24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Mawaziri wazidi kutumbua majipu

magufuliNA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KASI ya utendaji kazi wa mawaziri wa Rais Dk. John Magufuli, imezidi kukolea baada ya mawaziri wawili kwa nyakati tofauti kuwasimamisha kazi vigogo walio chini yao kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Uamuzi wa kwanza umechukuliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ambaye jana alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohamed Kilongo kwa kushindwa kutimiza wajibu kazini.

Waziri Maghembe, amechukua uamuzi huo, baada ya Kilongo kuhusishwa na tuhuma za uzembe wa ukusanyaji wa fedha za Serikali zinazotokana na maliasili  (maduhuli) kwa zaidi ya miaka 11 katika ngazi ya wilaya zilizokusanywa tangu 2004.

Waziri  mwingine aliyechukua uamuzi huo, ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba ambaye amewafukuza kazi wakurugenzi wote wa Bodi ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa kushindwa kukamilisha ujenzi wa mradi wa majengo ya machinjio ya kisasa yaliyoanza mwaka 2010.

WAZIRI MAGHEMBE

Waziri Maghembe alitangaza uamuzi huo, wakati wa kikao chake na wafanyakazi wa wizara hiyo, ambapo alimwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi kusimamia uchunguzi huo wa tuhuma hizo mara moja.

“Idara ya Misitu, ina uwezo wa kukusanya kiasi kikubwa cha fedha, kwa mfano tunaweza kukusanya Sh trilioni 5 hadi 10 katika msitu mmoja kama tutasimamia vizuri.

“Lakini wapo watu wanatumia mwanya wa udhaifu uliopo katika ugawaji wa leseni kula fedha za Serikali, wanazikusanya, zinaishia mifukoni mwao tangu 2004 hadi leo, maduhuli hayajapelekwa benki.

“Ninashangaa ‘Internal Orditors’ mpo hapa ndani… mnafanya nini? Watu wanakusanya fedha huko  hawazileti serikalini. Katibu mkuu naomba simamia suala hili tuchukue hatua kali za kinidhami,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Maghembe ameagiza maofisa misitu wa wilaya zote kukabidhi vitabu vyote vya maduhuli kwenye ofisi za kanda za wizara hiyo ndani ya siku 10 ili vikaguliwe kujua kiasi cha fedha kilichopaswa kuingizwa serikalini tangu 2004 hadi sasa.

“Kama watashindwa kuwasilisha vitabu hivi kwa ukaguzi ndani ya siku hizo, tutawachukulia hatua za kisheria kwa sababu haiwezekani tuwe na vichaka vya ulaji namna hii,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Maghembe alishangazwa na  uongozi wa TFS kuacha kutumia ofisi zao zilizopo wizarani na kuamua kwenda kupanga kwenye jengo la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa gharama kubwa.

Alisema amekerwa na jambo hilo na kutoa siku saba wafanyakazi wote wa TFS kurudi wizarani na vifaa vyao.

“Wakati tulipokuwa tunajenga hapa, tuliamua kupaita nyumba ya mpingo ‘Mpingo House,’ tukimaanisha jengo la misitu, jambo la ajabu wanakaa wanyamapori pekee, ninyi wa misitu mkaamua kuhama.

“Yaani mmetoka kwenye jengo la Serikali mnakwenda kupanga… hii nini maana yake, nani aliwashauri jambo hilo, nataka hadi Jumatatu ijayo mrudi na uchunguzi ufanyike kujua kwanini mkurugenzi alihama na kuisababishia hasara Serikali kwa kitendo hiki,” alisema.

WAVAMIZI

Profesa Maghembe alionekana kukerwa na wimbi la wananchi kuvamia hifadhi za misitu na kuwataka watu wote waliovamia hifadhi  hizo kuondoka wenyewe ndani ya miezi mitatu kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Watu wanavamia hifadhi za misitu ovyo ovyo, kwa mfano pale Tabora wamejenga kwenye hifadhi na wengine wanasema wamepewa vibali  na maofisa wa misitu wa eneo husika.

“Sijui kama eneo hili limekosa sifa ya uhifadhi, tunachunguza jambo hilo kubaini ukweli na tutawachukulia hatua maofisa watakaobainika.

“Nimepata taarifa, hata mbuga zilizoko Kigoma, Katavi na Kagera kuna uvamizi na watu wanatoka hadi nje ya nchi, waanze kuondoka wenyewe, vinginevyo tutaanza kuchukua hatua za kisheria kuwaondoa,” alisema.

Aliwaagiza maofisa wa idara ya misitu kuipitia upya ripoti ya tathmini juu ya hali ya uvunaji wa magogo ya mwaka 2007 ambayo iliibua bandari bubu 32 zinazojihusika na usafirishaji wa magogo nje ya nchi kinyume cha sheria.

“Wakati nikiwa katika wizara hii, tulifanya tathmini mwaka 2007 ambayo iliibua bandari bubu 32, kuna wizi  mkubwa wa magogo nchini. Sheria inasema magogo hayatakiwi kusafirisha nje ya nchi zaidi ya samani zilizotengenezwa kwa kutumia magogo hayo,” alisema.

Alisema kuanzia sasa Idara ya Nyuki itaanza kujitegemea kwa kuitenganisha na ile ya misitu ili kuiongezea ufanisi wa utendaji kazi wake.

“Kuna changamoto ya ukataji wa miti kwa matumizi ya nishati ya mkaa, naagiza watu wapewe vibali kwa kufanya shughuli hii ili walipe ushuru stahiki, na tuanze kufikiria kutumia njia mbadala ya makaa ya mawe ili tuokoe misitu yetu,” alisema.

MWIGULU NCHEMBA

Naye Waziri Nchemba amewatimua kazi wakurugenzi wote wa Bodi ya NARCO pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Ranchi za Taifa…..kwa kushindwa kukamilisha ujenzi wa mradi wa majengo ya machinjio ya kisasa yaliyoanza mwaka 2010.

Alichukua uamuzi juzi, baada ya kufanya ziara ya siku moja aliyotembelea ranchi ya Taifa ya Ruvu na kubaini ubadhirifu wa Sh bilioni 5.7 zilizokuwa zimetolewa kwa ujenzi huo.

Alisema mradi huo umetelekezwa tangu mwaka 2010, bila kuendelezwa na hakuna sababu za msingi zinazotolewa na viongozi.

Alisema kibaya zaidi bodi hiyo imeshindwa kazi, lakini inapendekeza kujengwa mradi mwingine kama huo ndani ya eneo hilo hilo.

Aliagiza vyombo vya sheria kuhakikisha vinawachukulia hatua wahusika wote walioshiriki ama kwa makusudi au kwa njia yoyote kuhujumu mradi huo.

Pia amewaagiza wataalamu wa wizara yake, kuhakikisha ndani ya wiki moja wanampelekea ripoti ya thamani ya jengo lililojengwa na fedha zinazotakiwa kumalizia ujenzi wa jengo hilo.

MWAKYEMBE NA KATIBA MPYA

Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ameahidi  kuwa Serikali itamalizia kiporo cha Katiba inayopendekezwa iliyoachwa na Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Dk. Mwakyembe aliyasema hayo alipofanya ya ziara ya kutembelea ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), mjini Dar es Salaam jana.

Alisema watahakikisha Katiba inapatikana kama Rais Magufuli alivyoahidi. “Hakuna mtu ambaye yuko juu ya Rais wa nchi, kauli aliyoitoa ya kumalizia kiporo cha Katiba pendekezwa pale ilipoishia, ndiyo itakayofanyiwa kazi,” alisema Dk. Mwakyembe.

MAHAKAMA YA MAFISADI

Kuhusu Mahakama Maalum ya Mafisadi iliyoahidiwa na Rais Dk. Magufuli wakati wa kampeni, Dk Mwakyembe alisema ahadi hiyo itakamilishwa ndani ya mwaka huu.

“Mahakama ya mafisadi iliyoahidiwa na Rais Magufuli inashughulikiwa, naamini itakuwa tayari hata kabla ya kumalizika  mwaka huu,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema anasikitishwa na namna ambavyo vyombo vya utoaji wa haki kama polisi, mahakama, mawakili, mahakimu, majaji na wakuu wa magereza wanavyotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa.

“Vyombo vya utoaji wa haki vilianza kuota vijipu tangu enzi za awamu ya kwanza, sasa yamekuwa majipu  inabidi yakamuliwe kabla Dk. Magufuli hajaingilia kati kuyatumbua bila ganzi,” alisema Mwakyembe.

SHABANI MATUTU, VERONICA ROMWALD  NA ESTHER MNYIKA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles