LONDON, UINGEREZA
WAZIRI Mkuu wa Uingereza, , amesema hataogopa kuwa mkweli kwa Rais Donald Trump wa Marekani iwapo rais huyo atatoa matamshi yasiyokubalika.
May alisema haya wakati akijiandaa kukutana na Trump Ijumaa ijayo na baada ya maandamano makubwa yaliyofanywa na wanawake jijini London na kwingineko duniani kupinga mtizamo wa Trump dhidi ya wanawake juzi.
Baada ya kura ya kujiondoa Umoja wa Ulaya mwaka jana, Uingereza imekuwa ikiangazia namna inavyoweza kuboresha uhusiano na Marekani na mataifa mengine yaliyo nje ya umoja huo, ili kudhihirisha kwamba hatua yake hiyo haijaathiri ushirikiano na nchi nyingine.
Inaelezwa kuwa mazungumzo kati ya wawili hao yatakuwa ni fursa muhimu kwa May ambaye tangu mwanzo ameonekana kujenga uhusiano mzuri na watu wa karibu na Trump.
Kwa mujibu wa May, watatumia pia fursa hiyo kujadili mpango wa biashara huria na umuhimu wa Jumuiya ya Kujihami ya Magharibi (NATO).