26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAZIRI WA JPM WAFUKUZA, WASIMAMISHA WAFANYAKAZI

Na WAANDISHI WETU

-MBEYA/IRINGA

MAWAZIRI wawili wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, jana walifanya uamuzi mgumu wa kufukuza na kuwasimamisha baadhi ya watendaji ndani ya wizara zao.

Wakati Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akivunja Bodi ya Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori Idodi na Pawaga (MBOMIPA), Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amewasimamisha kazi watumishi wanne wa Idara ya Forodha katika mpaka wa Tanzania na Zambia, mjini Tunduma.

Mbali na kuvunja Bodi ya MBOMIPA kwa tuhuma za ufisadi, Prof, Maghembe pia amevunja mikataba yote ambayo bodi hiyo ilikuwa imekwisha ingia na wawekezaji mbalimbali.

Prof. Maghembe pia ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kuanza uchunguzi wake na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuhusika na ufisadi katika jumuiya hiyo.

Alichukua uamuzi huo wakati wa ziara yake katika jumuiya ya MBOMIPA na kufanya mkutano na wajumbe wa bodi kabla ya kuivunja.

Alisema kuwa anashangazwa kuona MBOMIPA inajiendesha kwa hasara na kuomba kwa wahisani fedha za kujiendesha wakati kimsingi asasi hiyo ilipaswa kuwa msaada mkubwa kwa wanachama wao ambao ni vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.

“Hii ni aibu kubwa kwa chombo hiki ambacho kinapaswa kuwa msaada kwa jamii, chenyewe kimegeuka kuwa ombaomba. Hivi inawezekana vipi MBOMIPA kuomba hadi msaada wa sare na matairi mawili kwa wahisani? Hili ni jambo la aibu, kifupi halikubaliki… hakuna cha mwekezaji hapa wala cha bodi, tunaanza upya, vitu vyote tunaanza sifuri,” alisema Prof. Maghembe.

Katika hatua nyingine, waziri huyo ameagiza askari wa vijiji wa wanyamapori (VGS) ambao wanajihusisha na ujangili kukamatwa mara moja.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alimweleza waziri huyo kuwa MBOMIPA ni moja kati ya asasi ambazo zimekuwa zikimsumbua na ndiyo maana siku zote alikuwa hachoki kumtafuta na kumwomba kuingilia kati kutafuta ufumbuzi wake.

“Kazi hii nitaisimamia  mwenyewe na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, kama itatushinda basi tutakuwa tumeshindwa kumsaidia Rais Dk. John Magufuli na sitakubali kushindwa na naagiza wote wanaotakiwa kuondoka waondoke wenyewe,” alisema.

Mjumbe wa Kamati ya MBOMIPA, Vicent Kibiki, alimpongeza Waziri Maghembe kwa hatua alizochukua na kudai kuwa shida kubwa ni wanasiasa – madiwani na wenyeviti wa vijiji kuvuruga jumuiya hiyo.

Diwani wa Kata ya Idodi, Onesmo Mtatifikolo, alikanusha tuhuma dhidi yao akisema hazina ukweli kwani wao huingia katika mkutano mkuu mmoja ambao wanapokea taarifa za jumuiya hiyo na kupitia wao wameweza kuvunja mkataba mmoja baada ya kushinda kesi mahakamani, hivyo alidai wao kazi yao ni kuinusuru jumuiya hiyo.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Dk. Christopher Timbuka, alisema kuyumba kwa taasisi hiyo ni pigo kwa hifadhi hiyo, hivyo lazima chombo hicho kuwa imara zaidi na uamuzi wa waziri utasaidia uhifadhi na kukomesha ujangili.

 

Dk. Mpango

Kwa upande wake, Waziri Dk. Mpango aliwasimamisha kazi watumishi wanne wa Idara ya Forodha, katika mpaka wa Tunduma kupisha uchunguzi wa madai ya rushwa dhidi yao na kuhusishwa na upotevu wa lakiri 10 zinazotumika kufunga kwenye shehena ya mizigo inayopita mpakani hapo kutoka nje ya nchi.

Dk. Mpango aliwataja watumishi hao kuwa ni Harrison Mwampashi, John Makorere, Stephene Josia na Frank Kessy na kuviagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama mpakani hapo vinawahoji kuhusu tuhuma hizo.

Watumishi hao wanadaiwa kuiba lakiri hizo kutoka ofisi za TRA – Tunduma wanakofanyia kazi, na kwamba nne kati ya hizo zilikutwa zimefungwa kwenye mizigo ya malori yanayoshikiliwa katika mpaka huo baada ya uchunguzi kufanyika, huku malori mengine matano yakizuiwa baada ya kuonekana yana lakiri zilizochezewa.

Taarifa zaidi zinadai kuwa baada ya uchunguzi, mawakala ama wamiliki wa malori hayo wamedai kwamba walipewa lakiri hizo na watuhumiwa na kwamba uchunguzi zaidi umebaini kuwa kiwango cha mizigo kilichomo katika makontena yaliyobeba mizigo ya magogo na kufungwa lakiri hizo za wizi, hakilingani na idadi ya mizigo iliyoko katika nyaraka.

Kwamba jambo hilo linaashiria kuwa wanazitumia lakiri hizo kudanganya idadi na uzito wa mizigo yao ili kukwepa ushuru na kodi mbalimbali za Serikali.

“Hakuna kitu muhimu kama uadilifu kwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato na hatutasita wala hatutamwonea aibu mtu yeyote, tutachukua hatua kwa mujibu wa sheria ili kulinda fedha za umma,” alisema Dk. Mpango.

Alisema kuwa Serikali imebaini baadhi ya watumishi wa TRA na idara za forodha mipakani wanashirikiana na wafanyabishara wasio waaminifu kuingilia mifumo ya kukusanyia mapato, kitendo ambacho kinaweza kurudisha nyuma juhudi za Serikali kuwahudumia wananchi.

Aliwataka wafanyakazi wote wa forodha na Mamlaka ya Mapato, kuwa wazalendo na waaminifu katika kukusanya mapato ya Serikali na kuacha kujihusisha na vitendo vinavyokwaza ufanisi wa mamlaka hayo.

Wakati huo huo, Dk. Mpango, ametoa muda wa siku 30 kwa wanaobadilisha fedha za kigeni kiholela mipakani, waache mara moja, badala yake waheshimu sheria za nchi na kuunda vikundi vinavyoweza kuanzisha maduka ya kubadilisha fedha hizo.

Pia ametoa muda wa siku ishirini kwa wamiliki wote wa vituo vya mafuta ambao wameomba kupatiwa mashine za kielektroniki kuunganishwa na mfumo wa kodi na utoaji wa risiti wawe wamepata mashine hizo vinginevyo watafungiwa vituo vyao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles