29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE UKAWA AZUIA BOMOABOMOA DAR

bomoa*Mahakama kuu yaipiga ‘stop’ serikali

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

MBUNGE wa Jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF), pamoja na wenzake wamefanikiwa kuwaokoa wananchi waliokuwa katika simanzi, baada ya Mahahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kuzuia bomoabomoa ya nyumba.

Katika uamuzi huo uliotolewa jijini Dar es Salaam jana, mahakama hiyo imezuia kwa muda ubomoaji wa nyumba 681, zilizojengwa katika maeneo ya mabondeni katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo imetokana na maombi yaliyowasilishwa na wadai saba waliokuwa wakiwawakilisha wenzao 674 wanaopinga kubomolewa nyumba zao.

Wadaiwa katika maombi hayo ni Manispaa ya Kinondoni, Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Jaji Panterine Kente, akitoa uamuzi huo jana alisema mahakama imeridhika kwamba shauri la msingi halijafunguliwa, lakini kuna watu wanastahili kusikilizwa kupitia waombaji wachache.

Alisema ili kuwasilikiliza waombaji hao mahakama inatoa zuio la muda kwa waliofungua kesi ambao ni jumla ya wenye nyumba 681.

“Mahakama inazuia kwa muda ubomoaji wa nyumba hizo hadi maombi namba 822 yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

“Mawakili wa wadai mnatakiwa kuwasilisha mahakamani majina ya wenye nyumba 681, anuani zao na mahali zilipo nyumba hizo ili kurahisisha utekelezaji wa amri ya mahakama,” alisema Jaji Kente.

Jaji Kente aliitaka Serikali iendelee na zoezi la kutambua na kuweka alama za X ikibidi kubomoa nyumba za watu wengine ambao hawahusiki katika shauri hilo.

Jaji huyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza usikilizwaji wa maombi ya watu saba wanaotaka kuwawakilisha wenzao 674, katika kesi ya kuzuia ubomoaji wa nyumba hizo.

Wadai hao saba juzi waliwasilisha maombi ya msingi wakiitaka mahakama hiyo iwape kibali cha uwakilishi wa kupinga ubomoaji wa nyumba hizo.

Kabla ya maombi hayo kusikilizwa na kutolewa uamuzi , mawakili hao akiwemo Abubakari Salim, waliwasilisha ombi la kuitaka mahakama itoe amri ya muda ya kuwataka wadaiwa katika shauri hilo kusitisha ubomoaji na hali ibaki kama ilivyo sasa.

Wakili wa Serikali Gabriel Malata, alipinga maombi hayo na kudai kwamba wadaiwa hao hawana haki ya kuomba mahakama itoe amri ya kusitisha ubomoaji kwa kuwa bado hawajapewa kibali cha kufungua kesi ya msingi na kwamba mahakama haiwezi kutoa kibali kwa watu ambao hawatambuliki.

MBUNGE 

Zoezi la bomoabomoa lililokuwa linafanyika katika maeneo ya mabondeni katika jiji la Dar es salaam, lilichukua sura mpya  baada ya Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia kuliwekea pingamizi mahakamani.

Mbunge huyo anawakilisha mwamvuliwa wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao unaundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Hapo awali zoezi hilo la bomoabomoa lilianzia katika Bonde la Mti Msimbazi eneo la Mkwajuni jijini Dar es salaam likiwa limelenga kubomoa nyumba zaidi ya 5,000 zilizopo katika maeneo ya mabondeni.

Baada ya ubomoaji huo kuanza na zaidi ya nyumba 150 kubomolewa, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitangaza kusimamisha zoezi hilo  kwa muda wa siku 14, huku akiwataka wananchi kubomoa nyumba zao wenyewe kabla ya Januari 5, mwaka huu.

Kabla ya Lukuvi kusimamisha ubomoaji, Mtulia alipeleka pingamizi mahakamani kuzuia zoezi hilo ili kuwapa wananchi hao muda wa kujiandaa.

Mtulia alisema ana imani na Serikali ya awamu ya tano kuwa ni sikivu na itatenda haki kwa wananchi walioko mabondeni kwa kuwapatia muda, huku ikiangalia jinsi gani itawasaidia makazi.

NYUMBA  ZABOLEWA

Hata hivyo mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wamekosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa  jana.

Wakazi waliokumbwa na bomoabomoa hiyo ni wa maeneo ya Mkwajuni, Hananasif hadi Salender.

Hatua ya kuendelea kubomoa nyumba hizo imekuja siku 15 baada Lukuvi na na  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba kusimamisha kwa muda zoezi la ubomoaji.

Katika tamko lake hilo Waziri Lukuvi alitangazia wakazi hao kuwa zoezi hilo lingendelea Januari 5 mwaka huu ambapo MTANZANIA ilifika katika maeneo hayo na kushudia baadhi ya wananchi wakihamisha vitu vyao na wengine wakibomoa nyumba zao badala ya kusubiri kazi hiyo kufanywa na buldoza.

Ilipofika majira ya saa tano asubuhi  magari iana Catapillar maarufu kama ‘Tingatinga’ yalianza kazi ya kuvunja nyumba hizo.

Wakati zoezi hilo likiendelea baadhi ya wananchi walikuwa wakilalamika kuwa wamevunjwa kimakosa kwa kuwa wana vielelezo vya umiliki.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wananchi hao, Mwajuma Abdallah, alisema nyumba yake iliwekwa alama ya X kimakosa, hali iliyowafanya waanze kuvunja wenyewe, lakini walipofika wabomoaji hawakugusa eneo hilo, hali iliyowafanya wapate hasara.

Naye Hashimu Mwinyimkuu alisema kuwa waliambiwa kuwa watavunjiwa nyumba Januari 5, mwaka huu hivyo kwa kuwa hawana uwezo wa kukataa wametii amri  kwa kuanza kuondoa vitu vyao.

“Tuliambiwa kuwa tunakuja kuvunjiwa leo, ki msingi hatuna la kufanya hadi sasa hatujui tunaenda wapi kama unavyoona watu wengi wanafamilia kubwa, kiukweli hatuna la kufanya mpaka sasa,” alisema.

Mwathirika mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Janeth Mushi, aliilalamikia hatua ya Serikali kwa kuwaonea wanyonge na kuwanyanyasa kama wakimbizi.

“Sasa tumekuwa kama wakimbizi, watoto wanahangaika hawajala kutoka asubuhi hawaendi shule na sisi tunashindwa kufanya shughuli zetu za kutuingizia kipato kwa kuhangaikia pa kujisitiri na kulinda mali zetu zisiibiwe”, alisema.

Kwa upande wake Ofisa Mazingira Mwandamizi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Anold Kisiraga, alisema ni vyema wananchi wakakubaliana na agizo la Serikali la kuwataka wahame katika mabonde.

Kwa mujibu wa tathmini walioifanya kwa kukishirikiana na Wizara ya Ardhi walitegemea kuvunja nyumba 8,000 lakini mpaka sasa nyumba ambazo zitavunjwa ni zaidi ya nyumba 15,000 pamoja na zile zilizopigwa alama ya X.

Alisema tatizo la mafuriko linachangiwa na ujengaji wa maeneo ya bondeni kwa kuwa kunakuwa na shughuli ambazo zinaendelea kama uchimbaji wa mchanga na kutupa takataka ambazo mvua zikinyesha huziba mitaro.

Akizungumza bila kutaka jina lake kutajwa mfanyakazi aliyekuwepo eneo la tukio kutoka Wizara ya Ardhi alisema kuwa asilimia 90 wananchi waliojenga katika bonde hilo waliamua kuvunja nyumba zao wenyewe.

“ Wengi wameamua kutii na zoezi hili mwaka huu litakuwa rahisi sana hatutaacha kuvunja mpaka tumalize wananchi waelewe lengo la kuvunja nyumba hizo ili kuepuka majanga yanayoweza kutokea baadae” alisema.

Uwekaji X waendelea

Wakati uamuzi wa mahakama ukitolewa jana mchana, maofisa wa Baraza la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na wenzao wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, jana waliendelea na uwekaji wa alama ya X katika nyumba zilizojengwa katika Bonde la Mto Msimbazi ambapo nyumba zaidi ya 5000 ziliwekwa alama hiyo tayari kwa kuvunjwa.

Uwekaji huo ulianzia katika eneo la Tabata Matumbi na kumalizikia mtaa wa mogo Kata ya Kipawa huku upande wa pili wa mto huo ukimalizikia katika eneo la Daraja la Mbao la Segerea.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi hilo, Ofisa Mipango wa Manispaa ya Ilala, Alfred Mbyopyo, alisema zoezi hilo limezingatia maagizo yote yaliyotolewa na Serikali.

“Kwa leo pekee (jana), tumefanikiwa kuzifikia nyumba 5,346 na kutufanya kufikisha nyumba zaidi ya 10,000 kwa Manispaa ya Ilala pekee,” alisema Mbyopyo.

Alisema zoezi hilo limeendeshwa katika maeneo ya Tabata Matumbi, Vingunguti, Kiembe Mbuzi, Karakata na Kipawa huku upande wa pili wakijikita katika eneo la Tabata.

Aidha alisema kuna malalamiko machache ambayo yamejitokeza katika maeneo ya Mchikichini ambapo nyumba nyingi zilizowekewa alama ya X kuwa na hati ambazo zinatambulika.

“Kutakuwa na uhakiki baadaye kujiridhisha kama sheria ya ardhi imezingatiwa kikamilifu katika maeneo tuliyoyaweka alama hiyo,” alisema Mbyopyo.

POLISI WAPUNGUA

Katika hatua nyingine idadi ya askari polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) jana ilipungua kutokana na kutokuwepo upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi wa maeneo hayo.

Mmoja wa maaskari waliokuwa katika msafara huo ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema idadi hiyo imepunguzwa kutoka askari 90 hadi 60.

“Idadi yetu leo imepungua kutokana na upinzani kutoka kwa wakazi wa maeneo haya kupungua na pia kuna wenzetu wamekwenda katika bomoabomoa inayoendelea Mkwajuni,” alisema askari huyo.

Habari hii imeandaliwa na Kulwa Mzee,  Tunu Nassor, Grace Shitundu na Mauli Muyenjwa (DAR ES SALAAM)

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles