekunde 90 (wakati huu unakuwa unatembea taratibu).
- Rudia mzunguko huu mara saba.
Kwa kufanya hivyo utakuwa umefanya interval training na kupata faida lukuki katika mwili wako. Ikumbukwe kwamba Shirika la Afya Duniani linashauri kufanya mazoezi ya kiwango cha kati na cha juu kwa muda usiopungua nusu saa, angalau mara tano kwa wiki.